April 17, 2017



Kesho Jumanne Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inatarajiwa kukutana kwa ajili ya kupitia mambo mbalimbali yaliyowasilishwa hivi karibuni kwa kamati hiyo kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na rufaa ya Kagera Sugar iliyoikata baada ya maamuzi ya Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania (Kamati ya Saa 72) ya kuipoka timu hiyo pointi tatu na mabao matatu kutokana na kosa la kumchezesha beki Mohamed Fakhi dhidi ya Simba huku akidaiwa kuwa na kadi tatu za njano. 

Jambo jingine litakalojadiliwa hiyo kesho na kamati hiyo ni malalamiko ya Yanga dhidi ya Afican Lyon ambayo Desemba 23, mwaka jana iliikatia rufaa timu hiyo kwa kumchezesha mchezaji wa zamani wa Mbao FC, Venance Ludovick wakati usajili wake ukidaiwa kutokidhi vigezo na rufaa hiyo majibu yake hayakuwahi kuwekwa wazi tangu kipindi hicho.

Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya TFF zimedai kuwa, suala hilo linawapasua vichwa viongozi wa shirikisho hilo kutokana na wao kujichanganya hapo awali kwa kushindwa kulishughulikia kabla ya mchezaji huyo kuanza kuitumikia African Lyon akitokea Mbao FC.


“Jambo hilo linawaumiza sana vichwa TFF na hawajui nini cha kufanya baada ya kujichanganya hapo awali.


“Mbao walimwekea pingamizi wakidai kuwa ni mchezaji wao baada ya kusajiliwa na African Lyon lakini TFF wakachukulia poa tu na wakampatia leseni huku wakijua kabisa kuwa mchezaji huyo hana barua ya Mbao inayomuonyesha kuwa si mchezaji wao.


“Baada ya Yanga kumkatia rufaa ndipo waliposhtuka na kuamua kumsimamisha kimyakimya wakitumia kanuni ya 37 kifungu cha 13 kinachosema; “Mchezaji atakayebainika kutoa taarifa za uongo kufanikisha kuthibitishwa kwa usajili wake na kushiriki kucheza ligi kuu atafungiwa kwa kipindi cha miaka miwili na faini ya Sh 1,000,000. Matokeo ya michezo aliyocheza yatabaki kama yalivyotokea uwanjani,” kinasema chanzo chetu cha habari na kuongeza:


“Hata hivyo, ukiachana na kifungu hicho cha 13 cha kanuni hiyo, kifungu cha 14 kinasema kuwa; “Mchezaji atakayebainika kushiriki kucheza mchezo wa ligi kuu hali akijua kuwa hajathibitishwa kusajiliwa, atafungiwa kujihusisha na masuala ya mpira wa miguu kwa kipindi cha miezi 12 na faini Sh 500,000. Timu aliyoichezea itapoteza mchezo huo na timu pinzani itapewa ushindi.


“Kifungu hicho ndiyo kinawaumiza sasa TFF kwa sababu mchezaji huyo aliitumikia Lyon wakati usajili wake ulikuwa haujakamilika kutokana na wao kushindwa kulifanyia kazi pingamizi la Mbao FC, ndiyo maana suala hilo limechelewa kupatiwa ufumbuzi na hiyo kesho sijui itakuwaje kwani Yanga wao wamekikomalia kifungu cha 14 cha kanuni hiyo ya 37, wanataka wapewe pointi tatu,” kilisema chanzo hicho.

Aidha ishu ya Juma Nyosso kumdhalilisha straika wa Azam, John Bocco na kufungiwa kwa miaka miwili, inatarajiwa kujadiliwa pia kesho kufuatia beki huyo kuandika barua ya kuomba asamehewe baada ya kujutia kosa lake hilo na kudai kuwa amekuwa akiishi katika maisha magumu bila kazi.   


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic