April 1, 2017Na Saleh Ally
YANGA leo ni wenyeji wa Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja Taifa jijini Dar es Salaam, mechi ambayo mambo mengi yatatokea.

Pamoja na kwamba mengi yatatokea, yapo ambayo kwa asilimia kubwa hayatakwepeka kutokana na mechi yenyewe ilivyo, kumbuka Yanga ipo katika nafasi ya pili na pointi 53, Azam FC namba tatu ikiwa na pointi 44.

MOJA
Pamoja na Yanga kuandamwa na majeruhi wengi, bado Azam FC watataka kujaza viungo wengi wa ukabaji. Inawezekana kabisa Stephan Kingu, Himid Mao na Salum Abubakary ‘Sure Boy’ wakacheza chini. Lakini baadaye ataingia Mudathir Yahaya hasa kama Azam FC watakuwa wanaongoza, hii itaipa Yanga ugumu.

MBILI
Wachezaji watapaniki, hii inatokana na Yanga kuzitaka pointi tatu kwa nguvu kubwa. Lakini Azam FC wana mambo mengi ya kuthibitisha. Kwamba waliifunga Yanga mabao 4-0 Mapinduzi Cup, hawakubahatisha. Lakini Yanga watataka kushinda, hawatataka kucheleweshwa na kisaikolojia wanaamini Azam hawagombei ubingwa hivyo wanataka kuwatibulia tu dhidi ya Simba. Hii itafanya kuwe na jazba.

TATU
Kadi nyekundu inaweza kupatikana moja au mbili. Hii ni kutokana na presha lakini aina ya uchezaji wa timu hizi mbili.

 Kama Simon Msuva na Obrey Chirwa watakuwa katika kiwango kizuri leo, Kingu au Himid wanaweza kusababisha kadi nyekundu na wanapaswa kuwa makini kwa kuwa Chirwa na Msuva wana kasi na uwezo wa kunyumbulika.
Lakini kwa upande wa Yanga, angalia uchezaji wa mtu kama Ramadhani Singano ‘Messi’. Anakutana na Juma Abdul ambaye hayuko vizuri, hii ni hatari nyingine kwa Yanga na suala la kadi linaweza kutokea. Hivyo kadi nyekundu moja, mbili au sita hadi saba za njano, inawezekana kabisa.

NNE
Presha itakuwa kila sehemu hata kama Azam FC hawana uhakika wa kubeba kombe. Hii inaweza kusababisha mchecheto, yaani hali ya hofu kwa wachezaji wa kila upande.

Kuwa na hofu, kunaondoa utulivu na hii inaweza kuchangia kutokea kwa makosa ya kushangaza kabisa hasa kwa wachezaji upande wa ulinzi. Lakini kwa washambuliaji, huenda wakakosa mabao na kuwashangaza mashabiki kwa kuwa watakuwa wamepania kufunga na kumaliza kazi.

TANO
Kwa makocha, kila upande utakuwa na presha sana na huenda leo itakuwa siku ambayo George Lwandamina atawashangaza wengi hasa kama Azam FC itatangulia. Hatapumzika na huenda akawa na hofu kuu kwa kuwa mechi hii ni sehemu ya hukumu kwake hasa katika suala la ubora.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV