May 8, 2017
Na Saleh Ally
WAKATI Ligi Kuu Bara inakwenda ukingoni, mbio za wafungaji zinaonekana kuongozwa na wazawa ambao miaka mingi wanaonekana wamekuwa wasindikizaji.

Kuna baadhi ambao wamekuwa wakionyesha kujitutumua na wameendelea kuwa katika vita hiyo mfululizo bila ya kuchoka hata kama hawatakuwa wafungaji bora.

Angalau John Bocco wa Azam FC amekuwa akionyesha njia. Lakini hivi karibuni, ameonekana kupoteza mwelekeo katika ufungaji na huenda ile ishu ya kuandamwa na majeraha mfululizo imempoteza.

Simon Msuva anayecheza Yanga ndiyo yuko kwenye kizazi cha kukimbizana katika kuwania ufungaji bora. Msimu mmoja uliopita, alikuwa mfungaji bora na amekuwa akichuana vikali na Mrundi Amissi Tambwe ambaye ndani ya misimu minne ndiye anaonekana ni mshambulizi bora kabisa hasa unapozungumzia suala la kufunga mabao.

Ligi ya msimu huu ina radha nyingi sana na moja ambayo inavutia zaidi ni wale wanaochuana kuwania ufungaji bora.

Kwanza hauwezi kusema nani ataibuka mshindi hasa unamuona mshambulizi kama Tambwe anarejea katika kiwango chake mwishoni mwa ligi na sasa amefikisha mabao 10.

Tambwe ana uwezo wa kufunga hata mabao matano ndani ya mechi nne zilizobaki. Lakini bado unaona Tambwe na Obrey Chirwa raia wa Zambia, wamezungukwa na vijana wa Kitanzania wanaoonyesha pia wana uwezo mkubwa wa kucheka na nyavu.

Anayeongoza ni Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting akiwa na mabao 12 sawa na Msuva ambaye pia amekuwa akipambana kuibuka kuwa kinara.

Walio na mabao 11 ni Shiza Kichuya wa Simba na Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar ambayo imeonekana inapigania kupata nafasi ya tatu ikichuana na Azam FC.


Bocco hayupo mbali kwa kuwa ana mabao tisa baada ya kuwa amerejea na anaonyesha ana kiwango kizuri. Kama atatulia uwezo wa kufikisha mabao 12 anao.

Chirwa na Tambwe wamezungukwa na vijana wa Kitanzania na utaona si wale wanaotokea Yanga na Simba tu, wako kutoka katika timu mbalimbali na utaona zipo zile ambazo hata haziwanii ubingwa wa Bara.

Mfano Abdulrahman, timu yake inapambana kujiokoa ili isiteremke daraja. Lakini yeye ndiye anaongoza kwa ufungaji wa mabao, hili ni jambo zuri na vizuri kama atatupiwa macho kwa ajili ya kuendelezwa zaidi.

Hali kadhalika Mbaraka, naye timu yake haigombei kutwaa ubingwa. Lakini anapambana kuwa mfungaji bora na anaochuana nao wote ukiachana Abdulrahman na Bocco, waliobaki ni wale ambao timu zao zinazowania ubingwa.

Awali, ukiangalia listi ya wafungaji wanaowania ufungaji bora kwa asilimia 90, wanakuwa wanatokea Simba au Yanga na kama ikiteleza kidogo basi ni mchezaji kutoka Azam FC.

Mchezaji anayeweza kufunga mabao 10 akiwa Yanga. Hakika hawezi kuwa na nafasi nzuri ya ubora kama yule aliye Ruvu Shooting kwa maana ya viwango vya wachezaji ambao wangeweza kumsaidia.

Angalia Tambwe au Msuva wanaofunga mabao wakiwa wamezungukwa na nafasi nyingi zaidi za kuweza kufunga. Viungo kama Haruna Niyonzima na Thabani Kamusoko kwa Yanga au James Kotei na Said Ndemla na wengineo Simba.

Angalia mabeki, Juma Abdul, Hassan Kessy au Mwinyi Haji kwa Yanga au Besala Bokungu na Mohamed Zimbwe kwa Simba. Ni wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za ufungaji.

Kwa wale walio Kagera au Ruvu Shooting wanaweza kuwa na wachezaji bora lakini wanaokosa uzoefu au ubunifu wa juu kama wale walio Simba na Yanga ambao wanaongezewa ujuzi na makocha wa kigeni au wazoefu pia wakipewa hamasa ya juu na uongozi.

Kwa wachezaji ambao wanaonyesha njia, vizuri wakatupiwa macho ya hamasa ikiwezekana kuendelezwa zaidi kwa kuwa wanachoonyesha nyuma ya pazia kwamba ni wazi wanataka kushikwa mkono ili wafanye zaidi ya hapo. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV