May 26, 2017



Katibu mkuu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali, ameibuka na kusema kuwa alitambua mapema kuwa aliyekuwa mwenyekiti wa timu hiyo, Yusuf Manji atajiuzulu kwenye nafasi hiyo baada ya kusaini mkataba wa udhamini na Kampuni ya SportPesa huku akisisitiza kuwa hatakuwa tayari kwenda kumbembeleza arejee kwenye timu hiyo.


Manji ametangaza kujiuzulu katika nafasi ya mwenyekiti, Jumanne  ya wiki hii baada ya kuandika barua kwa makamu mwenyekiti wa timu hiyo, Clement Sanga, Bodi ya Udhamini na  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hali iliyowashtua mashabiki na wanachama wa  timu hiyo kwa kuwa hawakutarajia kiongozi huyo kuchukua maamuzi ya mtindo huo licha ya kufanikiwa kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara msimu huu.


Mzee Akilimali amesema kuwa kwa upande wake hakushtushwa na suala hilo kwa kuwa hakuna tajiri yeyote ulimwenguni anayependa kuwa chini ya mwenzake kwani kuondoka kwake anaamini kumechangiwa na kampuni hiyo ya michezo ya kubashiri.


“Binafsi suala hilo halikunishtua kabisa kwa sababu nilijua mapema litatokea, tangu siku ya kwanza tunasaini mkataba na SportPesa isipokuwa sikutaka kusema kitu kwa kuwa sikutaka matatizo kama yale yaliyojitokeza huko nyuma yajirudie maana nyumba yangu ilinusurika kutiwa moto ndiyo sababu nilikaa kimya.


“Ni sawa amesema ameomba kupumzika kwa kuwa ameshauriwa na madaktari hatuwezi kukataa hilo lakini naamini huu mkataba ndiyo chanzo kwani hakuna tajiri duniani ambaye anataka kuona anakuwa chini ya mwenzake na hata kama wataenda kumuomba kuendelea mimi sitaweza kufanya hivyo kwani litakuwa kosa kubwa sana kwangu,” alisema Mzee Akilimali.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic