May 15, 2017



Na Saleh Ally
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe ameamua kuachia ngazi katika nafasi hiyo na sasa atabaki kuwa mwanachama wa kawaida.

Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye amewahi kuwa mdhamini, mfadhili na hivi karibuni alitangaza kuingia katika mabadiliko kwa kutaka kununua hisa asilimia 51 za Klabu ya Simba, naye ameamua kukaa pembeni.

Kwa hali inavyokwenda, maana yake tunaweza kusikia na wengine tena wakiwa wamejiondoa katika uongozi au vinginevyo.

Wote hawa wawili wamekasirishwa na mchakato wa namna Kampuni ya SportPesa ilivyoingia mkataba na klabu yao jambo ambalo wanaona hawakutendewa haki na viongozi.

Kila mmoja anavyozungumza anaonyesha amekerwa na namna ambavyo mchakato ulipelekwa. Namna mambo yalivyokwenda na inaonekana viongozi walifanya siri hata dhidi ya viongozi wenzao.

Ukiwaangalia Mo na Hans Poppe utagundua kitu ambacho huenda hata wewe au mimi kingeweza kuwa kina uwezo wa kukukuta kama jambo hilo lingekutokea.

Wakati wa shida, watu walikufuata na kukuchukulia kama sehemu yao, mwokozi, mshauri na mpiganaji wao, lakini inapofikia wamepata neema, basi wanaona wewe si mwenzao tena.

Hans Poppe na Mo Dewji wanaamini wangeweza kuwashawishi SportPesa kutoa fedha nyingi zaidi za udhamini kuliko ambazo klabu imepata.

Inaonekana Rais Evans Aveva na wenzake wameamua kufanya mambo haraka kama walikuwa wanawakimbia wenzao, hawakutaka kuulizwa au walifanya hivyo kwa manufaa yao au wana faida ya pembeni.

Uamuzi waliouchukua Mo Dewji na Hans Poppe kujiweka kando. Wana haki kwa kuwa nao ni binadamu na wanastahili kufanya hivyo kwa mujibu wa hisia zao.

Kuna mambo kadhaa ya kufikiria, kujitoa kusaidia Simba huku ukibaki kuwa mwanachama nayo pia inaweza isisaidie sana. Vizuri kuwe na busara ya kulimaliza jambo hilo kwa njia za kujenga zaidi kuliko kujitenga.

Hakika ninawaelewa Hans Poppe na Mo Dewji, wanaona kuna hisia za usaliti kwa kuwa wamewekwa kando hasa baada ya wahusika kuona ni wakati wa neema tena, neema ambayo wawili hao wanaamini ingekuwa kubwa zaidi kama wangeshirikishwa.

Kwa nini Aveva na wenzake waliwakimbia wengine na Simba ikagawanyika wakati ndiyo inakwenda kupata neema? Hakika ni jambo la kujiuliza, kutafakari na mwisho kuamini kweli kuna tatizo ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi.

Hakuna anayeweza kumaliza matatizo ya Wanasimba isipokuwa ni Wanasimba wenyewe. Wanasimba ni pamoja na Mo Dewji na Hans Poppe.

Hakuna anayeweza kukataa kuwa Hans Poppe na Mo Dewji wamekosewa. Nafikiri ni hisia za kijeuri tu, zinaweza kupinga hili kwa kuamini hakuna kinachoshindikana hata fulani akiondoka kwa kuwa Simba ni kubwa.

Ukubwa wa Simba unatengenezwa na watu wenyewe ambao ndiyo akina Aveva, Mo Dewji, Hans Poppe na wengine. Raha zaidi ni watu wenye makampuni makubwa, maana yake wanaongoza watu wengi tayari.

Hivyo ni vizuri Simba kuwatumia na hasa kunapokuwa na mambo makubwa kama hayo kuliko kushirikisha watu ambao huenda wakawa si wazuri katika masuala yanayohusiana na ushindani wa soko kwa maana ya uendeshaji wa mambo.

Hans Poppe akikaa kando kama Mo Dewji, mwisho watakuwa wanaiumiza Simba na Wanasimba ambao wanawategemea kama askari wao.

Wamekosewa, waliowakosea wawe waungwana na kuzungumza maneno stahili na ikiwezekana kuwashawishi warejee.

Mo Dewji na Hans Poppe hakuna ambaye ameonyesha anaipinga SportPesa. Badala yake kila mmoja amechukizwa na mchakato ulioendeshwa na viongozi wenzake ambao anaona haukuwa uliijenga uaminifu na uwazi na badala yake uficho wa mambo tu.


Vizuri wakaonyesha busara, wakae pamoja na kulimaliza ili kuthibitisha ile kauli mbiu ya klabu ya “Simba Nguvu Moja.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic