May 5, 2017

Kocha wa zamani wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, ameibuka na kusema kuwa, anatamani kuiona Simba ikibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na kila siku amekuwa akiomba iwe hivyo.

Kerr ambaye aliinoa timu hiyo kuanzia Julai, mwaka juzi na kufungashiwa virago Januari, mwaka jana, kwa sasa anainoa timu ya Chesterfield ya nyumbani kwao inayoshiriki League Two ambayo ni ngazi ya nne katika mfumo wa ligi za England.

Muingereza huyo mwenye miaka 50 ambaye alikuwa beki wa kushoto wa Leeds United ya England, ameliambia gazeti hili: “Najua viongozi wa Simba kwa sasa wameshasahau mazuri mengi niliyoyafanya ndani ya klabu yao wakati nipo nafanya nao kazi.

“Bado naipenda Simba na ninawaombea waweze kuwa mabingwa wa ligi msimu huu, naona hilo linawezekana endapo wakiendelea kupambana, japo Yanga wanaonekana kupewa nafasi kubwa, lakini binafsi naamini Simba watakuwa mabingwa.”

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Simba inaongoza ikiwa na pointi 59 ikifuatiwa na Yanga yenye 56. Simba imebakiwa na mechi tatu, huku Yanga ikibakiwa nazo tano kabla ya kumalizika kwa msimu huu. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV