May 19, 2017

Na Saleh Ally
REAL Madrid wamebakiza uhitaji wa pointi moja pekee ambayo itawawezesha kuwa mabingwa wa La Liga, kombe ambalo limekuwa likiumiza vichwa vyao kwa muda sasa.


Madrid wana pointi 90 kileleni lakini Barcelona wana 87 na kila timu imebakiza mchezo mmoja tu. Kama Barcelona watashinda na Madrid wapoteze, basi watalikosa kombe kwa kuwa timu hiyo ya Catalunya ina pointi nyingi zaidi timu hizo zilipokutana msimu huu.

Kumbuka kwamba, baada ya kulingana pointi, kanuni za La Liga zinaangalia ‘head to head’, yaani mbabe zaidi kati ya timu mbili zinazowania ubingwa.

Madrid watacheza mechi ya mwisho dhidi ya Malaga wakiwa ugenini wakati Barcelona watabaki nyumbani kucheza na Eibar ambayo pia haina presha ya kuteremka daraja kama ilivyo kwa Malaga.Mechi ya Madrid inaonekana ni ngumu lakini ubora wa wachezaji wake kama Cristiano Ronaldo, Karim Benzema, Marco Asensio, Lucas Vazquez, Alvaro Moratta na wengine unaipa uhakika zaidi.

Katika wachezaji hao wa uhakika, ninamtupia jicho Marcelo Vieira Da Silva Junior, beki bora zaidi wa kushoto kuliko wengine wote duniani kwa kipindi hiki.

Wamewahi kutokea wengi lakini kipindi hiki ni “mali” ya Marcelo raia wa Brazil anayefanya vizuri zaidi katika kikosi cha Madrid akionekana kuwa na mchango mkubwa wa kupeleka makombe Santiago Bernabeu kama watakuwa makini katika mechi mbili tu za mwisho.

Madrid ikishinda dhidi ya Malaga pia dhidi ya Juventus ya Italia, itakuwa imebeba makombe mawili ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Marcelo ambaye ni beki “shavu” bora wa kushoto ni chaguo namba moja zaidi la Kocha Zinedine Zidane katika namba tatu na katika kikosi lakini sasa anakuwa beki anayeingia kwenye kundi la wachezaji nyota zaidi duniani.Heshima Uefa:
Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu, Marcelo amepewa na Uefa asilimia 83.6 za ubora wakati Cristiano Ronaldo ana 86.5 na Lionel Messi ana 81.4.
Hii inaonyesha kiasi gani Marcelo amekwenda kwenye ubora wa kufananishwa kiwango chake na washambulizi wenye kiwango cha juu kabisa.

Hii inamfanya kuwa ndiye beki wa kushoto mwenye thamani ya juu zaidi kuliko wengine wote kwa kipindi hiki.

Kwa wale ambao wamekuwa wakifuatilia soka katika kipindi cha miaka ya 1990 na mwanzoni mwa 2000, watamkumbuka Roberto Carlos ambaye pia alifanya vema zaidi akiwa na Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil kama ilivyo kwa Marcelo sasa.

Mechi za Presha:
Marcelo amekuwa ni nyota wa mchezo katika mechi nyingi kubwakubwa au zile zenye ushindani na presha kubwakubwa.

Kwa mwaka huu, alikuwa mchezaji bora wa mechi wakati Madrid ikiifunga Valencia kwa mabao 2-1, mechi ambayo Marcelo alifunga bao moja.Pia alikuwa mchezaji bora wa mechi wakati Real Madrid ikiitwanga Bayern Munich naye akionyesha uwezo mkubwa. Mechi ambayo itabaki kwenye kumbukumbu za wengi.

Katika msimu wa 2005-06 akiwa na Fluminence kwenye Ligi Kuu Brazil, Marcelo ambaye ni rafiki kipenzi wa Ronaldo katika kikosi cha Madrid, alifunga mabao 6 na kuzua mjadala mkubwa kama kweli alistahili kucheza kama beki au kiungo wa pembeni, yaani winga.

Kwa sasa ndiyo bunduki ya kushoto ya Kocha Zidane, mchezaji ambaye amekuwa akitumika kama kiungo wa pembeni na mfanya maamuzi wanapokutana na timu ina kiungo bora.

Kwa kuwa amekuwa akitaka kumtumia Marcelo kama ufunguo wa ushambulizi au kutuliza timu, Zidane amekuwa akilazimika kucheza kwa mifumo miwili tu.

Kwanza ni mfumo wa 4-4-2 ambao ameutumia katika mechi nyingi zaidi na 4-3-3 ambao ameutumia kama mfumo mbadala.

Ukiangalia mifumo yote hii miwili inaanza na watu nane au saba chini. 4-4-2 inakuwa na watu wanne katika ulinzi wanaoweza kusaidiwa na wengine wanne wakati 4-3-3 huu ni wanne wanaoweza kusaidiwa na watu.

Wingi wa watu nyuma, unampa nafasi nzuri Marcelo kujitawala na kufanya yake kwa usahihi. Kiasi fulani inashusha maksi zake katika ulinzi lakini inamfanya kuwa bora na beki hatari zaidi wa kushoto duniani.

Kila anapopanda, mfumo unaruhusu kufukia mapengo yake, naye amekuwa si muoga kwenda mbele na amefanya mambo yake kwa usahihi na kutimiza kinachotakiwa au zaidi.
Msimu huu, Madrid ikibeba La Liga, kwake itakuwa mara ya tatu, ikichukua Ligi ya Mabingwa, atakuwa kachukua mara ya tatu pia.

Marcelo ambaye ni shabiki wa Botafogo ya Brazil, kisoka alilelewa na babu yake aliyeitwa Pedro ambaye amekuwa akisema, yule ndiye aliyemtoa yeye zawadi kwenye mpira. Mara nyingi anasema: “Mimi ni zawadi ya babu katika mpira.”

Pedro ndiye alilipa fedha zake kumnunulia vifaa vya mpira hata nauli ya mazoezini na kila bao ambalo amefunga ametoa zawadi kwa mama na babu yake ambaye anasema kama si yeye, asingefika alipo. Pedro alifariki dunia Julai, 2014.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV