May 19, 2017Na Saleh Ally
MWAKANI Mungu akinijaalia uzima nitatimiza miaka 20 nikiwa rasmi mwandishi wa habari. Namshukuru Mungu kwa muda nimepita kwingi, nimeona mengi na nimejifunza mengi sana.

Katika hiyo miaka 19 niliyonayo leo, nimeandika mengi nikijua hayakuwafurahisha upande mmoja, yakawafurahisha upande mwingine na nikawa ninaendelea bila ya woga wala kuonea, leo niko hapa na nikijaaliwa uzima nataka kuendelea kujifunza zaidi.

Nimejifunza mengi lakini leo ningependa nizungumzie mojawapo hili linalowahusu wazee wa klabu hizi kongwe za Yanga na Simba. Hawa ni tegemeo la busara katika klabu hizi kwa kuwa baadhi yao wamekuwa viongozi na wanachama wa siku nyingi.

Kinachonishangaza, wengi wao wamekuwa wakijitokeza wakati wa kipindi cha matatizo tu au migogoro na mara nyingi mimi nimekuwa nikiona wanatumika vibaya.
Hii tabia haijaanza leo wala miaka mitano iliyopita, nimeikuta na naona inaendelea huku wazee wakiwa wamejifunika mwamvuli wa “heshima”. Kwamba kama utawasema kutaka kuwashauri au kuwakosoa, basi utaitwa hauna nidhamu.

Leo mimi naziba masikio, nawaambia ukweli kuwa wajifunze na ile methali isemayo; “Uzoefu ndiyo mama wa maarifa.”

Wao kama wazee wanategemewa kutokana na maarifa waliyonayo, maarifa ambayo wameyapata kupitia uzoefu wao ambao unaweza kuwa bora kuliko elimu ya digrii au zaidi na hasa ukitumika vizuri.

Wakiutumia vizuri uzoefu wao utakuwa na faida kubwa kwa klabu lakini kama watafanya kama ilivyokuwa juzi baadhi ya wazee wa Simba, basi wataendelea kujenga uadui na makundi ndani ya klabu zao.

Baadhi ya wazee wa Simba, waliita vyombo vya habari na kumshambulia Mohamed Dewji kwa maneno ya shombo ambayo mimi kamwe siwezi kuyaandika.

Walionekana wamelenga maisha binafsi, wakishangazwa na deni lake la Sh bilioni 1.4. Hakuna kiongozi hata mmoja wa Simba ametangaza kukataa au kulikanusha hilo deni, vipi wao wanalikana?

Lakini hawa viongozi, hawaonyeshi busara. Mimi nawachukulia kama watu wanaotumiwa na makundi ya watu kwenda kumponda mtu huyu na mwingine atachukua kundi la wazee wengine kumponda mtu mwingine.

Wanapaswa kukubali Simba ilikuwa na hali mbaya, wanajua wazi Mo Dewji alikuwa akitoa michango mingine ambayo si deni na inajulikana kwa wale waliokuwa wakiichangia timu au wasiochanga. Hivyo kuna sehemu yake ya kumshukuru badala ya kumkashifu kwa maneno ya kuudhi.

Anayedai chake si dhambi, viongozi kama wanalikataa hilo deni wazungumze. Lazima tukubaliane, anayekusaidia wakati wa shida hata kama ni mkopo huo ni msaada.

Katika vitu ambavyo ninaungana na wazee hao walichokisema ni suala la mchakato wa mabadiliko ya katiba. Hakika hili linapaswa kupita kwa njia sahihi ili kufika panapotakiwa kwa njia sahihi kabisa.

Anayekosea, wazee wanaweza kumrekebisha kwa maneno sahihi. Mfano hata wao wazee, mbona hawachangii kitu lakini wanavurumisha maneno ya kashfa kwa wanaochangia, hii si sahihi hata kidogo. Uzee isiwe ngao ya uonevu kwa wengine. Msiutumie vibaya uzee wenu.

Haitakuwa sahihi hata kidogo, badala ya kuzungumza mambo ya msingi. Au badala ya wazee kukemea yanayosababisha utengano ndani ya klabu, wao ndiyo wawe chanzo cha kusema maneno ya kashfa na kusababisha makundi.

Kuna ile methali: “Vijiti vingi pamoja, vigumu kuvunjika.” Viongozi wanapaswa kuwaunganisha Wanasimba badala ya kuangalia faida kwa maslahi yao binafsi au furaha ya muda tu kwa ajili ya kuwafurahisha watu fulani.

Simba ni ya wote, vijana na wazee na watoto pia kama ilivyo kwa Yanga. Sasa huu ni wakati wazee wakatuonyesha faida yao ili wathibitishe methali isemayo:

“Visima vya kale havifukiwi.”
 Kama watakuwa wanakwenda vizuri, watatuthibitishia kuwa haipaswi kuwafukia kwa kuwa wanahitajika. Hivyo waonyeshe busara na vizuri watafakari yale wanayozungumza mbele ya jamii kwa faida ya Simba.1 COMMENTS:

  1. Duh bora umewatolea uvivu.... Sijui kwa nini hawa wazee bado wana mawazo mgando... Kuleta migogoro ndio wanaona ni maendeleo.Mchakato wa kurekebisha vipengele vya sheria ulipitishwa kwenye mkutano wa wanachama kwa asilimia zaidi ya 95%....sasa hata 2% hawajafika wanataka kuanzisha vurugu.Hawana jipya waendelee kucheza zumna

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV