May 19, 2017







Na Mwandishi Maalum
Kampuni ya SportPesa ambayo ni mahususi kwa michezo ya kubashiri imeendelea kujizolea umaarufu mkubwa siku hadi siku barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Umaarufu huo wa kampuni ya SportPesa si tu kwamba umetokana na umahiri wake katika michezo ya kubashiri, lakini pia katika suala zima la maendeleo ya sekta ya michezo katika nchi zote ambazo kampuni hiyo imekuwa ikifanya shughuli zake.

SportPesa imeanza rasmi shughuli zake mnamo mwaka 2014 nchini Kenya na baada ya hapo imekuwa ikiendelea kutanua wigo wake katika nchi mbalimbali barani Afrika na duniani kote.

Tangu ilipoanza nchini Kenya, tumeshuhudia maendeleo makubwa katika tasnia ya michezo nchini humo. Tumesikia kama sio kushuhudia jinsi ambavyo kampuni hiyo imeingia mkataba na Shirikisho la Soka nchini Kenya la FKF, tumeshuhudia jinsi ambavyo kampuni hiyo imeweza kudhamini Ligi kuu ya soka nchini humo sambamba na vilabu kadhaa vya soka kama vile Gor Mahia, AFC Leopards, Ushuru FC na Nakuru All Stars.

Si tu kwa vilabu vikubwa, lakini pia tumeshuhudia SportPesa ikiweza kudhamini ligi mbalimbali za soka kuanzia ngazi ya chini kabisa ya mtaa na hadi leo tunavyoongea, juhudi zote hizo zimeweza kuzaa matunda na kuipandisha Kenya kwenye viwango vya ubora vya FIFA kutoka nafasi ya 135 hadi nafasi ya 75. 

Hakika ni mafanikio makubwa ambayo yameweza kupatikana ndani ya muda mfupi sana si tu kwa mchezo wa soka bali hata michezo mingine kama vile Ndondi, Mbio za magari na Raga ambayo SportPesa imeweza kuidhamini pia kwa nchini Kenya.

Tanzania
Baada ya kujiendesha kwa mafanikio makubwa nchini Kenya, Kampuni ya SportPesa iliona ulazima wa kutanua wigo wake kibiashara barani Afrika ambapo sasa waliamua kuingia rasmi nchini Tanzania ili kuendeleza hadithi ya mafanikio iliyoanzia nchini Kenya.

Siku ya Mei 9 kunako Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro iliyopo Kivukoni jijini Dar es Salaam, Kampuni ya SportPesa ilitambulisha ujio wake rasmi nchini Tanzania huku katika hotuba iliyotolewa na Mkurugenzi wa Utawala na utekelezaji wa kampuni hiyo Ndugu Abbas Tarimba, ikiweka wazi kuwa kampuni hiyo ya michezo ya kubashiri imekuja kuleta mageuzi makubwa katika tasnia ya michezo nchini.

Ikionyesha kuwa imejidhatiti katika kuanza utekelezaji wake mara moja, SportPesa ilianza kwa kutoa mchango wake wa Shilingi Milioni 50 ilizozikabidhi kwa Waziri wa Habari, Uatamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe ukiwa ni mahususi kwa ajili ya timu ya taifa ya soka ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys iliyokuwa ikijiandaa kwa ajili ya michuano ya vijana ya Afrika huko nchini Gabon.
Ulikuwa ni mwanzo mzuri katika kutambua mahitaji ya Tanzania hususani katika sekta nzima ya michezo ambayo kampuni hiyo ndiyo imejikita zaidi.


Udhamini wa Simba.
Baada ya kujitambulisha mbele ya umma wa watanzania, SportPesa ilianza kutekeleza ahadi zake moja kwa moja kwa kutangaza udhamini mnono kwa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam ambao ni mabingwa wa Tanzania bara mara 18.

Ikiwa ni klabu kongwe na yenye mafanikio makubwa nchini Tanzania, SportPesa iliona umuhimu wa kuingia makubaliano na klabu hiyo ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikiiwakilisha vyema Tanzania kwenye michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu.



Viongozi wa SportPesa wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Ndugu Pavel Slavkov sambamba na viongozi wenzao wa Simba wakiongozwa na Rais Evans Aveva, walitiliana saini mbele ya waandishi wa habari katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam siku ya Mei 12 ambayo Simba ilikuwa ikiumana na Stand United kwenye mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara.


Simba SC na SportPesa walisaini mkataba wa miaka mitano (5) wenye thamani ya zaidi ya Shilingi za Kitanzania Bilioni tano (5,000,000,000/= TZS) mkataba ambao utakuwa ukiongezeka kwa asilimia tano (5%) kila mwaka huku pia kukiwa na motisha kadha wa kadha endapo kama klabu hiyo itafanikiwa kunyakua ubingwa wa ligi (Nyongeza ya Shilingi milioni 100 za Kitanzania), Kombe la Kagame na Klabu bingwa/Shirikisho barani Afrika (Nyongeza ya Shilingi milioni 250 za Kitanzania).

Akizungumza baada ya kutia saini, Rais wa Simba, Ndugu Evans Aveva aliushukuru uongozi wa SportPesa kwa udhamini huo na kutoa ahadi ya kuhakikisha wanatekeleza matakwa ya mkataba huo.

“Nipende kuushukuru Uongozi wa SportPesa kwa kuona umuhimu kwa kuingia udhamini na klabu yetu ya Simba ikiwa ni katika adhma ya kuifanya klabu ya Simba kuwa na mafanikio. Kwakweli hii ni siku muhimu na ya kihistoria katika klabu yetu.

“SportPesa ni kampuni ambayo ina uzoefu mkubwa katika masuala ya udhamini wa soka kwani imeshafanya kazi na vilabu vingine vingine kama Arsenal na Southampton hivyo kwa uzoefu na ujuzi wao ambao wameuonyesha nchi nyingine kwa mifano iliyotukuka ni wazi kuwa tutanufaika vya kutosha”, alisisitiza Rais Aveva.



Udhamini wa Yanga
Siku chache baada ya kuingia makubaliano na klabu ya Simba, Kampuni ya SportPesa iliingia upande wa pili mitaa ya Twiga na Jangwani na kutangaza kuidhamini rasmi klabu ya Yanga ambao ni watani wa jadi wa klabu ya Simba.

Udhamini huo kwa Yanga ulikuwa ni muendelezo wa utekelezaji wa ahadi ya Kampuni hiyo ya kuleta mapinduzi ya soka nchini kupitia klabu hiyo ambayo ni ndio mabingwa wa kihistoria wa Tanzania bara wakiwa wameshanyakua taji la Ligi Kuu Bara mara 26 pamoja na kuiwakilisha vyema Tanzania kwenye michuano ya vilabu bingwa barani Afrika.

Viongozi wa SportPesa wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Ndugu Pavel Slavkov sambamba na viongozi wa Yanga wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Ndugu Clement Sanga, Katibu Mkuu Ndugu Charles Boniface Mkwasa na Ndugu Jabir Katumbi ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini walitia saini hati za makubaliano hayo kwenye hafla fupi iliyofanyika kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Jangwani jijini Dar es Salaam yakihudhuriwa na viongozi na wanachama mbalimbali wa klabu hiyo pamoja na waandishi wa habari.



Yanga SC na SportPesa walisainiana mkataba wa miaka mitano (5) wenye thamani ya zaidi Shilingi za Kitanzania Bilioni tano (5,000,000,000/= TZS) mkataba ambao utakuwa ukiongezeka kwa asilimia tano (5%) kila mwaka huku pia kukiwa na motisha kadha wa kadha endapo kama klabu hiyo itafanikiwa kunyakua ubingwa wa ligi (Nyongeza ya Shilingi milioni 100 za Kitanzania), Kombe la Kagame na Klabu bingwa/Shirikisho barani Afrika (Nyongeza ya Shilingi milioni 250 za Kitanzania) kama ilivyo kwa watani zao Simba.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Ndugu Clement Sanga aliushukuru uongozi wa SportPesa kwa udhamini huo na kutoa rai kwa wana Yanga kuungana kwa pamoja katika kuiunga mkono kampuni ya SportPesa.

“Kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Yanga na Mwenyekiti wangu Ndugu Yusuf Manji, napenda nianze kwa kutoa shukrani kwa kampuni ya SportPesa kwa kuona umuhimu wa kutusaidia na kuamua kufanya biashara pamoja na sisi.

 “Nipende kutoa rai kwa wanachama wenzangu wa Yanga kuhakikisha kuwa tunaheshimu mkataba huu mnono na pia tuunge mkono jitihada za SportPesa katika kuleta maendeleo ya michezo nchini”, alieleza Ndugu Clement Sanga.

Hizi ni dalili njema kwa vilabu hivi vikongwe nchini kwani kwa udhamini huu mnono, vitaweza kujiendesha kikamilifu hali ambayo itavinufaisha si tu vilabu hivyo, bali hata timu ya taifa ambayo inaundwa na wachezaji wengi kutoka vilabu hivyo viwili kama ambavyo anaeleza Ndugu Abbas Tarimba, Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa SportPesa. 

“Udhamini wetu kwa klabu za Simba na Yanga una lengo la kuziimarisha klabu hizi ili ziwe mfano wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini na kupelekea kuwa na timu bora ya taifa itakayoliletea sifa taifa kwa ujumla.” alisisitiza Ndugu Abbas Tarimba.

Uzoefu wa Kimataifa
Mbali na nchi za Kenya na Tanzania, SportPesa pia inaendesha shughuli zake nchini Uingereza, Afrika Kusini na Urusi ambapo tumeshuhudia ikiingia ushirika na vilabu mbalimbali vya Ligi Kuu nchini Uingereza kama vile Hull City, Southampton, Arsenal na hivi karibuni ikitangaza udhamini wake kwa klabu ya Everton ya nchini humo.

Sambamba na vilabu hivyo vya nchini Uingereza, SportPesa pia ina ushirika na Ligi kuu ya nchini Hispania maarufu kama La Liga ambapo washirika hawa kwa pamoja wataweza kulifaidisha soka la Tanzania kutokana na program za kubadilishana ujuzi miongoni mwa wataalam wa benchi la ufundi wa vilabu vyetu na vilabu washirika sambamba na kambi za mafunzo kwa wachezaji vijana kama ambavyo tumeona nchi ya Kenya ikinufaika kupitia ushirika huo.


Tuzo
Ni hivi majuzi tu, siku ya Alhamisi ya tarehe 18 mwezi huu ambapo kampuni ya SportPesa imepokea tuzo mbili huko jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini zijulikanazo kama Discovery Sports Industry Award (DSIA) ambazo ni mahususi kwa ajili ya kuwatunuku wanamichezo na makampuni yanayojihusisha na tasnia ya michezo kwa ujumla.
Nguli hao wa michezo ya kubashiri barani Afrika na duniani kote walitwaa tuzo mbili ikiwemo ya Udhamini bora kwa bara la Afrika kupitia udhamini wao wa michuano ya ngazi ya chini ya Super 8 iliyoanzishwa mwaka 2015 huko nchini Kenya sambamba na tuzo nyingine ya Kampeni bora ya kimichezo ya kiafrika kupitia kampeni yake maarufu ya “Made of Winners”
Huu ni uthibitisho tosha kwamba mchango wa kampuni ya SportPesa katika tasnia ya michezo unatambulika barani Afrika na duniani kote, hivyo ni jambo la kusubiri na kuona jinsi ambavyo kampuni hiyo imejipanga kuleta mapinduzi ya soka na sekta ya michezo kwa ujumla hapa nchini kama ambavyo imeahidi.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV