Mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) tayari umeanza, ambapo uchaguzi wenyewe utafanyika Agosti 12 mwaka huu mkoani Dodoma.
Hivyo nikiwa mmoja wa viongozi wanaomaliza muda wao katika Kamati ya Utendaji iliyopo sasa, ambayo iliingia madarakani Oktoba 2013, nimeona nipate fursa ya kuwashukuru tena wote walioniunga mkono hadi kufanikiwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF (nilishafanya hivyo baada ya kuchaguliwa), lakini leo kwa umuhimu wa pekee narudia kutoa shukrani zangu za dhati kwao.
Lakini pia niwashukuru wale ambao hawakuniunga mkono, lakini walikuja kuniunga mkono baadaye wakati wa kutekeleza majukumu yangu kwa namna mbalimbali. Pia niwashukuru wote ambao hawakuniunga mkono kabla ya uchaguzi na hata baada ya uchaguzi, walikuwa changamoto kwangu kuongeza ufanisi na kujirekebisha palipokuwa na udhaifu.
Kwa umuhimu wa pekee niwashukuru wafuatao:
(i)Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF: Sina neno la kuwaambia zaidi ya ahsante kwa imani yao kwangu na kunichagua kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji nikitokea Kanda ya Dar es Salaam.
(ii)Kamati ya Utendaji ya TFF chini ya Rais wa TFF Jamal Malinzi: Kamati hii ilinipa jukumu la kuongoza Kamati ya Ufundi kwa miaka minne iliyopita, lakini pia ilinipa heshima kwa kuwa Msimamizi wa Kituo cha Dar es Salaam.
(iii) Vyombo vya habari: Vilinipa ushirikiano mkubwa na kujihisi ni sehemu yao kuanzia waandishi wa habari za michezo hadi wahariri wa habari za michezo tulikuwa familia moja na tuliimba wimbo mmoja wa maendeleo ya soka nchini
(iv) TAFCA: Nilipata Ujumbe wa Mkutano Mkuu kupitia TAFCA, hivyo mchango wao kwangu ni mkubwa sana. Makocha wote niwashukuru kwa imani yenu kwangu.
(v) Wadau: Kila mmoja kwa nafasi yake kuanzia wachezaji, waamuzi, makamishna, viongozi mbalimbali wa soka,wadhamini wote wa soka waliopo nchini,wafanyakazi wa Wizara yenye dhamana ya michezo, vyombo vya ulinzi na usalama,watoa huduma wote Uwanja wa Taifa na wengineo ambao pengine nimesahau kuwataja, wajue nawathamini na kuwashukuru, wasichukulie kutowatambua ni kuwadharau.
(vi) Wafanyakazi wa TFF na Bodi ya Ligi: Nao nawashukuru na hakika ushirikiano wao hauna mfano.
(vii) Familia yangu: Naishukuru pia kwa kuniunga mkono na kuwa bega kwa bega nami, hasa pale nilipolazimika wakati mwingine kusafiri nje ya nchi au kufanya kazi katika muda ambao haukuwa rafiki kwa familia.
Uchaguzi wa Agosti 12:
Naomba niwajulishe wadau wangu wote hao kwamba mimi Kidao Wilfred sitagombea nafasi ya yoyote katika Uchaguzi Mkuu wa TFF utakaofanyika Agosti 12 mwaka huu.Hiyo maana yake ni kuwa sitatetea nafasi yangu ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, wala nafasi nyingine yoyote ya kuchaguliwa.
Naheshimu wajumbe wengi wa Mkutano Mkuu walioniomba kutetea nafasi yangu, hasa kwa kuzingatia nina sifa za kutosha kushika wadhifa huo, nikiwa nimecheza Ligi Kuu Tanzania Bara (kuanzia ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza) kwa miaka karibu nane, kocha kijana wa Ligi Kuu mwaka 2010.
Pia ni mhitimu wa kozi ya utawala na Menejimenti ya Soka, nikiwa na elimu ya ukocha Leseni A (Module 1) inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Level B niliyopata nchini Ujerumani, Mkufunzi wa makocha anayetambuliwa na CAF, Msomi wa Manunuzi na Ugavi nikiwa na Stashahada ya Uzamili katika Manunuzi na Taaluma ya juu ya Manunuzi CPSP(T).
Wajumbe waliona kwa sifa hizi na nyingine ambazo sijaziweka, bado mchango wangu unahitajika sana ndani ya Kamati ya Utendaji ya TFF, hususan kwenye maeneo ya Ufundi na ushauri juu ya taratibu za manunuzi nilipobobea.
Lakini baada ya kutafakari sana, niwaombe radhi ndugu zangu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, hasa wale waliosema wapo tayari kunipigia kampeni kwa hali na mali, kwamba sitagombea uongozi.Naamini wapo watakaoumizwa na hili, lakini yote ni kwa maslahi mapana ya mpira wetu.
Nimeona ni wakati muafaka wa kupata changamoto za kuusaidia mpira nje ya Kamati ya Utendaji ya TFF. Ninaweza kuwa sahihi au nikawa nimekosea lakini kuwa na uhuru wa kuamua ndio kitu ninachokipenda kwenye maisha yangu na sitaki kubadili hilo.
Najisikia fahari sana kwa miaka minne niliyokuwa mjumbe wa kamati ya Utendaji TFF dhamira yangu ya kuingia ndani ya vyombo vya maamuzi ilibakia na misingi ile ile na muda wote maslahi mapana ya soka ilikuwa kipaumbele changu kuliko utashi wangu binafsi.
Natoka huku nikiwa nimeonesha uthubutu wangu wa kusimamia mambo kwa weledi mkubwa, naamini wajumbe wenzangu ndani ya Kamati ya Utendaji na wadau wa soka kwa ujumla watakubali mchango wangu ndani ya vikao ulikuwa ni wa kijasiri, kiungwana, kifalsafa na usio wa kinafiki. Ni mchango ulioweka mbele maslahi ya Taifa kuliko yangu binafsi.
Mayo Angelou mwandishi mashuhuri wa mashairi wa Kimarekani alipata kusema: “Nimejifunza ya kwamba watu watasahau yale uliyosema, watasahau uliyofanya,, lakini kamwe hawatasahu nini uliwatendea wakaonekana walivyo leo.” Makocha wanaweza kuwa mashahidi wa hili.
Nimalizie kwa kusema kwamba miaka yangu minne ya kuwa TFF bila shaka kuna mambo ambayo sikuyafanya kwa usahihi, mimi ni binadamu, kiumbe dhaifu ambaye sijakamilika, maana aliyekamili huwa ni Mwenyezi Mungu pekee. Nawaomba radhi sana sana.
Mwisho niwaombee kila la heri wote wenye ndoto ya kuwania uongozi katika uchaguzi ujao, nikiamini nia ya mtu inajionesha si tu kwa yale anayoyasema, bali hata aliyoacha kusema.
Ahsanteni.
KIDAO WILFRED,
MJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI TFF,
(DAR ES SALAAM 2013-2017).
13.06.2017.
0 COMMENTS:
Post a Comment