July 22, 2017




Na Saleh Ally
UKIFUATILIA kumekuwa na gumzo kubwa kuhusiana na usajili wa Simba kwa ajili ya msimu mpya wa 2017-18 na kinachozungumzwa zaidi ni wingi wa wachezaji iliowasainisha.

Wachezaji wapya katika kikosi cha Simba wanafikia 12, kati yao wawili ni wa kimataifa ambao ni Emmanuel Okwi raia wa Uganda pia Haruna Niyonzima, Mnyarwanda ambaye amemaliza mkataba wake na Yanga.

Kwa upande wa wachezaji wazalendo ni 10 ambao ni kipa Aishi Manula kutoka Azam FC lakini kuna kipa mwingine Said Mohammed kutoka Mtibwa Sugar. Huyu alianza kutamba Majimaji, akatua Yanga kabla ya kuhamia Mtibwa.

Kama haitoshi, imemsajili kipa kutoka Mbao FC, huyu ni Emmanuel Mseja. Maana yake kikosi upande wa makipa kimevunjwa na kusajiliwa kipya kabisa.

Lakini Simba imewasajili pia mabeki zaidi ya watatu ambao ni Yusuph Mlipili (Toto), Jamal Mwambeleko (Mbao FC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Erasto Nyoni ambaye ameondoka Azam FC pia Shomari Kapombe.

Kwa washambulizi, unaanza na kiungo mshambuliaji ambaye ni Ally Shomari kutoka Mtibwa pia, halafu John Bocco aliyekuwa nahodha wa Azam FC.

Katika wachezaji wapya ambao Simba imesajili, mabeki ni watano na ukisema watu wa ulinzi imesajili nane. Utagundua kwamba Simba ilitaka kujiimarisha zaidi katika ulinzi ingawa unaweza kushangazwa kwa kuwa msimu uliopita, safu yake ya ulinzi ndiyo ilikuwa imara, ya pili baada ya Yanga.

Msimu uliopita, Simba ilifungwa mabao 17 ikiwa imefunga 50. Tena utaona ilizidi kuteleza katika mechi za mwisho kabisa za msimu. Kwa nini wameamua kuimarisha kikosi kwenye ulinzi kwa kufumua karibu kila sehemu?

Makipa watatu wote ni wapya, wameongeza mabeki wawili wa kati pia pembeni. Utapata jibu kwamba wameondoka makipa wawili, mmoja Simba wakiamua kumuondoa na Peter Manyika, baba yake Manyika Peter ameona hana nafasi ya kucheza, kaamua kumuondoa.

Katika ulinzi kwa beki wa kushoto Mohamed Zimbwe alipaswa kuongezwa mtu sababu Simba inaingia katika michuano ya kimataifa lakini Juuko Murshid amesisitiza anataka kuondoka na Abdi Banda ameishaondoka. Ilikuwa ni lazima kusajili zaidi katika ulinzi.

Kwa wachezaji kama Mlipili, hawana uzoefu na wanahitaji watu kama Mbonde na Nyoni. Kwa kifupi kunaweza kuwa na hesabu mbaya chache sana lakini zikawepo bora kwa asilimia ya juu.

Kwa upande wa viungo, Simba kumuongeza Niyonzima, hakuna anayeweza kupinga kwa kuwa wanahitaji pasi “zenye macho”, mtu wa kutuliza na kuubadili mchezo.
Wakati huo wamemsajili Okwi ambaye anaweza kubadili mchezo au kuongeza kasi ya mchezo na kujaza presha kwa timu pinzani ili waachie nafasi. Hakuna asiyemjua Okwi labda abadilike.

Kapombe labda kama ataandamwa na majeraha, akiwa fiti tunakubaliana anahitajika sana kwa kuwa Simba walimtumia Besala Bokungu ambaye hakuwa na kasi lakini aliutumia vizuri uzoefu wake. Lakini kama Kocha Joseph Omog atataka kutumia mashambulizi ya pembeni yanayoanzishwa na walinzi kama alivyofanya kwa Zimbwe Jr lazima kuwa na mtu kama Kapombe.

Mbele, kama kuna presha kama ya Okwi, Laudit Mavugo akafanya vizuri, halafu kuwe na krosi nzuri za Zimbwe, Kapombe, Kichuya basi Bocco atakuwa na nafasi nzuri ya kung’ara na kufanya vema.

Ukiangalia harakaharaka, unaweza kuona kama Simba wamekosea sana. Lakini hawako mbali na hesabu bora za usajili.

Pamoja na hivyo, mawili yanaweza kutokea. Kufanya vema au kuangushwa na mambo hayo mawili. Moja ni uendeshaji, maana wana wachezaji wapya ambao wanahitaji kuunganishwa na morali, uongozi lazima uwahudumie vizuri na kuwa na subira.

Pili wachezaji wenyewe, kama wataunganika kwa ajili ya kufanya kazi na kuweka malengo ya mafanikio yatakayoongozwa na upendo, watafanya kweli. Hapa pia wanahitajika kuunganisha “damu” yao mpya na ile ya zamani kufanya timu moja. Wasipofanya hivyo, watafeli na wanaodai Simba imesajili timu nzima leo, kesho watakuwa na hoja.

Lakini kwa Kocha Omog, lazima avumiliwe. Kama idadi kubwa ya wachezaji imeingizwa kwenye timu, wigo wa kupanga upya mambo utakuwa mkubwa lakini utahitaji muda. Hivyo asitupiwe mawe mapema kwa kisingizio kasajiliwa wachezaji “wazuri sana”.



1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic