July 21, 2017




Na Saleh Ally
HIKI ndiyo kipindi chenye presha kubwa kwa wachezaji na makocha wengi wanaozitumikia klabu mbalimbali hasa zile za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Huenda presha hiyo inaweza kufanana na wachezaji wa nje ingawa wao wana bahati ya kuona mipango inavyopita kwa utaratibu sahihi na mfumo uliokamilika na usio na mabonde yanayoweza kusababisha machungu yasiyo na sababu za msingi.

Acha mchezaji au kocha anayeachwa na timu awe na machungu ya kuondoka au vinginevyo lakini si kufanyiwa dharau au figisu, jambo ambalo si sahihi hata kidogo.
Kwa Ulaya au kwingineko ambako soka limeendelea, mchezaji atakuwa na uchungu kwa kuwa klabu inayomuacha, hakutaka kuiacha lakini anakuwa hana ujanja, afanye nini.

Lakini katika suala la taarifa kuwa ataachwa, stahiki zake atapata na kadhalika. Wenzetu wanajiweza na wamejipanga kwa suala la mambo kwenda kwa mpangilio ndiyo maana ulimwengu mzima ulishangazwa na uamuzi wa Kocha Mkuu Chelsea, Antonio Conte kumuandikia mshambuliaji wake, Diego Costa kwamba hana mpango naye.

Jambo hilo lilionekana ni jambo la ajabu kwa kuwa si kawaida kuonekana mambo yanakwenda kwa kuripua namba hiyo. Kwa kifupi, Conte alionekana kufanya mambo “Kiswahili” wakati huku limekuwa ni jambo la kawaida kabisa kufanya hivyo!

Nitatolea mfano mmoja, Kocha wa makipa wa Simba, Iddi Salim raia wa Kenya amekuja nchini kujiunga na kikosi hicho baada ya mapumziko akakuta tayari kuna kocha mpya.

Salim hakuwa amepewa taarifa, mwisho ameona makipa wakifundishwa na kocha mwingine na inaelezwa ni Mohamed Mwarami, kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars.

Safari ya Afrika Kusini ambako Simba imekwenda kuweka kambi, ameenguliwa. Hivyo amebaki Dar es Salaam akihangaika na viongozi na taarifa zilizotufikia kwenye dawati letu wamekuwa wakimzungusha kama pia.

Huyu anamueleza hivi, mwingine anamuambia hivi. Kaimu Makamu Rais wa Simba kasema hivi, Kaimu Rais wa Simba naye kamueleza vile na kiongozi mmoja kazungumza naye hivi.

Swali linakuja, kuna ugumu gani kumueleza mipango mipya ya Simba ni hii; baada ya hapo mnapitia mkataba katika ya pande mbili, kama ni malipo yanafanyika, unavunjwa na kila mmoja anachukua hamsini zake.

Mkataba huwa una faida gani sasa? Kama kila unapofikia wakati wa kuachana kwa pande mbili unakuwa hauheshimiwi na upande mwingine ambao ni wa unyonge unanyanyasika?

Tumeona mara kadhaa klabu za Tanzania na hasa hizi kongwe za Yanga na Simba zikilazimika kuwalipa wachezaji au makocha kadhaa. Hii ni baada ya kuwa wameshindwa kufuata yale ambayo yanakuwa ndani ya mikataba yao.

Ukiachana na hivyo, mchezo wa soka ni wa kuzunguka. Kocha huyohuyo anaweza kurudi siku nyingine, anaweza kuisaidia timu kupata wachezaji wapya huko mbele. Kwani inaweza kufikia yeye akawa balozi wa klabu ya Simba popote aendapo. Hii itakuwa hivyo kama mambo yalikwenda kwa kufuata utaratibu mzuri.

Sasa kuanza kumzungusha, jiulize sababu ni ipi? Mmefanya naye kazi msimu mzima, tena aliondoka na akakubali kurejea. 

Mwisho atakwenda kuzungumza na vyombo vya habari na kama ilivyo kawaida ya viongozi wa mpira mtaanza kuwanunia waandishi, kumtuma mtu wenu wa habari akanushe ukweli jambo ambalo naona ni kupoteza muda tu.

Onyesheni uungwani, nyie ni wanadamu, basi onyesheni thamani ya uanadamu. Kama imefikia wakati mnasitisha kufanya kazi na mtu, malizaneni naye vizuri na kila mmoja aendelee na maisha yake kwa amani.

Tuache tabia za “Kiswahili” katika sehemu ambayo mambo yanawezekana kuwa rahisi au yanayoweza kupita katika njia sahihi.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic