July 28, 2017



Na Saleh Ally
NAZIDI kuelekeza hisia za wazi kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa lengo la kuwashauri na kuwashawishi viongozi wanaowania uongozi kwa mambo kadhaa ninayoyaamini.

Kuna mambo kadhaa yanaendelea ya chinichini ambayo ninaamini zitakuwa ni kampeni za kimyakimya, kila mmoja akiwa amejipanga kuhakikisha anafanikiwa kuwashawishi wapiga kura.

Najua kuna siku tano rasmi za kampeni ambazo zimepangwa na kamati ya uchaguzi chini ya Mwenyekiti Revocatus Kuuli. Lakini siku hizo tano hazitoshi na kila mmoja anajua. Hivyo, wagombea wataendelea kufanya yao kimyakimya hadi siku hizo maalum za kuzungumza hadharani zitakapowadia.

Huenda siku tano za kuzungumza hadharani zitakuwa ni kama kumalizia lakini kila mgombea atakuwa anapita kuwashawishi wapiga kura kimyakimya kwa kuwa wao ndiyo waamuzi wa mambo.

Nataka kuzungumza na pande zote mbili. Wapiga kura na wagombea wenyewe, kwamba kwa lolote lile wajue wako kwa ajili ya kuusaidia mpira wa Tanzania ambao kupitia uongozi tofauti ndani ya Chama cha Soka Tanzania (Fat), baadaye TFF, tumeuminya kutokana na sababu nyingi sana.

Unagombea TFF, ujue kuna madeni kutoka kwa wapenda mpira. Unampigia kura mgombea, nakukumbusha isiwe matakwa yanayofurahisha nafsi yake kwa maana ya kutaka kujifaidisha, tafadhali hakikisha wanaoingia watakuwa na uwezo wa kulipa madeni mengi ambayo uongozi uliopita na uliopita na ule mwingine ulishindwa kuyalipa au kuyafanyia kazi.

Yako mengi ambayo yalikuwa chanzo cha kukwama kwa mpira wetu na mimi nitataja haya machache ambayo nimejifunza kupitia uongozi uliopita na ule uliopita.

Viwango duni:
Tunajua soka letu limekuwa na viwango duni kwa kuwa viongozi waliokuwa madarakani, nguvu zao waliwekeza katika mambo yao binafsi au matumbo yao.
Hawa wanaoingia, wanakuja kuinua kiwango. Kuisaidia timu ya taifa na zile za wanawake na vijana ili kuzidi kupandisha viwango vikiwemo vile vya Fifa. Tukiingia ndani ya 100, ni soko kubwa duniani. Hili lipewe kibaumbele kwa wagombea, wapiga kura angalieni watu sahihi.

Viwanja vibovu:
Viwanja vimechangia kushusha viwango, TFF haikuisimamia vizuri bodi ya ligi ili isimamie jambo hili. Kumekuwa na nafuu kwa kuwa mechi zinaonyeshwa Azam TV lakini hakukuwa na nguvu ya kutosha katika usimamizi wa hili.

Wanaotaka kuingia kuongoza waliliona, wana njia sahihi za kulifanyia kazi? Ni kina nani? Wapiga kura mtusaidie.

Mapato duni:
Tukubali, wadhamini wameongezeka hadi kwenye klabu hasa kubwa na hata zile ndogo, lakini vipi kuhusiana na uwanjani. 
Tokea mechi zimeanza kuonyeshwa live, kumekuwa na upungufu mkubwa wa mashabiki uwanjani jambo ambalo ni hasara kwa klabu.

Je, ni ushamba wa sisi watazamaji na live? Vipi England au Hispania kuna live na watu wanajaa uwanjani? Hapa kuna jambo la kujifunza na kulifanyia kazi kwa kuwa kweli tunahitaji Azam TV. Hivyo iendelee kuwepo lakini bado tufanye maboresho.

Matumizi mabaya:
Tunajua, mara nyingi tangu enzi za FAT, suala la matumizi mabaya ya ofisi limekuwa likichukua nafasi kubwa sana.

Matumizi hayo ni ufujaji wa mali za Fat au TFF na waliokuwa wakifuja waliona kama ni mali yao.
Waliowakosoa walionekana ni adui, waliohoji waliambiwa ni wanoko. Mwisho fedha zinatolewa kwa ajili ya maendeleo ya mpira ziliendeleza maisha na familia za watu. Hili si jambo zuri hata kidogo na limeonekana kuwagusa viongozi wengi wanaoingia madarakani mwisho inafikia inaanza kuonekana kila anayegombea kama anataka kwenda kujifaidisha.

Wapiga kura mnawajua hawa, acheni makundi au kuchagua kwa mihemko na mtusaidie kupata watu sahihi.

Urafiki, undugu, ukabila:
Nani anakataa kumekuwa na kubeba kirafiki ndani ya mpira wa Tanzania? Hii tumeona katika maofisi ya kawaida lakini katika ofisi za FAT au TFF, likachukua nafasi kubwa sana.
Mnajua nyote, ukiachana na urafiki hata ushabiki wa Usimba na Uyanga au ukabila nao umekuwa ukichukua nafasi na huenda utaendelea kuwa hivyo kwa kuwa tutaona aibu kuambiana ukweli.

Mimi nawaambia ukweli, nikiwakwaza nitakuwa nimewaamsha. Tuachane na urafiki, undugu na ushabiki wa Yanga na Simba katika suala linalolenga maendeleo ya mpira wetu.
Tunataka maendeleo bila ya makundi, hivyo wapiga kura pia muwe makini kutuchagulia kiongozi au viongozi watakaokuwa tayari kutoupa nafasi ukabila, urafiki na ushabiki.

Hakika tunataka maendeleo, hakika tunataka mabadiliko na tunataka kuona tulipofikia tunapiga hatua badala ya kuwa na mtu ambaye anaonekana atakuwa msaada badala yake anageuka kuwa sumu ya kuua mpira.

Chonde chonde, ukiona unagombea sababu ya kutuangusha, bora ujiondoe na wapiga kura, onyesha thamani ya kura yako usiitoe kujifaidisha, ufaidishe mpira wa Tanzania.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic