July 31, 2017



Na Saleh Ally
WALE ambao wamekuwa wakijiita ni viongozi wa Simba na wanataka kuzuia kila kinachotaka kufanyika ndani ya klabu yao ni “wapinga kila kitu”.

Wanaotaka kufanya hivyo tuamini wanaisaidia Simba? Kama wanaisaidia ni katika kipi?

Kuna hiki ambacho kimekuwa kikielezwa kwamba kuna mpango wa kuichukua Simba bila ya kufuata utaratibu unaotakiwa. Jambo ambalo na mimi napinga kabisa kama kweli lipo.

Lakini pia sitaki kuamini kwamba Wanasimba wote hawajielewi, hawana akili ya kung’amua kwa kuwa tu wale wanaojiita wazee wa Simba ndiyo wana uchungu peke yao kuliko wengine.

Kuna taarifa Simba wanataka kufanya mkutano, jana wazee hao wamefanya mkutano kuupinga kwa madai kuwa mdhamini wanayemuita ni mwenye mali Hamisi Kilomoni hajui lolote.

Tena imefikia hadi wanataka makundi ndani ya klabu kwamba wale asili na wale walioitwa Kanjibai jambo ambalo ni jambo baya kabisa na wanapaswa kuliepuka na kuachana na upuuzi wa namna hiyo.

Kama mkutano upo na utakuwa ni kwa mujibu wa katiba, basi ni jambo zuri ufanyike na baada ya hapo kama kuna upungufu wa mambo hao wanaojiita wazee ambao wengi ni wanachama walifanyie kazi hilo kwa kuwakumbusha wenzao kwamba kuna hili nao wapime.

Kikatiba, hakuwezi kuwa na mmoja anaonekana ana haki zaidi ya mwingine kama wote ni wanachama wa klabu. Kwamba kwa kuwa mmoja ni mkongwe, alikuwepo tokea enzi za Sunderland basi ana haki sana kuliko mwanachama wa Simba aliyejiunga hivi karibuni.

Wako wanaojidai wanaigombea Simba lakini hali halisi ni hivi; wanagombea matumbo yao na wanapiga kelele nyingi kwa ajili ya kutimiza matakwa ya matumbo yao yanataka nini.

Huenda hiyo haitoshi, wako watu wanaopiga kelele kusema wanataka kuiepusha Simba “kuchukuliwa”. Lakini ukifuatilia wanapiga kelele hizo kupitia baadhi ya viongozi ambao wameanzisha kampeni za chinichini wakitaka kurejea madarakani.

Wako waliokuwa viongozi wa Simba hawakufanikiwa, walifeli na sasa wameona mambo yametulia ndani ya klabu hiyo wanaona huenda kuna mafanikio yanakuja baadaye sifa wataipata wengine, basi wanaanza kufanya figisu na kawaida wanaotumika kuianzisha mara nyingi ni wanaojiita wazee.

Wazee wapewe heshima yao kama wao pia wanaheshimu wengine. Wakubaliwe wanachokisema kama kina hoja ya msingi na si kuheshimu umri wao hata kama wanachosema hakitakuwa ni sahihi. Pia ni vizuri kuwasikiliza kama chao kina msingi hata kama watakuwa hawana kitu.

Simba imepita kipindi kigumu cha majaribu kwa miaka mitatu mfululizo. Wazee walikuwepo na hatukuona msaada. Hao viongozi wa zamani wanaoendesha migogoro chinichini walikuwepo, sasa vipi baada ya nafuu ya msimu uliopita na kuonekana kuna nafuu inakuja msimu ujao, ndiyo wameanza kuipenda tena.

 Hivi sote tujiulize, anayezuia mkutano akiamini Simba “inataka kuchukuliwa” anamaana gani. Wanasimba wote ambao watakutana katika mkutano wakiwemo madaktari na watu wa kila aina watakuwa hawawezi kujua, kuhoji au kutaka kupata uhakika wa kila wanachokijadili kabla ya kupitisha?

Kama mzee Kilomoni ni kiongozi kwa mujibu wa katiba, vipi akataze mkutano unaotambulika kikatiba usifanyike. Kuendelea kuzuia mkutano ndiyo jibu sahihi? Au kuufanya na kuchukua uamuzi sahihi kama ni kupinga kinachotakiwa kufanyika au kukiunga mkono kutokana na hali halisi!

Wazee katika klabu kubwa wamekuwa chachu za kuanzisha migogoro. Wengi wamekuwa na hofu ya kuwaeleza lakini ukweli ni hivi, wanapaswa kuheshimiwa lakini waeleze ukweli wanapokuwa wanataka kuyumbisha jambo kwa faida ya watu.


Ninaamini Simba ina watu wa kila kariba. Wana uwezo wa kung’amua sahihi na isiyo sahihi. Kama kuna jambo la kuisaidia Simba, basi liongozwe kwa lengo la kuisaidia na si kuiangamiza kwa faida za wachache. Huu ujumbe uwafikie wazee wa Simba au wale wanaopingwa na wazee hao kama kweli kuna walakini. Fanyeni yote lakini uhai wa Simba ndiyo maisha sahihi.

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic