July 17, 2017



Na Saleh Ally
KUNA picha inasambaa katika mitandao mbalimbali ulimwenguni, wachezaji wa Everton FC ya England wakiwa wameshika bango lililoandikwa “Asante Tanzania”.

Kwa mujibu wa mtandao wa mashabiki wa Everton, unaeleza kwamba kwa Ulaya wanakadiria bango hilo limesomwa au kuonwa na zaidi ya mashabiki milioni 12 wa soka.

Pia wanaamini bango hilo limeonekana kwa zaidi ya mashabiki milioni 18 duniani kote kwa wale wanaoweza kusoma Kingereza na Kiswahili pia. Bado mtandao huo unaeleza bango hilo litakuwa limeonwa na zaidi ya watu milioni 50, mwishoni mwa mwezi huu.

Wanaamini hivyo kutokana na kasi kubwa ya maswali mengi ambayo wamekuwa wakipata kutoka sehemu mbalimbali duniani kuhusiana na Tanzania na maana ya neno Asante. Lakini pia taarifa wanazoelezwa na mashabiki wengi wa Everton wakiwemo wale wa nchi za Bara la Asia na hasa Thailand.

Wakati wa ujio wa Everton hapa nchini huenda ulionekana haukuwa na nguvu sana hadi siku nne kabla ya safari ilipofanikiwa kumsajili Wayne Rooney kutoka Manchester United.

Wakati Everton imekuja hapa nchini, hakuna anayeweza kupinga kuwa nchi yetu imejitangaza sana kupitia klabu hiyo hasa Wayne Rooney ambaye kwa sasa ndiye mchezaji nyota zaidi kwa wale raia wa England.

Wakati Everton wametutangaza na mwisho kumalizia kwa ujumbe mzuri wa “Asante Tanzania”, hakika ni faraja kubwa lakini vizuri tuwape shukurani zao waandaaji wa mechi hiyo, Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportPesa.

Tunakubali wote kuwa tumejifunza mambo kupitia ziara hiyo na mambo hayo yanaweza kuwa mazuri zaidi kama tutajifunza kupitia yale tuliyoyaona kabla ya Everton kutua nchini, walipowasili na baada ya wao kuondoka.

Maandalizi:
SportPesa walifanya maandalizi bora kabisa na kwa maana ya biashara huenda hata makampuni ya hapa nyumbani au klabu zetu zingeweza kujifunza.

Mfano angalia kwenye geti kuu la kuingilia wachezaji kwenda kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Utaona palipambwa kwa timu mbili za Everton na Gor Mahia, kabla haikuwahi kufanyika hivyo. Hata kama si timu, inaweza kutengenezwa picha nzuri inayohusu utalii wa Tanzania au vinginevyo pamoja na bendera yetu ya taifa ikawa ya kudumu au kadhalika.

Basi:
Mara zote tumeona timu zinakuja hapa na wanatumia magari ya kukodi yanayobaki kama yalivyo. Angalia SportPesa walichokifanya kwa basi la Shabiby. Hata kama walipata gharama lakini siku mbili basi hilo lililotembea na wachezaji, walijitangaza kwa kiasi kikubwa.

Walikuja Brazil na timu kadhaa kabla. Hatukuwahi kuitumia nafasi kama hiyo na vema hilo likawa somo pia.

Hata wakati wakishuka kwenye ndege, ngazi zilikuwa na jina la Tanzania na pia nembo za SportPesa.
Mengi yalikuwa mazuri ingawa mpangilio wa waandishi kuingia kidogo ulikuwa na walakini na wanapaswa kuurekebisha wakati mwingine.

Wachezaji:
Wachezaji wa Everton, licha ya kuwa na safari ndefu lakini walipata muda wa kutembelea sehemu mbalimbali wakiwa katika makundi. Mfano kuwatembelea albino, watoto wa Shule ya Msingi Uhuru, kukutana na Wamasai, kuweka maua kama ishara ya heshima katika makaburi ya mashujaa na kadhalika.

Uwanjani:
Uwanjani, utaona mapango yalivyokuwa na mpangilio mzuri na hata mpangilio mzima wa mchezo.

Mechi ilikuwa nzuri, imani yangu kama nilivyowahi kuandika awali, makipa walijifunza kama ilivyo kwa mabeki kwa kuangalia mabeki wenzao, pia viungo, washambulizi na hata makocha.


Hii ndiyo maana ya kumkaribisha mgeni anayeweza kuacha somo bora lakini kuwa na mwenyeji mtaalamu katika ukaribishaji mgeni na mwisho ni faida hii. Ndiyo maana nikasema kwa kuwa wachezaji wa Everton wamesema “Asante Tanzania”, nawaambia ahsanteni pia, nyie pamoja na wenyeji wenu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic