Beki wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga kwenye timu ya Baroka FC ya Afrika Kusini, Abdi Banda, amefunguka baada ya hivi karibuni kufunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na timu hiyo.
Banda ambaye amejiunga na timu hiyo hivi karibuni kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Simba, Jumanne ya wiki hii alifunga bao la kusawazisha katika mchezo wa ligi kuu ya nchi hiyo dhidi ya Orlando Pirates uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mchezo huo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Peter Mokaba unaotumiwa na Baroka, ulikuwa wa pili tangu kuanza kwa msimu huu ambapo Banda alifunga bao hilo dakika ya 73 kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na Sipho Moeti.
“Namshukuru Mungu kwa kuanza vizuri ikiwemo kufunga bao la kwanza la mashindano tangu nijiunge na timu yangu hii mpya, kikubwa nataka kupambana zaidi kuifikisha mbali timu yangu,” alisema Banda.
Kwa matokeo hayo, Baroka inashika nafasi ya 11 kati ya timu 16 baada ya kucheza mechi mbili na kupata pointi mbili. Mechi ijayo ni Septemba 12, mwaka huu watakapokuwa ugenini dhidi ya Chippa United.
0 COMMENTS:
Post a Comment