NA SALEH ALLY
HAKUNA anayeweza kukataa kuwa mchezo wa soka ni sayansi. Maana mambo yake kwa asilimia 90 yanahusisha hesabu ili kuyakamilisha.
Soka linahusisha hesabu kabla na baada ya mchezo. Lakini ni hesabu hata nje ya mchezo kama ambavyo unaona suala la mpangilio wa mambo katika mchezo huo, nini kifanyike.
Ukianzia uwanjani, mchezaji, kocha hufanya mambo yao yote kwa kufanya hesabu. Hata kutoa pasi, kuokoa, kufunga ni hesabu pia. Angalia faulo karibu zote hupigwa kwa hesabu.
Matokeo ya soka huwa hesabu, yale ya mwisho, uchezaji ulivyokuwa na kadhalika. Baada ya mechi kwisha utapiga hesabu za uchezaji wa wachezaji au kikosi kizima, pointi za matokeo zitaweka msimamo ambao unakwenda kwa hesabu.
Maana yangu kuanza na hesabu, nilitaka kukuambia mpira unataka kwenda kimahesabu zaidi badala ya unapozungumzia mambo yake. Au unapofikia umeamua kufanya jambo fulani la mchezo huo.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linataka kuongeza timu za Ligi Kuu Bara kutoka 16 hadi 20, jambo ambalo naona limekuwa la haraka na linahusisha mambo ya siasa.
Ninaona hivi; kwa kuwa viongozi wa TFF wana wapiga kura wao wa mikoani wangependa kutoa nafasi ya timu zaidi kuonyesha wanawajali.
Lakini sidhani kama ni jambo ambalo limefanyiwa utafiti wa kisayansi ili kuliruhusu lianze kufanya kazi. Maana kati ya vigezo vimeelezwa kuwa mchezaji wa Tanzania anatakiwa kucheza mechi nyingi. Pia imeelezwa kuwa mwamuzi anachezesha mechi chache ndiyo maana hatuna waamuzi wengi wa kimataifa.
Binafsi naona hapa si suala la idadi, badala yake ni ubora. Kama tutaangalia idadi halafu tusiwe na ubora, hata ingekuwa timu mia, bado yale ambayo yanazungumzwa leo kama sehemu ya upungufu yataendelea kuwepo kama yalivyo sasa.
Jiulize, Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), ina timu 16, lakini leo wametoa mabingwa wa Afrika, wao wametoa waamuzi bora kwenye Afcon, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho lakini kama haitoshi ina waamuzi wa Kombe la Dunia. Tumejaribu kujifunza kwao kwa timu 16 wamefikia hayo?
Moja ya ligi bora duniani ni ile ya Ujerumani ya Bundesliga. Hii ina timu 18 tu. Siwezi kukueleza kwamba Ujerumani wana waamuzi bora, wachezaji bora na timu bora ya taifa au timu bora za vijana kuliko sehemu nyingine duniani.
Utajiuliza kwa timu 18 pekee, vipi wanaweza kufikia yote hayo. Kwa nini wasingekuwa bora kwa kuwa na timu 30 katika ligi yao ili mchezaji acheze mechi nyingi zaidi na kufanya vizuri zaidi?
Lazima tujifunze kufanya mambo kisayansi na kuyafanya yaende kisayansi badala ya siasa. Kutaka mchezaji acheze mechi nyingi zaidi, TFF ilikuwa na nafasi ya kuboresha michuano ya Kombe la Shirikisho kwa upana zaidi, kuitafutia wadhamini na kuipa hadhi ya juu ili kufanya iwe na thamani na kila mmoja asikie fahari kushiriki.
Kuongeza ubora wa wachezaji wa Tanzania, si ligi kuu pekee. Angalia ligi daraja la kwanza, ni kama yatima vile. Bado haina usimamizi bora, haina mpangilio mzuri na haivutii kuwavuta wadhamini kwa kuwa hata utangazwaji wake kupitia TFF ni duni.
Unategemea kuwa na ligi kuu bora wakati wachezaji au timu zinazotokea ligi daraja la kwanza zina ubora duni au si zenye ushindani sahihi!
Kwani ubora ni mchezaji kucheza mechi nyingi za ligi pekee? Nafikiri TFF wanatakiwa kutafakari upya kuangalia yote haya na kujiuliza mfano kupitia Bundesliga na PSL kwamba pamoja na miundombinu bora, uhakika wa mambo na mpangilio bora, wana timu chache na wanaendelea kuwa bora katika upande wa timu, wachezaji na hata waamuzi.
Ni kweli uliyosema....twende kisayansi na si kisiasa.Timu 20 ni mzigo na gharama.
ReplyDelete