Bosi Msaidizi wa benchi la ufundi la Simba, Jackson Mayanja, raia wa Uganda, amefunguka kuwa, kombinesheni ya washambuliaji wao, Emmanuel Okwi na Juma Liuzio itaweza kuwa msaada mkubwa ndani ya kikosi hicho baada ya kujaribu kombinesheni za washambuliaji mbalimbali lakini zikafeli.
Kwa mara ya kwanza Okwi na Liuzio walianza pamoja kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting na kufanikiwa kuifungia timu hiyo mabao matano. Simba walishinda mabao 7-0 huku Okwi akifunga manne na Liuzio moja.
Mayanja amesema kutokana na kiwango cha wachezaji hao, wanaweza kuitumia pacha hiyo ambayo imeonekana kuelewana zaidi ya walivyokuwa wanacheza wachezaji wengine.
“Niwe mkweli kabisa hii pacha ya Okwi na Liuzio leo (juzi Jumamosi) ndiyo imetubeba na kuweza kuibuka na ushindi huu wa mabao saba, wote wamecheza kwa kasi na walikuwa wasumbufu kwa wapinzani wetu.
“Tuliamua kuwaanzisha wachezaji hao kwa sababu tuliona Liuzio ana kasi, nguvu na mwepesi wa kufanya maamuzi na kweli jambo hilo limesaidia kwani wapinzani wetu muda mwingi walikuwa wanamkaba yeye na kumuachia Okwi ambaye alikuwa anafunga kirahisi,” alisema Mayanja.
0 COMMENTS:
Post a Comment