September 18, 2017



NA SALEH ALLY
WAKATI mwingine unatamani kuwa na cheo ambacho hata si chako ili uweze kufanya jukumu ambalo unaamini kama linafanyika katika kiwango ambacho si sahihi kabisa.

Kila mtu ana kazi yake, lakini unaona mwingine ana nafasi lakini uzembe ndiyo unachukua nafasi kwa kiwango kikubwa bila ya hatua zozote kuchukuliwa.

Kusema umfukuze kazi mtu huenda linaweza likaonekana ni jambo la kuchochea mtu apoteze kazi, lakini kama ni mzembe au tatizo, unafikiri nini kinafuatia?

Kwa wanaokumbuka, msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kati ya viwanja vilivyokuwa vibovu na vililalamikiwa sana ni ule wa Majimaji wa mjini Songea.

Wadau walilia na uwanja huo baada ya kuonekana ukichezewa katika mechi kadhaa na ombi lilikuwa ni kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), kuhakikisha uwanja huo unafanyiwa matengenezo kwa ajili ya kuurekebisha hasa katika sehemu ya kuchezea.

Wote tunajua kwa nini wadau wanalia kutaka uwanja ufanyiwe marekebisho kutokana na kiwango chake duni utafikiri ni michuano ya mchangani.

Moja, hadhi ya Ligi Kuu Bara inapotea hasa kama uwanja unaotumika unakuwa katika kiwango duni kama ulivyo Uwanja wa Majimaji. Pili, afya za wachezaji na hata waamuzi zinakuwa hatarini kwa kuwa wanalazimika kucheza wakiwa na hofu.

Tatu, hofu hiyo ya uchezaji inasababisha kupunguza au kuondoa ladha yenyewe ya soka. Maana katika sehemu ya kutuliza mpira na kupiga pasi, wachezaji wanalazimika kubutua kwa hofu ya kupoteza mpira na kupata lawama au kusababisha madhara katika lango lao.

Wakati wadau wakilia msimu uliopita, ilikuwa mwishoni mwa msimu. Msimu umeisha, juzi, Majimaji walicheza mechi yao ya kwanza dhidi ya Yanga kwenye uwanja huo. Ilikuwa ni mechi yao ya tatu msimu huu lakini wakicheza kwa mara ya kwanza mjini Songea.

Wakati Majimaji ndiyo walikuwa wakicheza kwa mara ya kwanza, matarajio ilikuwa ni kuona uwanja ukiwa na mwonekano mpya wenye mvuto ukilinganisha na ule wa msimu uliopita.

Bahati mbaya kabisa, inaonekana haukuwa umefanyiwa marekebisho hata kidogo maana mwonekano wa safari hii, bora hata ule wa msimu uliopita. Ni sawa na kusema mechi ilikuwa inachezwa kwenye jaruba la mpunga la mjini Songea.

Hakuna anayeona aibu kuhusiana na mechi ilivyokuwa hasa kwa uongozi wa Uwanja wa Majimaji mali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao nimekuwa nikiwakumbusha mara kwa mara kuwa wanaweza wakavibinafsisha viwanja hivyo kama wamekubali vitumike katika Ligi Kuu Bara.

Kitu cha kwanza ningeweza kulia na Majimaji kuwa hawana uwanja wa mechi, hii inasababisha tuanze kulia na CCM. Lakini kwa kuwa uongozi wa Majimaji unakubali kuchukua fedha, swali langu linafuatia vipi unatoa huduma mbovu na kuchukua fedha?

Maana kuutumia lazima kulipia, halafu huduma ni duni na hakuna uboreshaji wa huduma. Hii si sawa, ni sawa na dhuluma pia ni sawa na kutojali wateja, jambo ambalo ninaamini kama uongozi ungekuwa ni wa meneja makini au uongozi wa CCM Mkoa Ruvuma, ungekuwa makini na kujali michezo ikiwa ni pamoja na kuijali Majimaji, basi wangefanya marekebisho.

Meneja ameshindwa vipi kulisimamia hilo, namchukulia kama mzembe ndiyo maana nikatumia kauli ya “Chukua Meneja wa Uwanja wa Majimaji,  mtupe ndani.” Maana huu ni uzembe na anaona mambo poa tu na hii inatokana na Majimaji kutokuwa na pa kukimbilia.

Hakika ni aibu, inakatisha tamaa na kusababisha kiwango cha soka kuendelea kubaki kilipo kwa kuwa viwanja havizidi vinne ambavyo vina kiwango sahihi kuchezewa mpira katika kiwango cha Ligi Kuu Bara.


Huenda kama kutakuwa na uwajibishwaji, basi mameneja wa viwanja vingine nao wataona aibu na kuachana na mazoea na kupiga kazi. Nasisitiza, kama Majimaji, Songea uko vile, kumtimua meneja poa tu ili akajifunze, maana kuanza upya si ujinga.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic