September 18, 2017



MUNICH, Ujerumani
MPAKA jana kabla ya mechi ya Dortmund vijana wa Hannover 96, ndiyo walikuwa kileleni kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga.

Hannover wapo mbele ya Bayer Munich ambao kwa miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakishindwa kuanza vizuri kwenye ligi hiyo lakini kishindo chao cha kumaliza ligi hiyo kimekuwa cha kutisha.
Juzi Jumamosi mashabiki wanaofuatilia Bundesliga kwa kutumia king’amuzi cha StarTimes ambacho kwa Tanzania kimekuwa kikirusha mechi zote kubwa mubashara ‘live’, walishuhudia michezo mikali sana wakiwa sebuleni kwao.
Bayern Munich, waliendelea kuonyesha umwamba wao kwenye ligi hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Mainz.

Staa aliyepotea kwa muda kidogo, Arjen Robben, juzi alirejea tena kwenye kasi yake na kufanikiwa kuifungia timu yake kwenye mechi hiyo iliyokuwa muhimu kwao kushinda.

Mbali na matokeo hayo, Werder Bremen wenyewe walipambana na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Schalke 04.

Mechi nyingine ilishuhudia Chadrac Akolo, ambaye ana uraia wa Uswisi baada ya kukimbilia nchini humo kama mkimbizi akitokea DR Congo mwaka 2009, akiifungia VfB Stuttgart iliyopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya VfL Wolfsburg.
Katika mchezo wa jioni wabishi kwenye ligi hiyo RB Leipzig walishuhudia kiungo wao Naby Keita akitolewa nje wakati walipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Borussia Moenchengladbach.


Katika mchezo wa Bayern, Thomas Mueller, alianza kwa kuwafungia bao safi katika dakika ya 11, kwa shuti kali ambalo lilimgonga Robben na kutinga wavuni.

Dakika chache baadaye Robben alifanikiwa kuifungia timu hiyo bao la pili, baada ya kuambaa na mpira kwa mguu wa kushoto na kufunga kirahisi kwa mguu wa kulia.

Mashabiki wa StarTimes walishuhudia Robben akifunga bao lake la kwanza kwa mguu wa kulia tangu Februari mwaka 2015.

Robert Lewandowski alifanikiwa kuifungia timu yake bao la tatu kwenye mchezo wake wa 100 akiwa na Bayern, huku Muller akitoa krosi safi iliyomkuta staa huyo wa Poland na kufunga bao la nne kwa Bayern.

Kwa sasa Bayern na Schalke 04 wana pointi tisa baada ya kucheza michezo minne wakiwa nyuma ya Hanover 96 ambao waliichapa Hamburg SV 2-0 juzi Ijumaa.
Augsburg waliendelea kuonyesha kiwango kizuri baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt. Ushindi huu umewafanya kuwa na pointi sita wakiwa katika nafasi ya saba.

Lewandowski ameendelea kutikisa kwenye ufungaji bora kwenye ligi hiyo baada ya kufikisha mabao matano.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic