JUZI Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es
Salaam, tulishuhudia mchezo wa Ligi Kuu Bara uliozikutanisha wenyeji Azam dhidi
ya Simba.
Matokeo ya mchezo huo yalikuwa suluhu. Awali kabla ya mchezo huo,
hofu ilikuwa kubwa kwa mashabiki juu ya usalama wao, lakini Jeshi la Polisi
Tanzania likawahakikisha kutakuwa na usalama huku likitoa angalizo kwa
mashabiki kwamba wawe wastaarabu.
Mashabiki walitahadharishwa mapema kwamba
wanatakiwa kufuata utaratibu uliowekwa, lakini pia kwa wale watakaofika
uwanjani na kukuta uwanja umejaa, basi warudi nyumbani na kushuhudia mechi
kupitia luninga. Kikubwa ambacho naweza kuwapongeza mashabiki, walifuata kile
ambacho walitahadharishwa mapema, lakini pia jeshi la polisi lilikuwa
limejipanga tayari kuweka ulinzi wa kutosha kuhakikisha hakuna uvunjifu wa
amani.
Mwanzo mpaka mwisho wa mchezo, hakukuwa na vurugu zile ambazo wengi
walikuwa na hofu nazo jambo ambalo linadhihirisha kwamba mashabiki wa soka hapa
nyumbani wamestaarabika na kuondoa ile dhana inayoonyesha kwamba mchezo wa soka
ni wa wahuni. Kumekuwa na dhana hiyo kutokana na kwamba, mara kadhaa kumekuwa
na vurugu viwanjani ambazo chanzo chake ni mashabiki, lakini kilichotokea juzi
pale Azam Complex, imeondoa dhana hiyo mbaya. Rai yangu ni kwamba, amani kama
hiyo iendelee kutokea viwanjani kote ili kuepusha uharibifu wa mali viwanjani
kama ilivyotokea Uwanja wa Taifa katika mechi kadhaa kama ile ya Yanga dhidi ya
TP Mazembe na ya msimu uliopita iliyowakutanisha Simba na Yanga ambayo
ilisababisha uwanja huo kufungwa kutokana na mashabiki kung’oa viti. Kutokana
na vurugu kutawala sana viwanjani, siku za nyuma Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilishindwa kutoa ruhusa kwa Azam FC kuutumia uwanja
wao huo kwa mechi za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga.
TFF ilikuwa haina imani
na usalama wa uwanja huo kwa jinsi ulivyo, kwanza unaingiza idadi ndogo ya
mashabiki ambayo ni 7000 tofauti na Uhuru unaoingia zaidi ya mashabiki 23,000
na ule wa Taifa unaochukua watazamaji 60,000. Mashabiki wa Simba na Yanga
wanapocheza na Azam wanakuwa wengi, hivyo TFF ilikuwa ikihofia kuzuka kwa
vurugu kama itatokea mashabiki watakuwa wengi tofauti na uwezo wa uwanja huo.
Lakini baada ya jeshi la polisi kujiridhisha juu ya kujipanga kwao kulinda
usalama na kuwadhibiti mashabiki, tukaona TFF ikiruhusu kwa mara ya kwanza
kutumika na mpaka dakika tisini zinamalizika, Azam ikashindwa kufungana na
Simba.
Baada ya mchezo huo kumalizika kwa amani, tunatarajia kuona tena Yanga
wakienda hapo na mambo yakiwa sawa katika suala zima la usalama kama ilivyo kwa
wenzao wa Simba. Mwisho kabisa niwaambie Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar na Mwadui
FC ambao nao walikuwa wanataka kuona mechi zao dhidi ya Simba na Yanga zinachezwa
kwenye viwanja vyao, kuvifanyia marekebisho ili kuipata haki yao. Kwa mujibu wa
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred, viwanja vya timu hizo ambavyo ni
Mabatini, Manungu Complex na Mwadui Complex havina hadhi ya kuchezewa mechi
hizo kutokana na kutokuwa na majukwaa ya kutosha.
Kama kweli viwanja hivyo
vinataka kupata haki kama waliyoipata Azam FC, hawana budi kufuata kile TFF
inavyotaka kwani tayari wameambiwa juu ya kuweka majukwaa kwenye viwanja vyao
ili hata zile mechi zingine wanazocheza hapo ziweze kuchezwa kwani wasipofanya
hivyo, kuna hatari ya kufungiwa viwanja vyao.
0 COMMENTS:
Post a Comment