September 30, 2017




Na Saleh Ally
BEKI wa Majimaji ya Songea, Juma Salamba alimpiga kiwiko mshambulizi wa pembeni wa Yanga, Emmanuel Martin ambaye alitolewa nje kwa ajili ya matibabu.

Mechi kati ya Yanga iliyokuwa ugenini dhidi ya Majimaji kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea iliisha kwa sare ya bao 1-1 mabingwa hao watetezi wa Tanzania Bara walilazimika kufanya kazi ya ziada kusawazisha.

Kama ni muungwana, lazima uwapongeze mabeki wa Majimaji kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kuwa walikuwa wanapambana na safu ya ushambuliaji iliyoifanya Yanga kubeba ubingwa zaidi ya mara mbili mfululizo, si jambo dogo.


Hata kama safu hiyo ilikuwa ina mabadiliko lakini utaona wengi wa wachezaji walikuwepo katika ubingwa mara mbili. Majimaji wakafanya kazi nzuri kuwasimamisha ingawa walifanikiwa kusawazisha.


Wakati mechi ilikuwa gumzo kutokana na soka kuchezwa kwa ushindani mkubwa, hilo lilikuwa jambo moja. Gumzo jingine likawa ni beki Salamba kumpiga kiwiko Martin ambaye alikuwa ameuma ulimi na madaktari wakafanya kazi ya ziada kumuokoa.



Mmoja wa madaktari alinieleza kwamba ilikuwa hatari kwa maisha yake kama wasingemuwahi. Daktari huyo alilaani kitendo hicho na kusema kilikuwa kibaya na kinapaswa kupigwa vita.


Kilichonishangaza, kuona ushabiki unachukua nafasi kubwa katika suala hilo ambalo linahusisha mambo mawili. Kwanza ujinga na ukatili wa binadamu mmoja na uhai wa mtu mwingine ambao ulikuwa hatarini kwa sababu ya ujinga wa yule mwingine.


Mijadala imepita mingi, ikiwemo ile ya mitandaoni ambayo kwangu naona hujumuisha watu wengi sana wasiojielewa au wasiopima wanachokitoa katika vichwa vyao na kuruhusu mikono yao kupitia vidole iandike!


Wako ambao walikuwa wakihoji kwamba: “Kwani Martin yeye ni nani, kwani wamewahi kupigwa wangapi?” Wengine wakaweka msisitizo: “Kwa kuwa mchezaji wa Yanga imekuwa ishu, vipi wengine huwa hamsemi!”


Hawa watu waliuliza au kuchangia maneno mengi sana ya ajabu. Wakati mwingine unajikuta ukitamani angalau kuona sura ya aliyeandika ili uweze kupata majibu ya maswali yako ambayo yanakuwa yamejikanganya kwa njia inayoshindwa kutoa majibu ambayo yanaweza kukusaidia kurahisisha mambo.


Kuumia kwa Martin ni jambo la kibinadamu na Martin alikwenda kucheza mpira na pale ndiyo kazini kwake. Adhabu aliyopewa hastahili na maumivu yake si sahihi. Vipi badala ya kuangalia alichofanyiwa uanze kuhoji mchezaji fulani hakushughulikiwa.


Kwani sisi Wtaanzania kulalamika ndiyo akili sana? Kuponda ndiyo ujanja sana? Au ndiyo kwa kuwa jambo liko katika macho ya watu kila mmoja angependa kuonyesha umahiri wake hata kuzungumza mambo ya kijinga ilimradi tu!


Nafikiri iko haja ya kujifunza na kuelewa ushabiki ni nini, tuwe
wakweli na kuwasaidia vijana wetu wanapokosea, tuwaeleze ukweli na kuwashauri nini cha kufanya badala ya kutaka kupoza makosa yao kwa makosa yaliyowahi kutokea.


Kama TFF chini ya Jamal Malinzi haikushughulikia mambo, hii chini ya Wallace Karia imeamua kushughulikia, basi tuiunge mkono irekebishe mambo ila kama italala, basi tuikumbushe bila ya woga.

Kama mchezaji amefanya ujinga kama ule wa Salamba, basi hakuna haja ya kuingiza ushabiki, tumueleze ukweli, ajirekebishe na baadaye awe msaada kwa taifa letu kwa kuwa umri wake unamruhusu.


Ushabiki “mandazi” hautusaidii sana, badala yake vizuri kuwa wazi kwa wachezaji wanapokosea ili kuwasaidia kubadili njia na kupita iliyo sahihi.

Ushabiki katika maumivu ya mwanadamu mwenzako si sahihi na alichofanya Salamba ni kitu cha kijinga kabisa na wengine wanastahili kukilaani na kuwa mfano kwa kutokifanya.


Salamba hawezi kupata timu nje ya Tanzania kwa ubora wa kupiga viwiko. Hivyo anachokipambania ni kupoteza muda na kujipunguzia uaminifu kwa kuwa mchezaji bora pia anastahili nidhamu ili kujijengea njia ya utimilifu wa ndoto zake.


Hivyo, tuwe wakweli, wanyoofu wa mambo na bila ya ushabiki, tupinge mambo maovu yanayohatarisha maisha ya wachezaji.


Kwa kuwa TFF wameanza kulishughulikia suala hili, basi tuwape nafasi ya kupita katika njia sahihi kwa mujibu wa kanuni na mwisho kuwe na jibu sahihi.


1 COMMENTS:

  1. Tatizo sio kwamba watu wanaunga mkono ujinga alioufanya Salamba la hasha. Tatizo ni ukigeugeu wa nyie waandishi inapotokea kosa kama hilo amefanya mchezaji wa Simba au wa Yanga. Ni rahisi kwenu kulaani makosa ya wachezaji wa timu zingine kwa makala ndefu na kushikwa na kigugumizi inapozihusu timu hizo mbili. Kuweni wakweli kwenye kuandika.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic