October 20, 2017



Na Saleh Ally
NILIMUONA aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja akiwa anazungumza kuushukuru uongozi wa Simba kutokana na makubaliano yao baada ya yeye kuomba kuondoka kutokana na matatizo ya kifamilia.

Mayanja alikuwa amekaa na Msemaji wa Simba, Haji Manara ambaye naye pia baadaye alimshukuru kwa ushirikiano wake akiwa pamoja nao na mambo mengine kadhaa.

Ukiangalia ni njia moja nzuri ya kutengeneza uungwana mbele ya jamii, jambo ambalo naweza kusema Simba wamefanya siasa nzuri yenye lengo la kuendeleza umoja, si jambo baya.

Ukituliza kichwa utagundua au utaamini kama ninavyoamini mimi kuwa Simba wameanza utaratibu wa kung’oa mti kwa kupunguza matawi kwanza na baada ya hapo itafuatia kazi ya kung’oa mizizi yenyewe.

Baada ya kumuona Mayanja akizungumza pale, bila ya kuwaza mambo mengi nikatamka “Safari ya Omog, inakuja”. Ninaamini haitakuwa na siku nyingi sana kwa kuwa tayari Mayanja ameng’oka.

Wakati fulani, Gazeti la Championi liliwahi kuandika kuhusiana na kutakiwa kuondoka kwa Mayanja ili nafasi yake ichukuliwe na kocha Mrundi. Baadaye Omog akaomba kwa juhudi kubwa kutaka Mayanja abaki kwa kuwa wamekuwa wakifanya kazi vizuri pamoja na kwa ushirikiano.

Baada ya hapo, mashabiki wengi wa Simba walilalamika kuwa walidanganywa kwa kuwa Simba haikuwa na mpango wa kumuondoa Mayanja na baadhi ya viongozi wakasambaza propaganda kutaka kuonyesha Simba haikuwa na mpango huo hata kidogo.

Leo lile limetimia kwa kuwa lilikuwa limepangwa siku nyingi ili Mayanja aondoke. Omog akaona kuendelea kufanya mambo ya kawaida ni kuzuia kuondoka kwa Mayanja, akafanikiwa. Safari hii imeshindikana na ninaamini Mayanja atakuwa ametupiwa virago na suala la hadithi za “matatizo ya kifamilia”, haliwezi kuwa sababu muhimu zaidi kwa kuwa hata akiwa Simba, Mayanja aliendelea kuyashughulikia matatizo hayo.

Viongozi wa Simba watakuwa wanayajua mengi kuhusiana na timu yao. Wakati tunasubiri safari ya Omog iwadie kuna mambo mengi ya kujikumbusha.
Masoud Juma aliyewahi kuwa mchezaji wa APR na kocha mwenye mafanikio wa Rayon Sports, zote za Rwanda, ndiye anatarajia kuchukua nafasi ya Mayanja. Raia huyo wa Burundi anajulikana kwa ubora wa kazi zake.
Masoud ni mwanadamu kama Mayanja na atakuwa na matatizo yake kama Omog kwa kuwa wote ni wanadamu.


Nanyi Simba mnapaswa kukubali kuwa hata viongozi nao ni wanadamu na mmekuwa sehemu ya matatizo hayo.
Wako wachezaji ambao wamekuwa wakilalamika kuhusiana na Mayanja na wengine wakiamini hawapati nafasi ya kucheza kwa kuwa Mayanja amekuwa tatizo kubwa kusababisha wasipate nafasi.

Wachezaji haohao bado hawakuwa wakionyesha juhudi sahihi ya kutosha ili kuwashawishi makocha hao kuwapa nafasi. Inawezekana vipi mchezaji anayeweza kusaidia kupatikana kwa matokeo awekwe benchi halafu ambaye asiye na msaada acheze! Huyo atakuwa kocha wa namna gani asiyeijali nafasi yake ya kazi kiasi hicho?

Wako wachezaji wavivu, wako wachezaji wenye majungu na wako wachezaji wasio na upendo pia kwa kuwa wote ni binadamu kama sisi na wana sehemu yao ya upungufu.

Kama viongozi wamechukua hatua ya kumuondoa Mayanja kwa matatizo yake, basi wana nafasi ya kuwarekebisha wachezaji wanaong’ara kwa midomo badala ya utendaji wa kazi.

Kama Omog naye ataondoka mapema au atachelewa hadi hapo baadaye lakini lazima wanaofanya kazi na Masoud wajue si kocha mwenye mzaha na kama walikuwa wakilalamika kwa Mayanja, wanaweza wakalalamika zaidi kwake.

Kocha huyo Mrundi anachotaka ni kazi, ana sifa ya ukali, hapendi mzaha kazini, pia ni mtu anayechukia kushindwa. Hivyo kila ambaye ni mvivu anaweza asivutiwe na Mrundi huyo na baadaye lawama za chinichini zikaanza ili kuonyesha ni mbaya.

Wakati Mayanja anaondoka huku tukisubiri na safari ya Omog kukamilika, basi wachezaji nao wabadilike ili wawe msaada kwa kocha mpya. La sivyo naye ataishia kuonekana ni mbaya au hafai kutokana na visingizio vyao.

Ninaamini uongozi wa Simba unafanya kila jambo kutaka mambo yaende vizuri, kikosi kishinde kulingana na usajili. Kazi kubwa ya uongozi ni kutengeneza umoja katika kikosi hicho ili watu waangalie zaidi suala la kupata ushindi kwa pamoja badala ya kutengeneza maneno mengi yanayovunja umoja.


2 COMMENTS:

  1. Kwani kuna ubaya gani mbona Juma Mwambusi kaondoka bila hata ya kuagwa!

    ReplyDelete
  2. Kwani we ndo msemaji wa simba naona unajua sana zaidi ya simba wenyewe

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic