October 20, 2017


Kikosi cha Simba, wiki ijayo kinatarajiwa kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga utakaopigwa Oktoba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.

Simba itaondoka jijini Dar kwenda Zanzibar baada ya mchezo wao wa kesho Jumamosi dhidi ya Njombe Mji utakaopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru.

Mmoja wa wachezaji wa kimataifa wa Simba ambaye hakupenda kuandikwa jina lake, ameliambia gazeti hili kuwa tayari wamepewa taarifa za kwenda Zanzibar kuweka kambi kwa ajili ya kuiwinda Yanga.

“Tumeambiwa mchezo wetu wa Jumamosi dhidi ya Njombe Mji ukimalizika, basi tujiandae na safari ya kwenda Zanzibar kuweka kambi ya muda mfupi kujiandaa na mechi ijayo dhidi ya Yanga.

“Nadhani uongozi unajua kule Zanzibar ni sehemu tulivu ndiyo maana imekuwa ikipenda kutupeleka kwenda kuweka kambi kama ilivyokuwa hivi karibuni tulipokuwa tukijiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga,” alisema mchezaji huyo.


Alipoulizwa Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon kuhusu mipango aliyoiweka kabla ya kuikabili Yanga, alisema: “Ngoja kwanza tumalizane na Njombe ndiyo nitaanza mikakati ya kuikabili Yanga. Siwezi kuidharau Njombe ambayo ndiyo tunapambana nayo kabla ya Yanga, hivyo akili yetu kwa sasa ipo kwa Njombe na si Yanga.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV