October 13, 2017




NA SALEH ALLY
KATI ya mambo ambayo yalikuwa yanazua mkanganyiko mkubwa katika uendeshaji wa soka hapa nchini lilikuwa ni suala la ushabiki au ubaguzi wa masuala ambayo yalipaswa kuamuliwa kwa kutenda haki.

Katika mchezo wa soka, suala la makosa lina kiwango kikubwa sana kwa kuwa ni mchezo ambao unajumuisha watu wengi katika makundi tofauti na kila moja likiwa na malengo yake.

Ushindani katika makundi hayo dhidi ya jingine na kila kundi likiwa limejumuisha watu wenye tabia tofauti ni rahisi sana kuzua hali ya sintofahamu.

Tumeona katika uongozi uliopita wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ulivyokuwa ukilalamikiwa katika mambo yaliyokuwa wazi kabisa lakini liliendelea kukaa kimya bila ya kufanya jambo lolote.

Mfano ile ishu ya Amissi Tambwe kumvuta korodani beki Juuko Murshid wa Simba au Donald Ngoma wa Yanga alipompiga kichwa cha wazi beki Hassan Kessy wa Simba wakati huo.

Hadi Kessy anahamia Yanga, hakukuwa na uamuzi wowote uliochukuliwa na mambo yaliendelea kuwa kimya bila majibu huku ikionyesha wazi kuwa TFF ilifanya makusudi.

TFF kwa nini ilifanya makusudi? Unaweza ukajiuliza maswali mengi sana na wakati mwingine ukachanganya kuhusiana na ushabiki wa kupitiliza wa viongozi wake huenda kwa kuwa waliwahi kuwa viongozi wa Yanga?

Fikra hizo zinaweza zisiwe sahihi lakini zikawa zimezalishwa na uzembe wa viongozi wenyewe na kwa kuwa matukio yote yaliwahusisha Yanga. Halikuwa jambo zuri na niseme wazi, TFF ilikuwa ikifanya mambo kizembe na ilifanya ubaguzi wa hali ya juu ambao ulipaswa kukemewa kwa nguvu nyingi sana.

Maamuzi ambayo yanasababisha kuzuka kwa hisia mbaya au ambazo zingeweza kuepukika ni jambo baya sana hasa kama unajumuisha jamii ya watu yenye imani na chombo ambacho kinaweza kutenda haki.

Hakuna haja ya kuficha mambo, tunajua Rais aliyepita wa TFF, Jamal Malinzi alikuwa Yanga na anaendelea kuwa Yanga, katibu wake alikuwa Yanga pia kama ambavyo wasaidizi wake wawili niliwapinga kabisa kutokana na uwezo wao mdogo waliokuwa nao kiuongozi waliokuwa Yanga pia.

Huenda hii ilichangia wakawa wanashindwa kuwa na maamuzi sahihi katika mambo ambayo yalikuwa wazi na yalistahili kuchukuliwa hatua ambazo zilitakiwa kuchukuliwa kwa wakati mwafaka kama ambavyo tuliona katika tukio ambalo Amissi Tambwe alikabwa na beki wa Ruvu au pale Juma Nyosso alipofanya ufirauni wake kwa John Bocco.

TFF ya sasa chini ya Wallace Karia ambaye ni shabiki wa Simba, tunaona kuna mabadiliko kwa kuwa kamati zimeamka na zinatenda haki katika mambo ambayo tunaona yana makosa.

Mfano kusimamishwa mechi tatu kwa beki Juma Salamba wa Majimaji ambaye alimpiga kiwiko Emmanuel Martin wa Yanga au kusimamishwa kwa mwamuzi msaidizi aliyekataa bao la Laudit Mavugo wa Simba dhidi ya Stand United.

Wote tuliona na tunakubali kamati imefanya kazi na pia Simba, Stand na timu nyingine zimepigwa faini kutokana na uzembe ziliofanya.

Kama Karia ameanza hivi, ni jambo zuri na inaonyesha itakuwa ni TFF inayofuata weledi. TFF itakayokuwa inaamua haki kwa wakati mwafaka bila ya kuangalia kiongozi wake mkuu au viongozi wanavutia au kupendelea timu fulani kutokana na mapenzi yao binafsi.

Hakika lazima tukubali, kama unataka kufanya vizuri katika jambo lolote, suala la haki linapaswa kuwa namba moja. Hakuna haja ya kumuunga mkono Karia aipendelee Simba au kuzishinikiza kamati kuipa kipaumbele badala yake ni kutenda haki kama walivyoanza na linapaswa kuwa jambo lenye mwendelezo kwa nia ya maendeleo ya mpira wa Tanzania.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic