October 16, 2017



Na Saleh Ally
NAWEZA kuamua kushangazwa na kila kinachotokea, mwisho utakuwa ni uamuzi wangu uliotokana na matakwa binafsi. Lakini inakuwa vigumu sana kujizuia kuamini kwamba mambo mengi yanayozungumzwa na mashabiki wa soka ni kweli hawajui au kila wanachosema huwa ni utani tu!

Nina haki ya kushangaa na hili ndiyo ninataka kuanza nalo tena nikiweka msisitizo mkubwa. Lakini nina haki ya kuhoji kwamba katika soka, watu wengi uelewa wao umeporomoshwa na ushabiki wa kupindukia?

Nani anayetaka kusema wanaopenda sana soka hawaelewi mambo? Hilo nitakataa kwa kuwa nina wengi ninawajua wanapenda soka na waelewa hasa wa mambo na wako tayari kujifunza yale ambayo yanawapa ugumu. Lakini vipi sasa wapenda soka wengi hawapendi kujifunza na mwisho wake karibu kila linalozungumzwa kwao ni ziro?

Ninaanzisha mjadala, hii ni mijadala miwili inayofanana, ninachagua kuichanganya kuwa mmoja kwa kuwa kuna jambo linaweza kuifananisha na kuwa jambo moja.

 Naanzia kule mitandaoni ambako naona kuna taswira sahihi ya wapenda soka ambayo nimeanza nayo kuifafanua kuwa inashangaza na kutaka kujenga hisia sisi tunaopenda soka, hatuelewi karibu kila jambo. Jambo ambalo ninaamini si sawa na kama wapo wanapaswa kubadilika.

Niliona kuna baadhi ya mashabiki wa Simba walikerwa sana na kiungo wao mpya Haruna Niyonzima raia wa Rwanda baada ya kusema ana jezi za Yanga ambazo amezihifadhi kama sehemu ya kumbukumbu.
Niyonzima alisema hilo wakati wa mahojiano ya moja kwa moja na Kipindi cha Spoti Hausi ambacho hurushwa na Global Tv Online lakini kwa nia nzuri kabisa akisisitiza kuna kumbukumbu ambazo anapaswa kuhifadhi kutoka Yanga.

Niyonzima alisema hata alipotoka APR ya kwao Rwanda, alihifadhi jezi na kumbukumbu kadhaa za timu hiyo wakati anakwenda Yanga na akasisitiza kuwa siku akiondoka Simba, ataendelea kuhifadhi jezi za Simba pia kama sehemu ya kumbukumbu. Baada ya hapo, imeonekana ni kosa na kuzua mjadala.

Hili ndiyo linalonishangaza na kuona kuwa hakika kuna kila sababu ya sisi tunaopenda mpira kujielimisha na kuachana na “siasa laini za soka” kuzungumza mambo madogo na kuyalazimisha kuwa makubwa bila ya sababu.

Kwa wale ambao hupenda kuonekana wanazipenda timu zao mbele ya jamii. Nawashauri hivi, kuzipenda timu zao ni jambo binafsi, furaha binafsi na hawapaswi kupata sifa au kupewa tuzo kwa kuzipenda timu zao. Wazipende kwa furaha zao na si kutaka kuonyesha watu.

Wako ambao wamekuwa wakiandika maneno ya matusi kumshambulia Niyonzima kwa hilo. Ninaamini wachezaji wengi wa Kitanzania nao angalau wana kumbukumbu ya baadhi ya timu walizopita lakini wasingependa kusema kwa kuwa wanajua mashabiki waliopo si waelewa na wanaweza kuanza kuwalaumu.

Siamini kama John Bocco anaweza asiwe na jezi hata moja ya Azam FC kama kumbukumbu kama ilivyo kwa Erasto Nyoni au Aishi Manula. Hili lina ubaya upi na kwa nini washambuliwe kama adui?

Najua mashabiki wengi wa Simba ni waelewa, wanaoweweseka ni wachache wapenda sifa wenye mapenzi ya matangazo. Lakini Niyonzima anapaswa kuwaonyesha yeye ni mwanasoka, awajibu uwanjani kwa kufanya kazi yake kwa ufasaha. Kwa mwanasoka mzoefu kama yeye kelele haziwezi kuwa chanzo cha kumvuruga hasa kwa ambao wanaonekana wagumu kusikiliza au kutazama na wakaelewa.

Kama nilivyoanza mwanzo nilianza na kusema naunganisha hoja. Hii ni kuhusiana na Ibrahim Ajibu wa Yanga ambaye sasa amefunga mabao matatu ambayo yameipa Yanga pointi tisa.

Ajibu anaanza kuonyesha anachokiweza, kwa wanaokumbuka wakati alipotua Yanga niliandika makala kuelezea namna ninavyomuamini na kumpa nafasi ya kufanya vizuri kama atafanya mambo kadhaa ambayo nilieleza huku nikiweka wazi upungufu au udhaifu wake.

Ajibu anajua mpira lakini sote tunajua alikuwa mzembe wa mazoezi na hakuna anayepambana kupata asichonacho. Kwa kuwa ameondoka Simba na anajua akikosea Yanga si kama ilivyokuwa Simba, lazima atajituma na kwa kuwa ana uwezo, basi atafanya vizuri.

Nilimshauri kuipenda Yanga zaidi na kusahau ya Simba ili kuepuka kujichanganya. Sasa Yanga ndiyo kazini na mipango yake ya maisha na si Simba tena.


Lakini ajabu zaidi, naona kuna ushindani wa Niyonzima na Ajibu na nimeona baadhi ya watu wakijaribu kuuchambua “kitaalamu” jambo ambalo linachekesha sana. Kwamba Simba imemtoa Ajibu imepata hasara kwa kuwa aliyeziba pengo lake Niyonzima hafanyi vizuri.

Kuna mengi pia ya kujifunza ili kufanya mambo vizuri. Niyonzima anacheza kiungo cha uchezeshaji na Ajibu ni kiungo mshambulizi. Hawa ni watu wa aina mbili tofauti na inakuwa kichekesho zaidi kulingamisha mabao ya Ajibu na Niyonzima ambaye kufunga kwake kama itatokea.

Hofu ni kwamba, kama Niyonzima atarejea na kuwa katika kiwango bora, inawezekana likawa suala la kuhesabu kiwango cha Ajibu kwa kumshindanisha na Niyonzima kama atatoa pasi nyingi za kufunga mabao au kuisaidia timu yake kwa kiwango cha juu zaidi.

Lazima tujifunze kuangalia mambo kisayansi na wakati mwingine kujua unachokizungumza kinafananaje na kile unachokifananisha. Hata kama sote tunajua mpira, basi si lazima kila mtu awe tu anachambua ili mradi mapenzi yake yanapokwenda.

Ajibu anaweza kufananishwa na Emmanuel Okwi na ikiwezekana apate ushindani unaoweza kumuinua zaidi kwa kuwa mimi ninaamini anaweza. Halafu acha Niyonzima tumfananishe na Thabani Kamusoko kuwa wanafanya vipi kazi zao hasa kama wote watakuwa fiti. Mpira ni sayansi na inapita katika njia zake.



2 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic