October 2, 2017




Na Saleh Ally
UKISEMA ni mapema sana kuanza kufikiria bingwa atakuwa ni nani katika Ligi Kuu England unaweza kuwa sahihi kabisa.

Maana timu zimecheza mechi saba kila moja na mbili zitakamilisha leo idadi hiyo. Kweli ni mapema lakini bado kuna nafasi ya kuona mwelekeo.

Mimi nakwenda moja kwa moja, kwamba ubingwa wa Ligi Kuu England maarufu kama EPL unakwenda Manchester na hakutakuwa na mjadala.

Nasema unakwenda Manchester nikiwa ninamaanisha jiji, yaani timu mbili zinazotoka katika jiji hilo tulivu ndiyo zenye nafasi ya kubeba ubingwa wa EPL na hili itakuwa vigumu sana kuligeuza.

Ingawa ni mechi saba  kwa timu zimechezwa, lakini naweka asilimia 95 hadi sasa ya ubingwa kwenda jijini Manchester yaani kuchukuliwa na Manchester United au Manchester City na hii nitakueleza kwa nini ninaamini hivyo.

Kwa miaka nenda rudi, ukiachana na mwaka juzi, ubingwa wa England umekuwa ukichukuliwa kwa zamu kati ya timu za Jiji la London ambalo ni kubwa kuliko yote ya England na Uingereza na Manchester. Leicester kidogo ndiyo walibadili mwelekeo lakini msimu uliofuata, Chelsea wakalibeba tena kombe hilo na kulirejesha jijini London.

Chelsea kwa miaka ya hivi karibuni, wameonekana ndiyo wakombozi wakubwa wa London kwa kuwa Arsenal wameonekana kutokuwa na nguvu ya kubeba EPL na Tottenham wamekuwa wakilikosakosa karibu misimu mitatu mfululizo sasa.


Tottenham ndiyo timu pekee inaonekana itakuwa na nguvu ya kuwatikisa wababe wa Manchester na kufanikiwa kubeba ubingwa huo kama wao watazubaa kidogo au kuteleza lakini unaposema hadi sasa mwenye nafasi ya kuwa bingwa ni nani, basi namba moja ni Manchester na namba mbili ni Manchester ndiyo maana nasisitiza, ubingwa utakwenda katika jiji hilo.

TAKWIMU:
Ukiangalia kwa kufuata takwimu ambazo ndiyo ufunguo wa mchezo wa soka, City wameshinda kwa mechi tano zilizopita mfululizo na United wamefanya hivyo kwa mechi nne mfululizo pia. Takwimu zinaonyesha katika mechi saba, United wameshinda sita sawa na City na wote wana sare moja, hawajapoteza.

Baada ya mechi saba za ligi, timu ambazo hazijapoteza hata mechi moja ni United na City pekee. United imefunga mabao 21 katika mechi hizo, City imetinga nyavuni mara 22. Kila moja imeruhusu mabao mawili tu.

Mwendo huu unazifanya kuwa timu bora zaidi hadi sasa, lakini hakuna nafasi inayoonekana kuzuia ubora wao kwa kipindi kirefu na kama watakwenda hadi mwisho wa nusu ya ligi, basi wana asilimia 90 nyingine za kuchukuana wenyewe hadi mwisho wa msimu.



MAKOCHA:
Usisahau hii ni vita kati ya makocha wawili mahiri na maarufu na wenye uzoefu mkubwa wa kupambana lakini wamefundisha timu tofauti na katika ligi tofauti na kote wamebeba makombe au ubingwa muhimu ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Usitoe mfano ule wa “mbona Arsenal huanza vizuri halafu wanamaliza vibaya”. Huyu ni Pep Guardiola na yule ni Jose Mourinho, fikiria mara mbili. Ni makocha wasiokuwa na makosa mengi na wanajua wafanye nini wanapotaka makombe.

Kumbuka Mourinho amebeba ubingwa England mara moja tatu, amebeba makombe Hispania, Ureno na Italia. Guardiola amefanya hivyo na Barcelona katika kiwango cha juu. Akachukua makombe Ujerumani. Maana yake atakuwa akitaka kuweka rekodi ya kuwa bingwa England pia na hili linamfanya kuwa na “wazimu” wa ushindi katika kila mechi kutaka ubingwa.

Ushindani kati yao ulianzia Hispania wakati Mourinho alipotoka Chelsea na kujiunga na Real Madrid na akaanza kazi ya kupambana kuvunja ufalme wa Barcelona ya Guardiola. Mechi ya kwanza wanakutana, Mourinho akapoteza kwa mabao 5-0. Utaona baadaye alichokifanya, alipunguza kila kitu na kufanya mambo yaende wengi ambavyo hawakutarajia.


Makocha hawa ni tofauti kidogo na Kocha Wenger na kama wameanza hivi, usitegemee kasi yao kuanguka kwa kushitukiza na unaweza kujifunza kwa Mourinho ambaye alikuwa na timu ya “ili mradi” msimu uliopita, alibeba Kombe la Europa League. Sasa ana timu imesimama, Guardiola akiwa amezoea mwendo wa EPL, unategemea nini?

Lazima timu nyingine zifunge mkanda hasa kama watataka kutibua plani ya ushindi ya Guardiola au Mourinho. Maana wana uzoefu na mipango ya ubingwa kwa kujua waanze na mguu upi kabla ya kuendelea. Bila ya ubishi, mguu walioanza nao unaona ukoje hadi sasa.


Kama nilivyoeleza awali, Tottenham inaonekana ndiyo timu pekee ya London inaweza kutibua “pilau la Manchester”. Hata kama mpira una miujiza, acha tusubiri lakini nafasi kubwa inaonekana ubingwa wa EPL utakwenda Manchester.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic