October 8, 2017



Na Saleh Ally
MISIMU miwili iliyopita nilieleza namna ambavyo nilishangazwa na kipa kinda wa Simba, Peter Manyika alivyokubali kiwango chake kuporomoka hadi kufikia kuhamia benchi.

Niliweka wazi ambacho niliamua alistahili kufanya kuliko kuendelea kusubiri akifia benchi. Lakini hata alipojaribu kurejea ikaonekana nafasi yake ilikuwa ndogo sana.

Taarifa kwamba kuna baadhi ya viongozi wa Simba wamekuwa na chuki naye kutokana na muingiliano wa masuala ya wapenzi, zikachukua nafasi na ikaonekana Manyika asingeweza kuwa na nafasi tena Simba. 

Hapo ndipo niliandika makala nyingine ya kumshauri akitaka kuimarika lazima aondoke na kwa umri wake alistahili kucheza badala ya kukaa benchi.

Siku chache baadaye, tulifanya mahojiano na baba yake Manyika Peter ambaye ni mmoja wa makipa magwiji kabisa hapa nchini ambaye alisifia nilichoandika kuhusiana na kuporomoka kwa Manyika na akaeleza namna alivyomfukuza nyumbani kwake baada ya kuona hamuelewi.



Akaeleza baadaye alivyofanikiwa kumshawishi kwa kumuomba msamaha kupitia wajomba zake na baada ya hapo akarejea kufanya kazi kwa ufasaha na kurejesha kiwango chake. Mwisho akasema, alichukua uamuzi wa kumuondoa Manyika Simba.

Alisema wazi pia pamoja na uamuzi wake, lakini ushauri wa makala yangu kwamba alipaswa kuondoka naye aliona ni jambo jema kwa kuwa lazima afanye hivyo maana pamoja na kiwango chake kurejea, bado ilionekana kuna baadhi ya viongozi kama wameapa kwamba Manyika hatacheza tena kikosi cha kwanza.


Uamuzi wa baba yake, awali kama uliwashangaza wengi lakini yeye alishikilia msimamo na kusema ilikuwa ni lazima aondoke hata kama atacheza timu ndogo ya Ligi Kuu Bara kwa kuwa alijua usalama wake ni kucheza ili kuonyesha alichonacho.



Ninajua wapo waliomshauri baba Manyika kumuacha mwanaye angalau kwa msimu mmoja lakini akashikilia msimamo wa kumuondoa na mtoto akamsikiliza na mwisho ameangukia Singida United.

Hadi sasa baada ya mechi tano za Ligi Kuu Bara, Singida United inashika nafasi ya tatu nyumba ya Simba na Mtibwa Sugar zenye pointi 11, yenye ikiwa na pointi 10.

Timu iliyofungwa mabao machache zaidi ni Azam FC, hadi sasa imefungwa moja na inafuatia Mtibwa Sugar na Singida United zilizofungwa mabao mawili halafu Simba iliyofungwa matatu sawa na Ndanda FC.

Manyika ndiye kipa namba moja wa Singida United akiwa anasaidiwa na mkongwe Ally Mustapha ‘Barthez’ ambaye aliwahi kuwa kipa namba moja wa Simba na Yanga.



Kocha wake, Hans van Der Pluijm anamjua vizuri Barthez maana alifanya naye kazi, lakini ameangalia kipaji cha Manyika jambo ambalo Simba walilipa nafasi kwa muda, akaharibu mwenyewe.

Aliporejesha kiwango chake, hawakutoa nafasi na kama unakumbuka ilibaki kidogo wamuache na kubaki na makipa wote wawili wa kigeni, jambo ambalo wadau walilipinga.


Leo Manyika ni kati ya makipa walioitwa katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kinachoivaa Malawi, leo katika mechi ya kimataifa
ya kirafiki.

Kwa hali ilivyo inaonekana ataanza kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula lakini hakuna ubishi kwamba msaidizi namba moja na mwenye nafasi kubwa ya kuwa kipa namba moja baadaye ni Manyika.

Manyika amepata somo, huenda atakuwa na akili nyingi ya kutorudia alichokifanya awali. Kama kweli kutocheza kwake Simba kuliendana na kilichoelezwa, yaani chuki. Leo waliohusika wanapaswa kujiadhibu wenyewe na waone aibu kwa uuaji vipaji kwa makusudi kwa sababu ya masuala yao  binafsi na iko siku itafikia kama wanachofanya ni kweli, kitakuwa hadharani.

Kuhusiana na uamuzi wa Manyika Peter ambaye ni mzazi na mwalimu wa Peter Manyika. Anapaswa kupongezwa na kuwa mfano wa wazazi ambao wanaweza kuamini uamuzi wanaochukua hata kama hawaaminiki au wanaonekana wanakosea.



Manyika angebaki Simba, bado angekuwa maarufu sana kwa jina la kipa namba mbili au wa kwanza katika wachezaji wanaobaki benchi.


Leo, ana kiwango au hadhi kama ilivyo kwa kipa namba moja wa Simba na kilichobaki sasa ni yeye kutuonyesha inawezekana ili wengine wenye uwezo waliong’ang’ania mabenchi ya timu kubwa, watafute njia mpya ya kukua badala ya kufa kisoko, eti kisa wanapata heshima au ujiko wa kuwa katika timu kubwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic