September 16, 2019






NA SALEH ALLY
MECHI ya Ligi ya Mabingwa kati ya wenyeji Yanga dhidi ya Zesco United kuwania kucheza hatua ya makundi ilikuwa na mvuto sana.


Mvuto ulikuwa ni namna timu zilivyokuwa zikicheza na aina ya upangaji mashambulizi kuhakikisha zinaibuka na ushindi.
Yanga kama ilivyokuwa kwa Zesco, kila upande ulitengeneza nafasi nyingi na kila upande ulionekana ulipania hasa kushinda.


Mwisho matokeo yalikuwa ni sare ya 1-1, hii ilitokana na pande zote mbili kutozitumia nafasi za kufunga kwa ufasaha. Kama wangekuwa makini, hata mmoja angeshinda basi idadi ya mabao ingekuwa ni zaidi ya hayo mawili, yaliyopatikana.


Zesco wamepata bao lao la kusawazisha, sekunde za mwisho katika dakika ya mwisho ya mchezo ikiwa ni muda mfupi baada ya mwamuzi wa mchezo huo kutoa kadi ya njano kwa kipa Metacha Mnata wa Yanga kutokana na kupoteza muda akijiangusha bila hesabu.




Yanga walistahili kushinda angalau bao 1-0, hili lingekuwa jambo jema kwa wawakilishi wetu hawa wa Tanzania kwani lazima tukubali, wakiingia hatua ya makundi, si faida kwa Wanayanga pekee, bali ni Watanzania wote.


Bao lililotibua hesabu za Yanga, limefungwa na Mzimbabwe, Thabani Kamusoko, kiungo mkongwe wa zamani wa Yanga ambaye Kocha George Lwandamina aliamini anahitaji “chumvi” yake aliyokula kwa wingi kama sehemu ya kufanya kilicho sahihi.


Kamusoko ndiye alikuwa moyo wa Zesco katika mechi hiyo, huku Yanga ikitumia viungo hadi sita kuhakikisha inamiliki mpira. Kweli ilifanikiwa kwa kuwa Abdulaziz Makame, Mohamed Issa ‘Banka’, Feisal Salum ‘Toto’, Papy Tshishimbi na Patrick ‘Papy’ Sibomana walikuwa wakipambana na Kamusoko aliyekuwa akiwaongoza viungo watano wa Zesco.


Kamusoko alikuwa chachu ya Zesco kuisumbua Yanga hasa wakati inashambulia kwa kuwa mpira wake ni ule wa moja kwa moja, direct football, mpira usiolenga mbwembwe na badala yake malengo ya kutimiza kile kinachotakiwa.


Angalia pamoja na nguvu ya viungo wengi, hasa ile “Pembe Tatu” au “Triangle” ya Yanga ya Makame, Fei Toto na Banka kuwa na nguvu, lakini ilishindwa kuwa na malengo hasa kutokana na “utoto” mwingi.


Angalia “back pass” nyingi walizofanya, walirudisha mpira zaidi ya mara tatu bila kuangalia na wachezaji wa Zesco wakainasa na kuanzisha mashambulizi yaliyokuwa hatari kwenye lango la Yanga. Hili likirudiwa kule Zambia, litaiondoa Yanga.


Kwa upande wa Kamusoko, hakukuwa na muda wa kuchezea au kufanya utani na unaona alikuwa anaifanya kazi yake kwa maelekezo ya kocha au kwa ujuzi na uzoefu wake na mwisho imekuwa faida kwa Zesco ambayo imepata faida ya sare kutokana na bao lake la kusawazisha.


Huenda Kocha Mwinyi Zahera hakumuona vizuri Kamusoko, maana mwishoni alisema hakuona alichocheza zaidi ya kufunga bao, lakini ninaamini hawezi kumsifia kwa kuwa alikubali aondoke na wengi tuliaminishwa “amekwisha”.


Wengi tuliambiwa Kamusoko sasa ni mzee na hana kitu, siku chache baadaye, tumemuona akiwa katika kikosi cha Zimbabwe kilichokwenda kushiriki michuano ya Afcon. Alicheza na akaonyesha kiwango kizuri, shahidi macho yetu.


Hiyo haitoshi, leo Zesco ni tegemeo tena anacheza dakika 90 kwa ushindani wa juu akionyesha kiwango bora. Kufunga bao katika dakika 90+, maana yake hata baada ya dakika 90, alikuwa bado hai na ana uwezo wa kufanya vizuri na huu ni ujumbe mwingine tunapata wadau wa soka Tanzania.


Kama unakumbuka hivi karibuni, baada ya kipa mkongwe Juma Kaseja kuibuka shujaa akiisaidia mara mbili Taifa Stars kusonga mbele, akianza na dhidi ya Kenya na baadaye Burundi.


Kaseja naye ilikuwa hivyo kama Kamusoko, ingawa Kaseja ni wetu kwa maana ya Mtanzania lakini ubora wa Kamusoko nao unaweza kuunganishwa hapa kwamba tuliaminishwa kwa matakwa ya watu binafsi lakini si uhalisia.


Kamusoko bado alikuwa na nafasi ya kuwa msaada Yanga, angeweza kufanya vizuri zaidi lakini huenda alidharauliwa, hakuaminiwa, mwisho akafa moyo na kuonekana ameisha na hafai.


Kaseja ilikuwa hivyo na leo tumeona kwa Kamusoko na inawezekana wako wengi sana wanafanyiwa hivyo kwa kuwa kuna wale walioshika mpini wanafanya wanavyotaka kuwamaliza wengine lakini kwa matakwa binafsi.

Yanga haitakiwi kukata tamaa kwa kuwa wakiamua itawezekana lakini tujifunze na tutumie mafunzo haya ya Kaseja na Kamusoko kubadilika.


 Zesco imeondoka imetuachia somo na lazima tukubali, kuna kitu kinapaswa kufanyika ili kuing’oa Zesco lakini Yanga lazima iende Zambia ikijua Kamusoko bado ni hatari kwao, asibezwe kwa maneno wakati vitendo vyake vinaonyesha ni mtu hatari.

























3 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic