November 3, 2017



NA SALEH ALLY
NIMEKUWA nikishangazwa sana na watani, Yanga na Simba kugeuzia hasira zao kwa waandishi kwa kila kile wanachoteleza kwa hisia kuwa wanaonewa.

Simba na Yanga utafikiri watoto mapacha wanaopenda kupendwa na kuthaminiwa hata kama wanafanya vibaya kupindukia, bado wangependa kusifiwa.

Mmojawapo akifanya vema akasifiwa, mwingine hata kama anafanya vibaya naye hupenda tu kusifiwa. Ukisema wana mambo ya kitoto wala hautakuwa umekosea.

Maana ukiwasifia sana, siku wakiharibu pia watakuambia unatusifia sana hadi tunaharibu. Ukitaka upotee katika taaluma yako hasa ukiwa mwandishi, basi jikite kwenye kutaka kuwafurahisha Simba na Yanga, nakuhakikishia utayumba na mwisho utakwama kabisa.

Ukitaka kufanya vizuri katikati ya Simba, kitu namba moja “piga kazi” bila ya woga ukiangalia ukweli, haki na usahihi bila ya kujali nani anafurahi au kukasirika. Kila mmoja ana akili timamu ya kupima na kupambanua, hivyo ataamua analoona ni sahihi au la. Kitu kizuri ukweli huwa unauma lakini haufichi uhalisia kwa yoyote yule.

Wakati nimezoea kuona hivi kwa Wanasimba na watani zao Yanga. Juzi nilishangazwa sana kumsikia askari mstaafu, Abdul Mingange naye akiingia kwenye siasa za Yanga na Simba.
Mingange alikuwa akihojiwa katika kipindi cha michezo cha Radio One. Mtangazaji alitaka kujua Mingange vipi ametoka kufundisha timu za Ligi Kuu Bara hadi kwenda kuwa kocha wa timu ya vijana ya Azam FC? Mtangazaji aliona kama Mingange alikuwa amejishusha “kithamani!”


Mtangazaji alikuwa na haki ya kuuliza, ajabu Mingange alionekana kuhamaki, akatoka nje ya hoja na kuzungumza mambo utafikiri shabiki wa soka wa mtaani ambaye unaweza kumuona yuko sahihi kutokana na kuwa shabiki na si mtaalamu wa jambo fulani kama ilivyo kwa Mingange.


Kwanza alianza kulaumu kwamba waandishi hawawaandiki makocha wazawa, wanawapendelea wa nje tu! Alimueleza mwandishi yeye alipambana kuiokoa timu isiteremke daraja zikiwa zimebaki mechi chache lakini haonekani kama amefanya kazi yake!


Kwangu ilishangaza sana, niliona Mingange naye ameingia katika siasa za mpira au kama ndiyo yuko hivyo basi hastahili kuwafundisha vijana, anaweza kuwachanganya kwa kuwa moja ya mbinu bora ya kuwakuza vijana katika michezo ni subira.

Mingange alionekana hakuwa ni mvumilivu anayeweza kujenga subira inayoweza kutoa matunda bora hapo baadaye kwa kusema jambo ambalo halina uchunguzi.


Hata kujulikana kwamba amejiunga na Azam FC, ilijulikana kupitia vyombo vya habari vya Tanzania na waandishi si wazungu wa Uingereza. Kama ni kuiokoa timu, inajulikana na ndiyo maana Mbeya City wakamchukua ambako hakukaa kabla ya kuondoka.


Ninaamini Blog ya SALEHJEMBE imekuwa ikimuandika sana Mingange kwa kuwa ni mtu anayetoa ushirikiano kila anapotafutwa. Sasa sijui alitaka aandikwe kuhusiana na nini kama inajulikana kila kitu chake kupitia vyombo vya habari.

Wakati pia, kuandikwa si kuandikwa tu. Lazima kuwe na jambo linalosababisha kuandikwa kama ambavyo Radio One walimtafuta baada ya kujiunga na timu ya vijana ya Azam FC.

Mingange anajivunia kitu kikubwa pekee ni kuiokoa timu kuteremka daraja na hakuna kingine, lakini bado angependa aandikwe ikiwezekana zaidi ya kocha aliyechukua ubingwa. Waungwana hata sisi tunapaswa kuwa watenda haki si kulaumu tu.

Makocha au wadau wengi wa mpira wakiwa hawajaanza kujulikana hupenda kushirikiana na vyombo vya habari, wakishajulikana inakuwa shida na kikubwa au urafiki wao na vyombo vya habari unakuwa ni lawama tu. Hata kama atakosana na chombo kimoja, basi atajumuisha vyote akiwataja waandishi kwa jina moja kwa kosa la mtu mmoja au chombo kimoja.

Nafikiri Mingange ambaye ni kocha mzoefu, mwanajeshi mstaafu anapaswa kuwa mfano wa kuonyesha namba moja ni kupiga kazi na si longolongo. Lawama tu haziwezi kujenga kwa kuwa sikuwahi kumuona akishukuru kila alipoandikwa. Mzee piga kazi. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic