November 3, 2017



Na Saleh Ally
NIMEONA Msemaji wa Simba, Haji Manara akisumbuka sana kupambana na watu mitandaoni, akijaribu kutaka kuwaonyesha kwamba alilozungumza au mambo aliyoyazungumzia yana ukweli.

Manara amefanya hivyo baada ya mashabiki wengi wa Yanga kumshambulia wakionyesha kukerwa kwake na huenda wako wale wa Simba ambao wanaona kama yeye alichangia wao kutoshinda kwa kuwa kabla ya mechi dhidi ya Yanga, alionyesha wana uhakika wa kufanya vizuri. Mwisho ikawa sare ya bao 1-1 huku Yanga wakionekana kupiga soka safi zaidi na mashambulizi yao yaliitikisa Simba.

Manara ana haki ya kupandisha morali ya Simba anapokuwa akizungumzia mchezo wowote wa timu yake na ingekuwa ajabu kama kweli angesema wanakwenda uwanjani wakiwa hawana uhakika hata kidogo wa kuifunga Yanga.

Alichosema kwamba wataifunga Yanga, wamejiandaa na wana uhakika. Si jambo baya wala geni na hata kama Ulaya iko hivyo, basi wanaosema husisitiza wanautaka ushindi, shida kuna kitu kimoja, namna ya uzungumzaji.

Maana inaweza ikawa moja lakini uzungumzaji ukawa tofauti. Usemaji wa Manara unaweza ukawa unawakwaza ambao wanamsikiliza lakini kitu kizuri kabisa kwake ambacho nakiona, sijawahi kusikia akimkashifu mtu au kumsemea maneno mabaya zaidi ya kuweka utani.

Ushabiki wa Manara unaweza kujumuisha utani kwa kuwa ndiyo Simba na Yanga zilivyo. Naona “dunia” ya wachache wanaojilazimisha kuwa “wengi” imeamua kumshambulia mfululizo kutaka kuonyesha kila anachofanya si sahihi.

Kuna ambaye anakosea kama mwanadamu na huenda yanatokana na matamshi na binafsi mara kadhaa nimewahi kumueleza hata kwa maandishi, lakini si kila anachofanya kinaonekana ni kosa.

Katika suala la kumlalamikia mwamuzi, Manara alionekana akiwaambia waandishi kwamba Simba wanaamini walistahili kupata penalti dhidi ya Yanga lakini haikuwa hivyo baada ya mwamuzi, Elly Sassi kutotoa penalti.

Mitandaoni, huenda ni mashabiki wa Yanga wamekuwa na jazba kuona ile video ikionyeshwa huko na huenda ingefichwa na anayeibandika mtandaoni atageuka kuwa adui, huenda wanaona anaishambulia Yanga.

Wale wa Simba, nao wakiona video hiyo, mazungumzo yao yanaonekana kujaa jazba wakati wakiilalamikia penalti hiyo.

Wako ambao huenda ni wa Yanga au Simba wamekuwa wakihoji vipi video hiyo iwekwe kwa kuwa hakuna uwezo wa kubadilisha. Naona ni watu wasiojua maana ya mjadala. Mnaweza kuwa na mjadala unaozalisha au kusaidia kukuza au kubadilisha kitu baada ya kutokea.

Huenda mwamuzi alifanya kosa la kibinadamu na kuwa bora ni lazima mwamuzi ajirekebishe na kupunguza makosa kwenda katika ubora wa juu. Yeye anaweza kujifunza kupitia mijadala hiyo, halikadhalika wakufunzi wa wawaamuzi wanaweza kuitumia sehemu hiyo kama somo ingawa wao wanapaswa zaidi kuangalia kiuweledi badala ya ile ya kishabiki.

Wako wale ambao kila kitu wanatukana, huenda wanaamini kuwa mitandaoni wana haki ya kutukana matusi ya nguoni wakiwa wamejisahau kuwa sheria ya mtandao imeanza kufanya kazi.

Jambo zuri sana kujadiliana na mwanadamu anayejenga hoja badala ya yule anayeamini matusi ya nguoni. Yeyote anayetukana anakuwa ni mtu asiyejielewa, asiyejitambua, hajui au hana jambo la kujadili kuhusiana na kinachozungumziwa ndiyo maana anaona kukatiza ni kutukana tu. Huu ni ulimbukeni uliopitiliza.

Manara anapaswa kuwa na moyo mgumu na ajue anafanya kazi ambayo kamwe haiwezi kuwa ya kuwafurahisha watu. Hivyo aendelee kujali kazi yake na kuifanya kwa ubora ulio sahihi.

Kitu kikubwa zaidi anachotakiwa kuangalia, katika wale wanaotoa maoni asiwachukulie kama wote wanafanana au kulingana. Badala yake wale wenye hoja za msingi anaweza kuyachukua maoni yao na kuyafanya sehemu ya kujiimarisha au kuboresha utendaji wake.

Inshallah, mwakani nitatimiza miaka 20 nikiandika habari za michezo, lakini nimekuwa nikijifunza kupitia mashabiki wa juzijuzi kwa kuwa hauwezi kujua mtu atazungumza nini. Pale ninapoona kilichozungumzwa kweli kina hoja, bila ya kujali aliyekizungumza ni chipukizi au mkongwe, nakichukua na kukifanyia kazi.

Niliona wengi wangependa na Manara aanzishe gazeti la klabu kama walivyofanya Yanga. Yeye alipinga kwa hoja ambazo niliona hazina mashiko, kitu kizuri unaweza kuiga. 

Bado nina swali, nani ana uhakika jarida hilo la Yanga limekuwa na faida. Anayesema zimechapwa kopi 100,000 ana uhakika au ndiyo ushabiki? Limeiingizia Yanga faida kweli?

Hivyo ni wazo zuri kupewa Manara lakini kabla ya kulichukua, vizuri afanye uchunguzi wa kutosha kuliko kuiga tu ilimradi kwa kuwa watani wamefanya. Wale wanaomshauri naamini wana nia nzuri lakini nao si sahihi kulazimisha kwa kuwa ni ushauri wao basi lazima ufanyiwe kazi tu.

Mti wenye matunda ndiyo unaopopolewa, Manara asitegemee kupumzika kwa kipindi hiki na madongo kwa kuwa watu watampopoa nani? Hivyo kwa mazuri na mabaya atazungumzwa tu kwa kuwa ndiye msemaji maarufu zaidi kwa kipindi hiki akifuatiwa na Masau Bwire na Thobias Kifaru.


Maana yake anatakiwa kuwa mvumilivu, mwenye subira, anayesikiliza na anayeweza kuzizuia jazba zake lakini naye awasilikize wale ambao waliomueleza halafu wana hoja za msingi.

7 COMMENTS:

  1. Nimekua nikifatilia makala zako kwa mda mrefu sana bro salehe
    Na nimekua muumini mzuri sana wa haya unayohubiri,navutiwa sana na utendaji wako wa kazi,nakupongeza sana na Mungu abariki kazi ya mikono yako na kinywa kiendelee kutoa busara kama hizi,makala hii nzuri ni kama jibu kwa manara hasa juu ya yule mchambuzi nguli aliye msema
    Nami naomba wachambuzi wengine waige mazuri kwako naamini sisi wasomaji tutanufaika kuliko ilivyo sasa

    ReplyDelete
  2. Narudia tena kusema Saleh Ally ni mlima kwenye mkusanyiko wa vichuguu. JEMBE Hans chuki haendeshi kampeni za majungu bali anakosoa,anaelimisha na kuburudisha.Continue with the good work

    ReplyDelete
  3. Ushasahau kama aliwai kumkashifu tshishimbi dhidi ya shilole?

    ReplyDelete
  4. Mimi kama shabiki wa simba sc nimekuelewa sana.

    ReplyDelete
  5. SALEHE ni mnafiki tu....ngoja labda watakupa ajiri hao maswahiba zako

    ReplyDelete
  6. Manara hajui kutofautisha kati ya sisa na mpira......suala na kuamua mtu ameshika kwa kukusudia au hakukusudia amepewa mwamuzi mamlaka hayo na sio simba wala manara. Aache mdomo kamaanataka kuwa anaropoka na kushindana sense akawe msemaji wa vyama vya siasa huko......juzi Madrid wamefungwa goli mfungaji na mtoa pasi wrote wakiwa wameotea....umemsikia Afisa habari wa Madrid alinyanyua mdomo?. Hebu yeye huyo jamaa aache maneno ya hovyo na kashfa na mdomo.

    ReplyDelete
  7. Well articulated.

    Vijana walioanza ushabiki juzi ni kama hawajui utani wa Simba na Ynga ulivyo mkubwa lakini wa kistaaraju tangia Enzi.

    Hwataki kuona nhoja wasiyoipenda. hawajui hoja lazima zitolewe hata km huzipendi, hawajui haki pekee waliyo nayo ni kujibu kwa hoja zenye mantki na siyo kutukana.

    nadhani wengi watajifunza hapa.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic