November 3, 2017




NA SALEH ALLY
Majibu ya Yanga na Singida United yatapatikana kesho, kwamba nani ni mbabe zaidi ya mwenzake katika Ligi Kuu Bara hasa mzunguko wa kwanza.

Mechi hiyo inakuwa ni ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kuwakutanisha baada ya mara ya kwanza kukutana katika mechi ya kirafiki na Yanga kupoteza kwa bao 1-0.

Singida United watakuwa wenyeji wa Yanga katika Uwanja wa Namfua mjini Singida, uwanja unaoweza kusema nao pia ni wageni kwa kuwa ndiyo watakuwa wanautumia kwa mara ya kwanza katika mechi za Ligi Kuu Bara baada ya matengenezo kukamilika.

Hans van der Pluijm anahusika katika ubingwa wanaoushukilia Yanga, alikuwa kocha mkuu kabla ya George Lwandamina kuchukua nafasi yake na akapanda cheo kuwa mkurugenzi wa ufundi.

Baadaye, Pluijm aliamua kuondoka Yanga na kujiunga na Singida United wakati Lwandamina raia wa Zambia alimalizia kazi na kupa Yanga nafasi ya kutetea ubingwa wake ilioupata mikononi mwa Pluijm.

Sasa wakali hao, kila mmoja angependa kushinda dhidi ya mwenzake lakini utamu unakuja kutokana na takwimu za msimamo wa ligi hiyo.

Yanga ina pointi 16 katika nafasi ya pili na Singida United, ina 13 katika nafasi ya 6. Kama Yanga watapoteza kesho, basi watakuwa wakilingana pointi na Singida United na kuingia kwenye hofu ya kupitwa na wapinzani wao Simba watakaokuwa wakicheza na Mbeya City, Jumapili hasa kama watashinda.

Presha ya Yanga inakuwa kubwa zaidi kwa kuwa wangependa kufanikiwa mambo hayo mawili kwa pigo moja takatifu. Lakini wakikubali maana yake wako katika presha kuu tena mara mbili.

Presha ya kwanza itakuwa ni kuzidiwa na Simba kama watashinda au kutoa sare na wanaweza kuzidiwa na Mtibwa Sugar au Azam FC pia kama watashinda.

Lakini, watakuwa wametoa nafasi ya kufikiwa na Singida United na kuongeza presha nyingine.

Kwa Pluijm, naye ana presha, kushinda dhidi ya Yanga ni jambo zuri zaidi kuwaonyesha wamekosea pia kuwafanya waajiri wake wapya waamini wamebeba "Jembe" hasa.

Lakini pia kuhakikisha wanawafikia Yanga itakuwa nu kuongeza hali ya kujiamini katika kikosi chake.

Bado Pluijm naye ana presha ya kuzidiwa kwa pointi na Prisons ambayo ina pointi 13 pia. Kama Singida watafungwa na Prisons washinde, basi ni presha maradufu na wanaweza kuporomoka hata hadi nafasi ya nane hasa kama Lipuli na Mbeya City nao watashinda.


SINGIDA:
Pointi 13
Nafasi ya 6
Mabao ya kufunga 6
Mabao ya kufungwa 4

YANGA:
Pointi 16
Nafasi ya 2
Mabao ya kufunga 11

Mabao ya kufungwa 4

1 COMMENTS:

  1. Yanga vs Singida matokeo ya mechi ya kirafiki yalikuwa Yanga 3-2 Singida utd utakuwa umesahau

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic