November 13, 2017




NA SALEH ALLY
KESHOKUTWA Jumatano dirisha dogo la usajili litafunguliwa na timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara baada ya mechi 9, zitakuwa na nafasi ya kujipanga upya na kurekebisha sehemu ambazo zinahitaji kufanya hivyo.

Baada ya mechi 9, timu zitakuwa zimeona kulingana na zilipo. Nafasi zipi baada ya kukusanya kiasi kipi cha pointi na zenyewe zinajua ukusanyaji wake wa pointi ulipita katika njia zipi.

Wakati wa kufanya usajili wa maboresho ya kikosi, hakika unahitaji utulivu wa hali ya juu kwa ajili ya kuhakikisha safari iliyobaki inasomeka kwa mwendo sahihi baada ya mabadiliko.

Kuangalia kikosi kilivyo, mabao ya kufunga na kufungwa yalikuwa mangapi. Ushindi na sare yanakuwa ni matokeo ya ujumlisho wa kilichofanyika hasa baada ya kuangalia ‘performance’ mfano, walinzi walicheza vipi, tatizo la kiungo na ushambulizi limekaaje.

Maana yake iko hivi, ili kupata majibu sahihi wakati wa dirisha dogo na dira ya nini cha kufanya. Benchi la ufundi linapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi ya kufanya uamuzi wa kipi cha kupunguza au kuongeza na isiwe viongozi wenye matakwa au kero zao ndiyo wageuke kuwa makocha.

Lengo hasa ni kutaka kuwakumbusha viongozi wa timu yoyote ile inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwamba suala la dirisha dogo la usajili, zaidi linakuwa ni ‘mali’ ya benchi la ufundi kwa kuwa ndilo limeona kwa ukaribu zaidi kilichopungua na wana nafasi kubwa ya kujua mahitaji kwa maana ya kipi hasa kinachotakiwa kuongezwa.

Kama viongozi watachukua nafasi kubwa kwa kuwa wao ndiyo wanao waongoza makocha na benchi la ufundi basi watakuwa hawatendi haki na ikiwezekana watakuwa wanazuia kazi ya kiufundi ya makocha kufanyika katika misingi ambayo ni sahihi.

Lakini kama makocha nao watakuwa waoga, pia watakuwa wanaiangusha taaluma yao kwa kuwa kama watapelekewa mchezaji wanayeamini hana msaada kwao na baadaye kweli akafeli, basi mwisho wao ndiyo watakaoanguka na viongozi watakaa kando na kuwa sehemu ya wale wanaowasema wao kwamba wameshindwa.

Dirisha dogo, kazi yake ni kuimarisha. Hivyo huu ni wakati wa timu hizo kujiimarisha kupitia upungufu waliopitia katika mechi tisa za Ligi Kuu Bara na halitakuwa jambo la mzaha kama alivyofanya Dk Louis Shika wakati alipokwenda kununua nyumba za mfanyabiashara Said Lugumi zilipokuwa zinapigwa mnada.

Dk Shika alikubali kununua nyumba za Lugumi kwa zaidi ya Sh bilioni tatu akijua hana. Wakati mnada ukiendelea, alisema “Nafikiri 900 itapendeza zaidi.” Baada ya hapo msemo huo ndiyo umekuwa gumzo kila sehemu na hasa mitandaoni.

Faida ya msemo huo sasa ni utani na utaona, Dk Shika alikwenda kufanya mzaha katika jambo ambalo wahusika hawakuwa wakihitaji utani zaidi ya kuhakikisha wanaifanya biashara kwa kuwa suala hilo halihusishi utani.

Ndiyo maana nawasisitiza viongozi kuwa, wakati wa dirisha dogo la usajili, wanapaswa kuwa makini sana na utani wa Dk Shika kwa kuwa baada ya dirisha hilo, basi hakutakuwa nafasi ya mabadiliko hadi mwishoni mwa ligi.

Kama nafasi ndiyo hii, basi hakutakuwa na mzaha hata kidogo na vema mambo yakaenda kitaalamu na kuangalia kile kilicho sahihi kwa kuwa hakutakuwa na nafasi nyingine tena ya kufanya marekebisho.

Matakwa binafsi, mihemko, kufanya mambo ili kupata bakshishi, lisiwe jambo litakalopewa kipaumbele badala yake umakini kwa njia za kitaalamu ndiyo upewe nafasi ili kufanikisha kinachotakiwa kubadilishwa.

Nimeamua kuwakumbusha hivi kwa kuwa mara nyingi sana tumeona timu zikifanya mabadiliko wakati wa dirisha la usajili lakini baada ya dirisha kufungwa na zenyewe kuwa zimefanya mabadiliko, mambo yanakuwa afadhali ya jana. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic