November 24, 2017




Na Saleh Ally
UKIIANGALIA juujuu Ligi Kuu Bara utaweza kuona kama vile mambo ni kawaida na kila kitu kinakwenda vizuri lakini kuna mambo mengi yanayoanisha kuwa ina matatizo mengi ya kiufundi.

Siku chache zilizopita niliandika makala kuelezea namna ambavyo kuna malalamiko ligi kuwa ngumu. Nikaeleza kuwa makosa mengi kutoka kwa waamuzi yamepungua hivyo hakuna “mchekea”, hivyo kama ni kula lazima iwe kwa jasho.

Kawaida waamuzi wanapokuwa na uamuzi sahihi kwa zaidi ya asilimia 90, lazima ushindani unaongezeka na kufanya ugumu kuongezeka na ushindi unakuwa na shida.

Bado ubora wa wachezaji na makocha kwa maana ya mbinu, ndiyo unakuwa ukombozi wa timu pale mambo yanapokuwa magumu. Ubora hushinda ugumu kwa kuwa kila unapozungumzia bora katika soka, maana yake ni hesabu.

Kwa asili, mchezo wa soka ni hesabu kila jambo lake. Anza na vikosi ni hesabu, kujipanga uwanjani au utoaji pasi pia ni hesabu. Hata mabao ni hesabu na matokeo ya mchezo huo ni hesabu kama unapozungumzia uchezaji kwa maana ya takwimu.



Kuwa na hesabu katika kila kitu, kumeufanya mchezo wa soka kuwa tofauti kabisa na ukiangalia katika Ligi Kuu England unaweza kujifunza mengi na ligi hiyo bora kwa maana ya umaarufu na ushindani uwanjani inaweza kuwa mfano.

Ligi hiyo maarufu kama EPL, ina timu 20 lakini hadi sasa kila timu imecheza mechi 12 na huku nyumbani katika Ligi Kuu Bara, kila timu imecheza mechi 10.

Jumla ya mechi 160 zimechezwa hadi mzunguko wa 10 wa Ligi Kuu Bara. Kinachoshangaza kwamba ni mabao 135 tu yamefungwa na hii inaonyesha kuna tatizo kubwa katika mambo mawili makuu. Kama ni wastani maana yake hakuna hata uhakika wa bao moja katika mechi moja na hiki ni kiwango cha chini sana katika ufungaji. Maana yake, washambuliaji au wanaohusika na ufungaji, hawana kiwango bora.

Tatizo la kwanza ni wafungaji wenye uwezo wa juu katika vikosi 16 vinavyocheza Ligi Kuu Bara lakini inawezekana pia kuna tatizo kubwa la makocha wenye uwezo mkubwa wa kubadili mbinu za washambuliaji ili waweze kufunga mabao mengi zaidi.

England wamefunga mabao 270 baada ya kila timu kucheza mechi 12 ambazo hazina tofauti kubwa sana na zile za Tanzania Bara. Sote tunakubaliana kwa EPL kuna wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa ambao unatokana na mafunzo bora.

Ufungaji ni kipaji, lakini watu wanafundishwa kufunga kwa ubora wa juu. Tunajua kuwa EPL ni ligi ngumu sana na kama ubora wa ligi kigezo ni ugumu, basi huenda hadi sasa England wangekuwa hawajafikisha hata mabao 100.

Difensi zao ni bora kwa kuwa zinalindwa kwa mifumo bora ya viungo na walinzi na pia makipa wenye viwango bora kabisa. Washambuliaji wao wamekuwa na viwango vya juu zaidi na kuweza kufunga mabao mengi zaidi.

Hivi karibu, sehemu nyingi ambako soka limepiga hatua walichofanya ni kuanzisha kozi za makipa kuwapeleka katika mifumo bora ya ulinzi na ya kisasa. Wanafanya hivyo kwa kuwa washambuliaji wamekuwa wakipewa mbinu mpya na kisasa wakati makipa wanaendelea kubaki na mbinu za kizamani.

Kwa kiwango cha washambuliaji tulionao, si rahisi kufananisha na wale waliopo England. Unaweza kuwa mfano halisi kwamba wastani wa mabao ya kufunga unaweza kuwa chini kwa kuwa wafungaji wabunifu ni wachache.

Washambuliaji wengi hucheza kwa kutumia vipaji vyao badala ya mafunzo maalum. Utaona mafunzo ya makocha wengi ni kupiga mashuti, penalti, faulo lakini ni aghalabu kusikia kuna darasa la washambuliaji.

Ulaya kama Arsenal au Manchester City, zimebadili hata aina ya ukaaji wanapokuwa vyumbani kwa kuwa wanataka kila kitengo kikae pamoja na washambuliaji mara nyingi wanakuwa pamoja. Lengo ni kufanya wawe na mawasiliano.

Ukiachana na wafungaji, viungo ambao wanafanya kazi za kuwalisha mipira, pia wana viwango vya juu kwa maana ya vipaji lakini mafunzo bora ambayo yanawafanya kurahisisha mambo kwa wafungaji wao.

Angalia mchezaji kama Robbie Brady wa Burnles amepiga krosi 94 katika mechi 12 au Kevin De Bruyne aliyetoa pasi za utelezi “through” 15 katika mechi 12.

Ukiangalia idadi ya pasi hizo za utelezi za De Bruyne, hapa nyumbani unaweza kupata kisingizio cha viwanja kwamba ni vichache. Lakini uliza pasi ndefu ni ngapi zilizopigwa na kufika. Lakini krosi 94 kapiga mchezaji mmoja, jiulize hapa nyumbani kwa idadi hiyo unaweza kukusanya timu au wachezaji wangapi kuzifikia?

Ubora ni kitu cha mjumuisho, kinachukua vitu vingi kutengeneza neno hilo moja “bora”, tena hasa linanapokuwa suala la ujumuisho, yaani timu.

Ni suala la kujiuliza kwa kila mshambulizi, kwamba kweli ana kipaji lakini ana mafunzo. Kama hayapo, yeye binafsi anafanya kazi ipi ya ziada kujiongeza na kujitengeneza kuwa bora zaidi.

Tabia za kuamini England ni bora na Tanzania haiwezi kuwa bora ni kosa kubwa. Ubora wao unaweza kuwa juu lakini kujifunza kupitia wao na mifumo mbalimbali mipya inayotolewa na walimu, kuna uwezekano wa kutengeneza ubora ndani ya Tanzania.

Hadi sasa mshambuliaji anayeongoza kwa kufunga mabao ana mabao nane, anayemfuatia ana sita na wote wawili wameishapiga hat trick. Hii pia inaonyesha namba ambavyo ufungaji unasuasua.

Ufungaji wa timu nyingi kupitia wafungaji wake, unaweza usiwe ni watu wanaolenga zaidi kufunga badala yake wakataka kuonyesha kucheza mpira wa mbwembwe ambao unafurahiwa zaidi nchini.

Kuna tofauti kidogo unapowaona Emmanuel Okwi wa Simba na Obrey Chirwa. Kweli wanataka kufunga, wanakimbia kwenda kufunga, wanataka kujaribu kufunga na hawachoki kurudia.

Mwingine anaonekana hivyo ni John Bocco ambaye kweli amepania kufunga na ukiomuona anacheza utaona kweli anataka kufunga ndiyo maana amekuwa kero kwa mabeki wa timu nyingi za Ligi Kuu Bara. Ibrahim Ajibu wa Yanga na Shiza Kichuya wa Simba au Mbaraka Yusuf wa Azam FC.

Kuna Mohammed Rashid wa Prisons mwenye mabao sita pia ingawa anaanza kuonekana kama kupoteza kasi yake. Hili limekuwa tatizo jingine, kwamba anayeanza kufunga kwa kasi, akipaniwa basi “anapaki”.

Ubora wa mfungaji, anazidi kuwa bora kila anapopaniwa. Naye anakuwa anajipanga kimafunzo akitumia kipaji chake lakini nia ya kutaka kufanya vizuri na kutokubali kushindwa.

Kweli mazingira ya England ni tofauti na Tanzania Bara, lakini ubora katika eneo lako kwa kuwa ndiyo mazingira yako, ni muhimu kwa kuwa hauwezi kuamuliwa ulichonacho kwa kuangalia matokeo ya England.

Takwimu za Bara zinaonyesha, kuna wafungaji wazuri na wanaweza kufunga, lakini hawana mafunzo mazuri na wao wanapungukiwa mambo kadhaa.

Mfano kila wanapobanwa wanashindwa kukurupuka, huenda wangefanya vizuri zaidi kama wana mafunzo bora lakini jiulize wanaowanoa wana mafunzo hayo kitaalamu? Wamebobea katika eneo hilo au kwa kuwa ni makocha tu, basi wanaweza kufanya kazi hiyo?

Mengi kama viwanja yanaweza kuwa sababu ya kutuangusha, lakini tukiyatumia kama ngao na sehemu ya kukubali tuna mattaizo na hatuwezi kuamka. Basi mwisho katika mechi 160, yatafungwa mabao hata 20 na tukaendelea kuvibeba visingizio hivyo.

Kuna kila sababu ya washambuliaji kutafakari pia kwamba walipo sasa ni sahihi, wafungaji bora kuwa na mabao 19 ni sawa? Pia waangalie kama wanaridhika.


Walimu pia, wanajiongeza na kujifunza mbinu mpya za ushambulizi wanazoweza kuwapa washambuliaji wao ili wafanye vema zaidi au kuwaimarisha kutoka walipo na kwenda? Au wanasubiri wanapoishia na wao wanakuwa wamegota walipo?

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic