December 23, 2017



Kocha wa Simba, Joseph Omog, amempiga mkwara beki Asante Kwasi kwa kumpa masharti ili aweze kupata nafasi kikosi cha kwanza huku sharti la kwanza likiwa ni kujituma kwa juhudi.

Omog, raia wa Cameroon, amemwambia Kwasi raia wa Ghana kwamba, hataangalia umaarufu wa mchezaji katika kupanga kikosi chake huku akitaja kigezo anachokiangalia ni uwezo pekee.

Kocha huyo alitoa kauli hiyo juzi mara baada ya mazoezi ya Simba kumalizika kwenye Uwanja wa Boko Beach Veterani jijini Dar es Salaam.

Kwasi ni miongoni mwa wachezaji ambao wamesajiliwa na Simba kwenye usajili wa dirisha dogo lililofungwa Desemba 15, mwaka huu. Mwingine aliyesajiliwa ni mshambuliaji Antonio Domingos.

Omog amesema amepata taarifa za kusajiliwa wachezaji wawili, lakini akasisitiza kuwa anataka kuwaona wakipambana mazoezini ili wamshawishi awape nafasi kikosini.

“Kwasi na Domingos ndiyo wachezaji wetu wapya, hawa wamesajiliwa na uongozi, hivyo nitakuwa katika nafasi nzuri ya kuwazungumzia nikikabidhiwa rasmi.

“Lakini niseme tu, hao wanakuja Simba lakini wajue kwamba mimi siangalii ukubwa wa jina la mchezaji au nchi aliyotokea katika kupanga kikosi changu, hivyo ili apate nafasi ya kucheza sharti langu la kwanza ni kujituma kwa bidii anishawishi kwa kunionyesha kiwango kizuri uwanjani.

“Hilo ndilo sharti langu la kwanza ili mchezaji acheze, sharti la pili ni nidhamu ya ndani na nje ya uwanja ambayo ndiyo msingi bora wa mchezaji.

“Nawakaribisha wachezaji hawa wakiwa wanafahamu hayo masharti hivyo wasiogope, waje wafanye kazi kwa mafanikio,” alisema Omog.

Omog alisema, katika timu yake anataka kuona ushindani wa namba ukiongezeka pale mchezaji anapopata nafasi ya kucheza, hivyo Kwasi na Domingos wanatakiwa kuonyesha viwango vyao.


Aliongeza kuwa, anawasubiria wachezaji hao wapya waliosajiliwa na viongozi kwa ajili ya kuona uwezo wa kila mmoja kwenye mazoezi ya timu hiyo mara baada ya kuripoti.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic