Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Ammy Ninje ameibuka na kuweka wazi kuwa Watanzania wanatakiwa wamsamehe kutokana na kile kilichotokea kwa kikosi hicho wakati wakiwa nchini Kenya walipokwenda kushiriki michuano ya Chalenji.
Ninje alipewa mikoba ya kuiongoza Kili Stars kwenye michuano hiyo ambapo mpaka waliporudi jijini Dar jana alifanikiwa kutoka sare mchezo mmoja tu na kupoteza michezo mitatu ya Kundi A, jambo ambalo liliwafanya washindwe kupata nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali.
Ninje aliyewahi kuinoa timu ya vijana ya Hull City ya England, amesema kuwa kwa sasa Watanzania hawana budi kumsamehe yeye pamoja na kikosi kizima kutokana na kushindwa kutekeleza kile ambacho walitumwa.
“Kiukweli mimi nawaomba Watanzania wanisamehe tu kwa sababu tumeshindwa kuwa wawakilishi wazuri kwenye michuano hii ya Chalenji baada ya kupoteza mechi na kutupwa nje, japo tulipanga kufanya vizuri.
“Kikubwa tumejifunza mambo mengi ambayo yatakuwa faida kwa timu hii kwenye mashindano yajayo ila kwa sasa ukweli ndiyo huo kwamba tumeshindwa kurudisha yale matokeo ambayo mashabiki wa soka walikuwa wanayatarajia kutoka kwetu,” alisema Ninje.
0 COMMENTS:
Post a Comment