December 11, 2017


Kocha Msaidizi wa Simba, Mrundi, Masoud Djuma, amesema kuwa, kwa muda mchache aliokuwa akimfanyia majaribio straika Mzambia, Jonas Sakuwaha, amemuona anafaa kusajiliwa kikosini hapo, hivyo kilichobaki kamati kufanya kazi yake.

Mzambia huyo ambaye alianza majaraibio wiki mbili zilizopita, Ijumaa iliyopita alifunga bao moja katika ushindi wa 3-1 walioupata dhidi ya KMC katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar.

Akizungumzia uwezo wa mchezaji huyo, Masoud alisema: “Kabla ya hapo sikuwahi kumuona, lakini nilipokabidhiwa ndiyo nikaanza kuuona uwezo wake.

“Nilikuwa nampeleka uwanjani kufanya mazoezi wakati timu ilipokuwa mapumzikoni, alianza taratibu lakini kila siku zilivyokuwa zinakwenda akawa anazidi kuwa vizuri.

“Inaonyesha anaipenda sana kazi yake na hicho ndicho kimemsaidia mpaka nikamuona anatufaa. Ni mzuri katika kujiweka kwenye nafasi kutokana na nafasi anayocheza, ni nadra kwake kupoteza mpira akiwa nao, lakini pia ni msumbufu kwa mabeki. Sasa mchezaji kama huyo ndiyo anahitajika.

“Mimi kazi yangu ilikuwa ni kumuangalia uwezo wake na nimeridhika naye, hivyo naiachia kamati ifanye kazi yake, kwa upande wangu hana shida yoyote, akisajiliwa atatusaidia.

Endapo Mzambia huyo atasajiliwa, ina maana kwamba Simba itatakiwa kupunguza mchezaji mmoja wa kimataifa kwani hivi sasa wapo saba.


Alipoulizwa Mrundiu huyo ni nani atapunguzwa ili Mzambia huyo asajiliwe, alisema: “Hiyo siyo kazi yangu, uongozi ndiyo unajua, lakini mpaka usajili utakapofungwa atajulikana ni nani tunamuacha kwa sababu mchezaji kuhama timu ni kawaida.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV