December 11, 2017



NA SALEH ALLY
MICHUANO ya Chalenji inayoendelea nchini Kenya imezua mjadala mkubwa sana yakiwemo mambo mengi ambayo huenda ilikuwa vigumu kuyatarajia kwamba yanaweza kutokea.
Timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ndiyo iliyosababisha mjadala huo hasa baada ya kupoteza mechi mbili katika tatu za michuano hiyo.

Kilimanjaro Stars imetoka sare na Libya lakini baada ya hapo, imepokea vipigo vinavyofanana vya mabao 2-1 kutoka kwa Zanzibar Heroes na baadaye Rwanda maarufu kama Amavubi

Kibaya zaidi, katika mechi zote mbili, Kilimanjaro Stars imetangulia kufunga na baada ya hapo, Zanzibar na baadaye Rwanda walisawazisha na kuimaliza kabisa. Hivyo Kilimanjaro Stars ndiyo kibonde mkuu katika Kundi A la michuano hiyo baada ya kuambulia pointi moja ndani ya mechi tatu.

Pamoja na hivyo, Kocha Mkuu, Ammy Ninje ameonekana si mtu anayejuta na lolote na huenda angependa mambo yaonekane ni kama Ulaya vile ambako amekuwa akiishi kwa kusema: “Until next time”, yaani hadi wakati mwingine tena.

Ninje alisema neno hilo wakati akihojiwa baada ya Kilimanjaro Stars kufungwa na Rwanda katika mechi ya juzi. Kibaya zaidi alisisitiza kwamba alijivunia uchezaji wa kikosi chake bila ya kueleza hata kosa moja au kitu ambacho aliona kilimkwamisha.

 Nimeona miijadala mingi, wengi wakilalamika na Kingereza chake kuonyesha kuwakera, kwangu si jambo la msingi sana ndiyo maana hata hiyo “Until next time”, zaidi naizungumzia katika lugha yetu ya Kiswahili kwamba Watanzania wamechoshwa na kauli hiyo kwa kuwa wameipita sana wakiwa wanasubiri mafanikio bila ya mafanikio.

Watanzania tumechoshwa na matarajio yasiyofikiwa, tumekuwa tukiahidiwa na mambo yanabaki vilevile. Hii nazungumzia katika uongozi uliopita, mwingine na mwingine.

Huenda Ninje anaona kawaida tu kwa kuwa hayajui machungu yetu na amekuwa akiishi Uingereza si Tanzania. Inawezekana kabisa anaamini ndiyo tunaanza kufikia hapo au kuanza kupambana kwa ajili ya mabadiliko kwa kuwa hakuwepo.

Niliwahi kuzungumza na Ninje wakati ule tulipoelezwa mchezaji kutoka England alikuja kuitumikia Taifa Stars chini ya Mshindo Msolla, lakini baadaye ikagundulika hakuwa na kiwango na akashindwa hata kuitumikia timu hiyo.

Sitaki kuhoji uwezo wake kwa nini alipewa Kilimanjaro Stars kama inavyoelezwa alikuwa akifundisha timu za watoto. 

Lakini lazima hata TFF wapime mambo kwamba Ninje hajawahi kufundisha soka la ushindani kwa maana ya klabu mfano Ligi ya Mabingwa au hata timu nyingine za taifa.
Amewekwa Kilimanjaro Stars kama mwanafunzi tu, inaonekana wazi anajifunza mapya na kujua soka la Afrika.

Lakini naona huenda alikuwa mcheshi na mtu mwema kwa uongozi wa TFF, hivyo ungependa kumfurahisha pia kwa kuamua kumpa nafasi hiyo ambayo itamtengenezea CV atakaporejea Uingereza na kutaka kufundisha timu ya huko.

Naona si sahihi kuitumia Kilimanjaro Stars kama sehemu ya kumtengenezea Ninje CV yake ili afanikishe mambo yake hapo baadaye wakati Watanzania tunaendelea kuogelea maumivu jambo ambalo si sahihi hata kidogo.

Ukiangalia kikosi cha Kili Stars, wachezaji hawakucheza kwa morali na sidhani kama walikuwa wakiamini kweli wana mtu sahihi mbele yao ambaye alikuwa akiwaongoza. Huenda hata wao wanapokuwa wanaingia uwanjani pia walikuwa wakikerwa na Kingereza kingi cha mchanganyiko na mazungumzo kwa mwendo wa majivuno.

Wao pia nawaona hawakuwa sahihi, hata kama ni hivyo bado walipaswa kujua Tanzania Bara si mali ya Ninje wala TFF. Hivyo walipaswa kufanya kazi zao kwa juhudi kubwa na kuhakikisha mambo yanafikiwa.

Mnatuangusha, mnatuumiza na “Until next time”, zimepita nyingi na sasa tunachotaka ni mafanikio kwa kuwa Tanzania haiwezi Afrika, haiwezi dunia na hata Afrika Mashariki na Kati kweli sisi tuwe ndiyo akina Sudan Kusini?






1 COMMENTS:

  1. WAKALE BHANA...WANAJUA SANA:---
    La Kuvunda Halina Ubani, Mgaagaa na Upwa Hali Wali Mkavu, Mzalau mwiba mguu huota tende, Ukitaka cha Uvunguni Sharti Uiname, Ategemeae cha Nduguye Hufa Maskini...Na Ganda la Muwa la Jana Chungu kaona Kivuno.

    Hizi ni sentensi nyingi za majuto na kujifariji...hatuna kipya..kukiwa na wachezaji wazuri basi tunakosa kocha mzuri. Tukiwa na wachezaji na kocha wazuri magumashi yatatokea kwenye uongozi. Hii ndio soka ya Tanzania. Wengi magumashi..tunapeana vyeo kwa kujuana. Hata mimi leo ukinipa timu siwezi rudi kwa aibu hiyo. Kwanza nawajua wachezaji wa kazi, wachezaji wa kuchezea mpira..najua kila mtu na namba yake..na najua ili niende kwenye mashindano ni aina gani ya mpira wa kucheza. Naheshimu kazi iliyofanya na kila kocha aliyepita pale kwenye timu ya Taifa. Mi nikwambie...hata Mayanga hana sifa ya kuwa kocha wa Timu ya Taifa.

    Usijisifie na kucheza na Botswana au Malawi Muda wote...tukampa ujiko. Tena ni ni mechi za majaribio. Nikwambie...utamsifia Mayanga kwa kile alichofanya pale South Africa kwa kushika nafasi ya Tatu (3) ila angalia sisi tulikuwa na kikosi gani na wenzetu walikuwa na vikosi gani.

    Ninje kamkuta Mayanga...na hiki ni kikosi cha Mayanga na wala si cha Nje. Muulize Ninje kamuita mchezaji gani yeye kama yeye zaidi ya kupewa kile kile na kuongezewa baadhi ya wachezaji.

    PENDEKEZO:
    Ni wakati sasa wa kufanya vitu kwa siriasi na kuacha kubebana. Tunahitaji matokeo bhana...piga hesabu watu milioni hamsini hatuna kikosi cha kwanza cha Timu ya Taifa chenye wachezaji 25...ni aibu. Ninje nae alitaka aende kwenye mashindani asifungwe...au alitaka timu icheze mpira akapishana na Mayanga

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic