December 11, 2017



Uongozi wa Klabu ya Yanga umefunguka kuwa unakumbana na changamoto nyingi katika kuendeleza ukarabati wa uwanja wake wa Kaunda kutokana na gharama kubwa za vifusi pamoja na mvua kuendelea kunyesha hivi sasa, hivyo kusababisha kuwa katika wakati mgumu.


Yanga ipo katika mchakato wa kutengeneza uwanja wake wa Kaunda uliopo makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo maeneo ya Jangwani jijini Dar es Salaam, ili uweze kutumika kwa ajili ya mazoezi kwa wachezaji.

Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema zoezi la ujenzi wa uwanja wao limeonekana kuwa gumu kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo na kudai kuwa wanajitahidi kuhakikisha wanazipatia ufumbuzi ili kufanikisha zoezi hilo kwa wakati.

“Kuna changamoto nyingi ambazo tunakumbana nazo katika maendeleo ya ujenzi wa uwanja, vifusi vimekuwa havipatikani, tumekuwa tukisaka kila mahali na pale tunapovipata inakuwa ni gharama kubwa kuvifikisha hapa klabuni.

“Mvua pia imekuwa kikwazo kikubwa kufanikisha zoezi letu hilo la upatikanaji wa vifusi, lengo letu ni kuhakikisha tunafanikiwa kumaliza ndani ya wakati lakini changamoto hizo zinatukwamisha, tutaendelea kupambana nazo.


“Kuhusu gharama ambazo tutazitumia kutengeneza uwanja hadi sasa bado hatujazifahamu, kwani mchakato wa awali uliopo ni kujaza vifusi kisha hapo baadaye ndiyo tutajua tutatengeneza uwanja wa aina gani na kufahamu gharama halisi, tuna mainjinia wengi pamoja na wadau mbalimbali ambao wataweza kufanya mchakato huo wa mchanganuo wa ujenzi wa uwanja kwa ujumla,” alisema Mkwasa.

SOURCE: CHAMPIONI

1 COMMENTS:

  1. SIJUI ILA NGOJA NIAMINI.....::
    Kwa akili zangu ndogo na uwezo wangu wa kufili..niliamini kabisa Yanga inaweza kufanya kitu zaidi ya hiki kinachofanyika.

    Unajua kwanini???
    Huwezi sema Yanga hawawezi pata eneo la ekari kuanzia kumi kwa gharama inayotumika kujaza vifusi pale Jangwani. Jangwani patabaki kuwa Jangwani ila si lazima uwanja ujengwe pale.

    Ningekuwa Kiongozi:
    Moja ya kitu ambacho ningefanya ni kununua eneo linaloweza kuwa na ukubwa wa kuanzia ekari kumi (10) nje ya mji. Naamini maeneo yaliyo nje ya mji tunaweza kupata kuanzia milioni tano (5,000,000/=). Kwahiyo ekari kumi ni kiasi cha milioni hamsini (50,000,000/=) hayo ni makadilio yangu na inawezekana tukapata chini ya hapo. Uwanja wa mpira unaweza kubebwa na eneo la ekari nne (4) wenye uwezo wa kuchukua watu kuanzia elfu ishirini (20,000). Pichi (Pitch) inaweza kujengwa kwa wastani wa milioni kuanzia 600,000,000/= kutegemea na ubora wa pichi yenyewe. Nikijumuisha majukwaa na mazaga mengine uwanja unanitimia. Kikubwa nilitaka kuonesha ukuwa wa eneo la uwanja tu.

    Ekari sita (6) zitakazobaki nitajengwa viwanja viwili vya mazoezi kwa kila ekari mbili mbili. Kiomoja kwa ajili ya Nyasi Bandia na kingine ni kwa ajili ya nyasi halisi.Ekari mbili zitakazobaki zitajenga Hostel, Swimming, pamoja na Eneo la Gym.

    Kwanini Tunateseka??
    Viongozi wengi si wabunifu. Yanga ni Taasisi na si ofisi ya mtu mmoja. Ukiondoka wewe anakuja mwingine ataendelea kuongoza.

    Kwanini nimesema hivyo??
    Unaweza kutumia rasilimali zilizopo kupata mkopo wa kujenga alafu mdhamini akawa ni TFF ili kila mechi tutakayocheza itakatwa hela kadhaa ili kurudisha mkopo husika. Tutumie Benki kwa ajili ya kuchukua mkopo wa ujenzi ili tujenge hivyo vitu tulivyosema. Tushirikishe wadau kupata fedha kwa ajili ya ununuzi wa Eneo tuachane na Jangwani. Jangwani tupakarabati patumike kama Hotel pamoja na Jengo la Mafya. Maeneo haya yataweza kutuingizia pesa zaidi kuliko kuwaza uwanja kuweka pale.

    Mwisho:
    Ushauri wangu kwa mjomba angu Mkwasa...Naheshimu sana kazi uliyoifanya, unayoifanya na utakayoifanya. Wewe ni mbunifu ila fanya kile kinachowezekana. Fumba macho usiogope lawama. Hapo hapawezekani mzee wangu. Ukijenga wewe wananchi wa eneo litakalozunguka lazima nyumba zao zitakwenda kwa kuwa wapo bondeni. Angalau kuna mahitaji mengi ya Kilabu ila tuanze na wadau kununua eneo nje ya mji. Kama watu wanasafiri na Timu kwenda Songea hatuwezi shindwa kwenda Goba, Kiluvya na hata Kitunda kuangalia mpira.

    Tuangalie eneo linalowezekana...fungua akaunti yetu ya kuchangia. Kila mshabiki na hata mwanachama akiweka elfu moja (1000/-) endapo watakuwa elfu hamsini (50,000) tutapata milioni hamsini (50,000,000/=). Hatuwezi shindwa kufanya makubwa

    Naomba Kuwakilisha

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic