Uongozi wa Singida United ya mkoani Singida umempa jukumu kocha mkuu wa timu hiyo, Hans Pluijm kuhakikisha anafanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo.
Singida United imeteuliwa kushiriki michuano ya Mapinduzi kwa mara ya kwanza inayotarajia kuanza kutimua vumbi Desemba 29 huku ikitarajiwa kuanza kufungua dimba na Mlandege katika mchezo utakaochezwa saa 8:30 mchana.
Singida ambayo imepanda daraja msimu huu itashiriki Mapinduzi kwa mara ya kwanza ikiwa kundi moja na Yanga, Mlandege, Taifa Jangombe, Zimamoto na JKU ambazo zipo Kundi B huku Kundi A zikiwa timu za URA, Jamhuri, Mwenge, Simba na Azam FC.
Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga, amesema kuwa, lengo lao kubwa ni kuona wanafanikiwa kutwaa kombe hilo, japokuwa ni mara yao ya kwanza kushiriki katika michuano hiyo, hivyo wanahitaji kufanikiwa kufanya vyema.
“Tunashukuru kuitwa kushiriki michuano ya Mapinduzi na ni jambo la kheri sana, tutakwenda kwenye michuano kwa ajili ya kupambana na si kushiriki japokuwa itakuwa ni mara yetu ya kwanza.
“Tunahitaji kombe hili pia liweze kutua Singida kwa mara ya kwanza, tunaitumia michuano hii kama maandalizi kwetu kwa ajili ya ligi kuu na hatuendi kwa ajili ya kujifurahisha.
“Kikosi chetu kipo vizuri, tunaamini uwezo wa kutwaa kombe hilo upo chini ya kocha wetu Hans Pluijm,” alisema Sanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment