December 18, 2017




NA SALEH ALLY
UKIFUATILIA usajili wa Ulaya, utagundua kumekuwa na uwazi katika mambo mengi sana tofauti na nchi za Afrika na hasa hapa nyumbani Tanzania.

Kawaida kunapokuwa na usajili, tumeona namna watu wanavyokuwa wazi kila jambo likiwekwa wazi na hata kiasi gani cha malipo kinatakiwa na timu fulani inataka kulipa na nyingine haitaki.

Hata kama mjadala wa biashara utaendelea hadi mwafaka utakapofikiwa, basi kila kitu kitakuwa wazi hadi mchezaji husika atakapojiunga na timu yake mpya.

Hali hii imekuwa ikiusaidia sana mpira wa Ulaya na kwingineko ambako wamekuwa wazi kwa mambo mbalimbali, lakini nitakueleza haya mawili.

Kwanza ni mchezaji mwenyewe, anapojua kuwa watu wanajua ni kiasi gani amenunuliwa, atakuwa anapambana kuhakikisha anafanya vema ili kuwaonyesha hiyo ni thamani yake au wakati mwingine yeye ni zaidi.

Kuna wataalamu na mitandao mbalimbali ya Ulaya ambayo huwapa wachezaji thamani nao wanalijua hilo. Hivyo kila wanapocheza, pamoja na kuisaidia timu hulenga kupandisha thamani yao kwa kufanya kazi yao kwa juhudi na maarifa. Hapa kunakuwa na msaada mkubwa kwa mchezaji mwenye.

Pili ni suala la mijadala. Hauwezi ukaukimbiza mchezo wa soka mbali na mijadala, hauwezi ukatengeneza njia tofauti ili ipite nje ya mchezo huu, ni kupoteza tu muda. Badala yake vizuri kutengeneza mjadala sahihi unaokuwa unasaidia afya ya mchezo wenyewe.

Ukifuatilia mijadala ya soka Ulaya inakuwa na nafasi kubwa ya kuusaidia mpira wao kwa kuwa mambo yako wazi na watu wanaweza kuhoji thamani ya mchezaji na msaada wake.

Unapoweka ushabiki pembeni na kujadili kitu kwa vipimo sahihi basi unakuwa umeisaidia mpira. Hapa nyumbani, ushabiki maandazi umewaongoza wengi kuwa wajinga na kujikuta wakijadili ubora pekee na kukimbia upungufu wa klabu zao wakiamini wanazilinda, kumbe ndiyo wanazididimiza.

Haya mambo mawili hayapatikani hapa nyumbani kwa kuwa siri ni utamaduni wetu hata pale uwazi unapokuwa unahitajika. Kama klabu imetoa kitita cha usajili, ina haja gani ya kuficha?

Tunakubali hata Ulaya, wanafanya hivyo katika baadhi ya wachezaji au matukio na utagundua ni kwa asilimia takribani kumi tu. Wakati hapa nyumbani usajili ni siri kwa asilimia 99.

Mohamed Salah wa Liverpool, sasa ana mabao 13 anaongoza wafungaji wa Ligi Kuu England. Wakati Liverpool ilipotakiwa kuipa AS Roma kitita cha pauni milioni 34, wengi walipinga wakiona hakuwa akistahili dau hilo kubwa na wao Liverpool wakaona sahihi.

Leo hakuna anayeilaumu Liverpool kwa kuwa inaonekana ilikuwa sahihi na sasa thamani ya Salah inaonekana ni zaidi ya hapo kutokana na kazi yake nzuri.

Mjadala kama huu, unaweza kuanzisha na mwingine kwa manufaa ya mpira au unaweza kubadili akili ya watu wengine katika jambo jingine.

Usajili wa nyumbani si kweli kuwa siri inatokana na wachezaji au viongozi kuficha yaliyo katika mikataba. Lakini ujanja ujanja wakati wa usajili na baadhi ya wahusika kufaidika, imekuwa ikichangia mambo haya kutokea na kuendelea kila siku.

Viongozi wa klabu wamekuwa wakifaidika kwa asilimia kubwa na usajili wa wachezaji wanaojiunga na timu zao ingawa wengi wanatumia maelezo mengi kutaka kuonekana ni wasafi.

Faida kwao, imekuwa ni hasa kwa mpira wa Tanzania. Lazima tukubali kuwa wale wanaoongoza klabu za wanachama wawe wazi, waache longolongo na kutaka kuonyesha wanalinda maslahi ya klabu kumbe ndiyo wanaomaliza kila kitu kwa kufaidisha matumbo yao.


Tunapaswa kuingia waliko wenzetu kama kweli tunataka maendeleo ili kuzisaidia klabu zetu na wachezaji wenyewe. Wekeni uwazi maisha yaende kwa mijadala huru na uwazi.

2 COMMENTS:

  1. KUNA UTOFAUTI MKUBWA...:
    Kuna usemi unasema "MKATABA WA KAZI NI SIRI KATI YA MWAJILI NA MWAJILIWA"...nahisi umeshawahi kuisikia hiyo sentensi na ndio kinachofanyaika hadi kwenye vyombo vya habari. Katika mfumo wa mpira ni wale wachezaji wenye majina makubwa hata Ulaya ndio angalau vyombo vya Habari vinataka taarifa kwa ajili ya kuuza taarifa kwenye vyombo vyao.

    Unajua ATSU yule wa Newcastle amenunuliwa kwa kiasi gani, lakini ukiulizwa kuhusu ZAPATA COSTA utajua..kwanza ameenda timu kubwa lakini cha pili ni mchezaji ambae tayari alikuwa na jina kubwa. Hapa kwetu unaweza usijishughulishe kutaka kujua ADEYUNI AHMED alinunuliwa kwa kiasi gani kwenda KAGERA. Ila ukataka kujua mkataba wa YOHANA NKOMOLA umeghalimu kiasi gani..unajua kwanini??kwanini taarifa ya jina la Yanga litabeba HABARI kwenye vyombo vyetu.

    Si kila mchezaji vyombo vya habari vinataka kujua au kila timu Duniani chombo cha habari kinataka kujua habari yake...ila ni pale inapotaka kufanya kazi kwa maslahi.

    Lakini pia timu zinajibu masuala ya mchezaji pale vyombo vinapotaka kujua taarifa. Angalau pia timu zetu za Tanzania zinaharibiana kwenye muundo wa usajil pale unapoweka taarifa zako hadharani. Kwa mfano..leo Simba inamtaka Banka na Yanga imesikia na fungu wanalotoa....timu pinzani ipo tayari kuharibu hilo dili kwa kuongeza mzigo. Siku hizi mpira si mapenzi tena kama walivyokuwa wanafanya wajomba zangu na baba zangu. Siku hizi mpira ni kazi. Weka dau tuondoke zetu

    ReplyDelete
  2. Brother sio kila kitu ulaya kipo wazi kihivyo kwani hata usajili wa Neymar junior kutoka kwao Brazil kwenda Barcelona uligubikwa na usiri mzito.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic