Na Saleh Ally
BAYERN Munich ilirejea tena uwanjani, jana katika Ligi Kuu ya Ujerumani maarufu kama Bundesliga baada ya mapumziko ya sikukuu mfululizo yanayotumika kama mwisho wa mzunguko wa kwanza wa ligi.
Kawaida Bundesliga ndiyo ligi pekee kubwa ya Ulaya huwa na mapumziko marefu na hii inatokana na utamaduni wa Ujerumani kuhakikisha wanaupisha msimu wa sikukuu mwishoni mwa Desemba kila mwaka.
Mara ya mwisho ligi hiyo maarufu ilikuwa imepigwa Desemba 15, StarTimes kupitia king’amuzi chao walionyesha mechi ya Bayern Munich ikishinda kwa bao 1-0 ikiwa ugenini dhidi ya VfB Stuttgart kwenye Uwanja wa Mercedez-Benz Arena.
Ushindi huo uliifanya Bayern kuzidi kujikita kileleni kutokana na kufikisha pointi 41 na mpinzani wake wa karibu Schalke 04 wakiwa ugenini kwende Uwanja wa WWK Arena wakaambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Eintracht Frankfurt na kufikisha pointi 30.
Wakati wanafikisha pointi hizo, maana yake Bayern imetengeneza pengo la pointi 11 baada ya kila timu kuwa imecheza mechi 17 za Bundesliga. Kawaida kukamilisha ligi, kila timu hucheza mechi 34.
Maana yake tayari Bundesliga iko nusu na timu sasa zinaanza kushuka mteremko katika mzunguko wa pili ambao utatoa jibu nani atakuwa mbabe na watakaomfuatia na akina nani watateremka daraja.
Ukiangalia vizuri, utaona wakati wanaanza mzunguko wa pili kwa kila timu kurudiana na mwenzake, Bayern wana nafasi kubwa tena ya kuwa mabingwa kwa kuwa walikwenda mapumziko wakiwa na pengo kubwa la pointi 11.
Hii inaweza kuwa sababu kubwa itakayowafanya kuwa na nafasi ya kufanya vizuri na huenda katika mechi 17 zilizobaki, kama watashinda 10 basi uhakika wa ubingwa unakuwa kwa asilimia 95 kwa kuwa timu hiyo ni vigumu kupoteza mechi saba katika 17.
Pamoja na kushinda au pengo la pointi kuwa kigezo cha kwanza kwamba wana nafasi ya ubingwa ipo sana, lakini kudorora kwa wapinzani wake wakubwa Borussia Dortmund ambao wataanza kutoa majibu kama wamerejea au bado vilevile watakapocheza dhidi ya Wolfsburg wao Dortmund wakiwa nyumbani Signal Iduna Park.
Hadi sasa, Dortmund wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 28, likiwa ni pengo la pointi 13 dhidi ya Bayern au Bavarians. Jambo ambalo linawalazimu kutumia nguvu za ziada huku wakiomba dua na wapinzani wao wateleze.
Hata hivyo, benchi la ufundi la Bayern, haliwezi kukubali kuona kuna kuteleza kwa kupitiliza kwa kuwa uongozi wa klabu hiyo pia hawataki utani.
Tatu utaona, rekodi za mechi 17 zilizopita, zinazibana timu tano zinazoonyesha zinaweza kuwa wapinzani wa Bayern katika kuwania ubingwa mwishoni kulingana na pointi zilizokusanya.
Ukiachana na Schalke wenye pointi 30, timu tano za Dortmund, Leverkusen, RB Leipzig na Monchengladbach, kila moja imekusanya pointi 28 na ina nafasi ya kukimbizana na Bayern hasa kama itakuwa haina mwendo mzuri katika mzunguko huo wa pili wa lala salama.
Pamoja na hivyo, rekodi ndiyo zinawaangusha kwa kuonyesha hazikuwa na mwendo mzuri hasa katika ushindi katika mechi hizo 17 zilizopita.
Katika mechi sita zilizopita, Bayern ilishinda tano na kupoteza moja na ndiyo timu pekee katika Bundesliga msimu huu kushinda mechi nne katika sita ilizocheza.
Katika mechi sita, Schalke imeshinda mbili na sare nne, Dortmund imeshinda mbili, sare mbili na kupoteza mbili. Leverkusen imeshinda tatu na sare tatu, Leipzig imepoteza mbili, sare tatu na ushindi moja tu huku Monchengladbach ikiwa imepoteza mbili, sare moja na ushindi mbili.
Rekodi hizo za ushindi, sare na kupoteza zinaonyesha ‘endiketa’ kwamba timu hizo zikiendelea na mwendo huo, mapema tu Bayern itakuwa bingwa huku ikiwa na mechi kibao mkononi.
Kiuhalisia inaonekana hata Bayern nao hawako vizuri kwa kiwango cha juu cha kutisha. Lakini wanakutana na Bundesliga ambayo timu nyingi zinaonekana zinahitaji mabadiliko.
Timu zote za Bundesliga zimeshapoteza katika mechi 17, Bayern wamepoteza mara mbili na ndiyo chache zaidi, wanafuatia Schalke na Leverkusen ambao kila moja imepoteza mara tatu.
Kiwango cha kupoteza mechi sawa ni kikubwa kwa kuwa ukiachana na timu hizo mbili zilizopoteza mechi tatu, kuna timu saba zimepoteza mechi tano zikiongozwa na Dortmund. Hivyo kama yatatokea mabadiliko ya Bayern kupoteza hata mechi mbili tu, halafu wapinzani hao wakashinda mbili mfululizo, mabadiliko yatakuwa makubwa katika msimamo.
Ingawa Bayern imeendelea kutawala, lakini kwa wanaoangalia Bundesliga kupitia StarTimes wanaweza kukueleza kwamba mechi nyingi za Bundesliga hazitabiriki kutokana na uchezaji wa ufundi na ushindani wa juu.
0 COMMENTS:
Post a Comment