Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba, Hassan Dalali amewaambia wachezaji wa timu hiyo waweke wazi kinachowasibu kuliko kuendelea kufanya vibaya wakati wanaelewa hali halisi.
Dalali ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, amewataka wachezaji hao kuweka wazi ili kuinusuru timu na matokeo mabovu hasa baada ya kutolewa katika hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.
Kabla ya Kombe la Mapinduzi, Simba ilitolewa kwenye michuano ya FA baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 na Green Warriors ya Mwenge jijini Dar es Salaan inayoshiriki Ligi Daraja la Pili.
Mara ya mwisho Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilikuwa mwaka 2012 na tangu hapo haijawahi kutwaa ubingwa huo zaidi ya kuishia nafasi ya pili msimu uliopita.
Dalali alisema; “Iwapo kuna mgogoro ndani ya Simba ni vyema ukatatuliwa na wachezaji wakae chini na viongozi wao kwa lengo la kutatua matatizo yaliyopo.”
“Wachezaji wanatakiwa waonyeshe uwezo uwanjani kwani tunahitaji ubingwa msimu huu, inavyoonekana kuna mgogoro ndani ya klabu, hivyo wachezaji waone umuhimu wa Simba wakae na viongozi wao,” alisema Dalali ambaye anaishi Tandale eneo lenye makazi mengi ya watu Jijini Dar es Salaam.
“Timu ikifungwa wanaoumia ni wanachama na mashabiki na inaonekana wachezaji hawaumii kwa haya yanayotokea Simba, hivyo wayajadili matatizo yaliyopo na kuyamaliza ili timu ifanye vizuri,” aliongeza Dalali ambaye alimkabidhi kijiti cha uenyekiti Ismail Aden Rage mwaka 2010.
Dalali alisema endapo timu itaachwa kama ilivyo, ni wazi Simba haitaweza kutwaa ubingwa wowote msimu huu licha ya kubakiwa na Ligi Kuu Bara pekee katika michuano ya ndani inayowania ubingwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment