January 22, 2018





Na Saleh Ally
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Said Salim Bakhresa aliamua kuwekeza katika upande wa vyombo vya habari kwa kuanzisha Azam Media Group ambayo imekuwa maarufu zaidi kupitia Azam TV.

Azam TV ni runinga ambayo umaarufu wake mkubwa uko katika michezo ingawa kuna mambo mengi yanaweza kupatikana katika king’amuzi chake.

Kuna filamu, tamthilia, taarifa za habari, masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kadhalika.

Pamoja na yote hayo, suala la michezo kupitia soka, limekuwa ni chachu kubwa zaidi kwa runinga hiyo ya Azam TV ambayo binafsi naona imekuwa ikipambana kwa kiasi kikubwa kabisa na sasa imeingia katika sehemu ya maendeleo ya michezo kama sehemu ya chachu.



Mfano hakuna anayeweza kukataa Gazeti Kubwa la Michezo la Championi kwamba lina mchango mkubwa sana katika michezo nchini kwa kuwa limekuwa likieleza kinachoendelea na limekuwa likikosoa au kupongeza kwa wale wanaosaidia au kuchangia kukua kwa michezo.

Kwa upande wa runinga, hakika Bakhresa na wafanyakazi wake wanastahili pongezi kubwa katika maendeleo ya walipofikia sasa tena kwa kiasi kikubwa.

Kwanza ni kuanza na Bakhresa mwenyewe kufikia uamuzi wa kuwekeza na kujikita zaidi katika michezo na leo Watanzania wanaweza kusema kuhusiana na matatizo mengi ya soka ya Tanzania kupitia yale waliyoyaona katika runinga hiyo.



Nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 1990, nilikuwa nikipiga kelele kuhusiana na Uwanja wa Sokione Mbeya ‘pichi’ yake kuwa na kokoto. Lakini Chama cha Mpira Tanzania (Fat) na baadaye TFF, hakuna aliyejali kwa kuwa hakukuwa na kile kinachoweza kuwakamatisha kama sehemu ya ukweli.

Lakini baada ya kuingia kwa Azam TV na kuanza kuonyesha mechi za Ligi Kuu Bara, nafasi ya kuyakumbushia niliyoyalilia kwa zaidi ya miaka minne ikawa imewadia na wadau wengi wakaanza kulia utafikiri ni jambo jipya na miezi sita tu ilitosha kupitishwa kwa amri ya uwanja huo ufanyiwe marekebisho haraka.

Kuna mambo mengi sana yamebadilika baada ya ujio wa Azam TV. Inawezekana yenyewe imekuwa kama chachu lakini wadau wanapata nafasi ya kuyafafanua hayo mambo wakiwa na mifano halisi kupitia suala la kuona.

Sote tunajua kwamba hata waamuzi wamekuwa na hofu ya dhuluma ya wazi kama ambayo walikuwa wakifanya awali wakijua wazi, Azam TV itaweka mambo yote hadharani na wao kuwa katika wakati mgumu. Lakini pia hiyo imewaondolea hofu waamuzi watenda haki, hawana sababu ya kuogopa tena kwa kuwa wanajua ukweli utaonekana.



Kumpongeza Bakhresa kwa kuwekeza lakini kuwapongeza viongozi wa juu wa Azam TV kusimamia maadili na kufanya mambo yaende sawasawa kwa kuwa hili si jambo dogo hasa kwa wale ambao mnajua kazi ngumu ya uongozi ilivyo.

Katika kundi la watu wengi kama ilivyo kwa wafanyakazi wa Azam TV, wako wanakuwa na nia nzuri na wengine wakitaka kujifaidisha wao ndiyo maana utaona wanarukia baada ya kuona mafanikio yanaanza kupatikana. Lakini ukweli mwisho unakuwa hauwezi kupingwa. Hapa, viongozi wanakuwa na kazi ngumu zaidi ndiyo maana nasema wanastahili kupongezwa.
Kumekuwa na masuala mengi ambayo yanastahili ukosoaji, hakika hili ni jambo zuri na kama unawakosoa Azam TV kwa nia ya kujenga linakuwa ni jambo zuri zaidi na wao hawapaswi kuwa waoga wa kukosolewa chanya kwa lengo la kuwasaidia kujua pale kunapokuwa na kasoro.



Azam TV ni mamilioni ya fedha, Watanzania wanapaswa kuiunga mkono kama chombo cha wazalendo kwa kuwa Bakhresa angeamua kuwekeza nchi jirani pekee na bado mambo kwake yakawa mazuri kama mfanyabiashara.

Kabla ya Azam TV, hakuna kampuni ya kigeni iliyowahi kuwekeza kwa kiwango cha juu namna hiyo kwa kuwa inaona vitu vya Tanzania huenda ni vya kubahatisha. Lakini Azam TV wamekubali kuingiza mabilioni ya shilingi katika soka ya Tanzania.

Binafsi nimekuwa nikitaka Simba na Yanga kuongezewa kwa kuwa ni wakubwa na wana haki kutokana na kuwa na mashabiki wengi ambao ndiyo mtaji wao. Ninaamini hata hili siku itafikia na Azam Media watalielewa na kulifanyia kazi.

Kuna athari za watu kupungua viwanjani baada ya runinga, huenda hili pia linatakiwa kufanyiwa ubunifu kutoka TFF na ikiwezekana klabu zenyewe kwamba watu wanaweza kuona mubashara na wengi wakaenda uwanjani, tunajua sote watu wanapenda soka Tanzania.

Tusiache watu wa Rwanda na Uganda wakaipenda na kuipongeza Azam TV kuliko hata Watanzania wenyewe. Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete alikwenda kuzindua Azam Media na kulisisitiza suala hilo.

Kwa wanamichezo na wapenda soka, pia wanapaswa kuliangalia hili. Bakhresa angeweza kuamua kuwekeza kwenye viwanda tu na kuachana kabisa na mambo ya michezo na vyombo vya habari, tungempata wapi.

Sasa hapa alipo, badala ya kukosoa kila siku kisa eti hakuna “slow motion” au imechelewa, au mpira unarushwa kwa kutumia kamera chache, au rangi haiko vizuri siku hiyo, au mchambuzi kababaika, haya ni mambo yanayowezekana kubadilishika.

Pamoja na kila kitu, hapa walipofikia Azam TV, wanastahili kupigiwa makofi ya pongezi angalau kidogo kuliko kuendelea kulalamika tu kwa kila jambo ambalo wanafanya.

Tuangalie nasi kama wanadamu tunakosea sehemu ngapi. Tukubali hata kama ni biashara lakini faida kwa nchi yetu kupitia michezo na mambo mengine inaonekana.

Kwa kuwa ndiyo wako mwanzoni, kadiri wanavyosonga mbele watakuwa na nafasi ya kujitolea na kufanikisha zaidi au kubuni yenye faida zaidi. Tuwape pongezi na tusihofie kuwakosoa kwa nia ya kujenga.

Kumbuka Azam haohao pia wanawekeza katika michezo kama udhamini wao huo ambao fedha zake zinaingia michezo na usisahau wadhamini wachache waliokuwa tayari kuwekeza mabilioni kama hayo michezoni maana kumekuwa hakuaminiki.




1 COMMENTS:

  1. INAWEZEKANA HUU NDIO ULIKUWA UJUMBE WAKO KATIKA HILI....:
    Sasa hapa alipo, badala ya kukosoa kila siku kisa eti hakuna “slow motion” au imechelewa, au mpira unarushwa kwa kutumia kamera chache, au rangi haiko vizuri siku hiyo, au mchambuzi kababaika, haya ni mambo yanayowezekana kubadilishika.

    Nshukuru.....Ngoja nirudi kwangu.
    Ili ufanye vizuri ni lazima upate kasoro yaani ukosolewe..mambo yako yataenda sawa. Ukitaka kusifiwa kila siku utashindwa kufanikiwa. Umeona ulivyoikosoa taarifa ya Kocha wa Simba kulipwa 42,000/- kwa sekunde basi ndio hivyo na wengine lazima wakosoe. Wengi wa sisi watanzania tunapendwa sana kusifiwa ndio maana upo tayar kuninunulia soda kwa kuwa nimekusifia...Unakumbuka kwenye mziki wa Dansi pale Mango Garden????basi ndio watanzania tunapenda hivyo kutajwa majina na kusifiwa. Ukikosolewa unarusha ngumi.

    Azam wamepelenda mapinduzi katika mfumo wa Televisheni Tanzania na kuongeza chachu ya ushindani wa kibiashara. Hakuna steseheni yoyote ya TV ambayo ina muundo mzuri wa upashaji wa habari kama Azam (Kwa muono wangu)..ila makosa wanayo.

    Kosa 1: Unaweza unga kifurushi kwa mfumo wa kubadilisha kifurushi...labda utaambiwa cha 7000 kwa wiki lakini matokeo yake itakulazimu uwapigie ili wakuunganishie. Sasa hapa je kama huna uwezo wa kupiga unafanyaje.

    Kosa 2: Ufinyu wa eneo la kurusha vipindi na ubunifu. Hili ni jambo ninaloliona. Tumekosa ubunifu katika urushaji wa vipindi. Mandhari ya eneo la kipindi yaendane na kipindi chenyewe. Taarifa ya habari eneo hilo na madhari hayo, michezo eneo hilo na madhari hayo hayo. Embu kama michezo tuweke eneo linaloendana katika mfumo wa kimichezo. Mimi napenda watu wa Citizen Kenya utaona michezo eneo lake linavyowekwa. Tujifunze.

    Kosa 3: Uwanjani....mara ya kwanza kabla hatujaanza kufanya kazi kwa mazoea tulikuwa tunafaida sana sisi watu wa majumbani. Kila kona ya uwanja tulikuwa tunaiona lakini sasa tunasubili sana. Sijui wale wafanyakazi wa mara ya kwanza wameondolewa au sijui wapo na wanafanya kazi kwa mazoea???!!!

    Kosa la 4: Kwanza Yanga na Simba ndio timu zinazosababisha hata ving'amuzi vya Azam Media Group vikapata wateja wa kutosha hadi vijijini. Watu wanataka kuwaona wachezaji na timu zao. Nilitegemea leo hii pale Bukoba mechi ya Simba isioneshe Live kwenye TV kwa watu wa Bukoba tu. Hii itasaidia sana washabiki wengi kwenda uwanjani.

    MWISHO:
    Tuvisaidie hivi vilabu vyetu kongwe Simba na Yanga katika hili. Na waandishi wa habari lazima tuweze kulisimamia ili Azam TV waweze kulifanyia kazi. Sehemu simba na Yanga zinapochezwa tunaomba channel husika isioneshe ili watu waende uwanjani. Kama inafanyika Singida basi mechi hiyo isioneshe Singida ila maeneo mengine waoneshe.

    Tunaomba Waziri wa Michezo aangalie hili na aweze kuongea na wahusika maana ni zuri kwa ubunifu na litasaidia kuongeza washabiki uwanjani. Pia hivi vilabu nje ya mkataba unaoingiwa na TFF katika haki ya matengenezo nao waweze kupewa fursa ya kukaa na Azam TV kujua ni jinsi gani ya kuboresha OFA yao.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic