MSEJA |
Kitendo cha mlinda mlango wa Simba, Emmanuel Mseja, kuitumia jezi namba 30 iliyokuwa ikivaliwa na kiungo wa zamani wa timu hiyo, marehemu Patrick Mutesa Mafisango, kimeelezwa ndiyo sababu ya yeye kushindwa kufanya vizuri kikosini hapo.
Mseja aliyejiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Mbao FC, amekuwa hana nafasi kikosini hapo baada ya kushindwa kuitumikia timu hiyo kwenye mechi 12 za Ligi Kuu Bara ambazo Simba imeshacheza mpaka sasa pamoja na mechi moja ya Kombe la FA.
Kipa huyo ambaye anatajwa ni chipukizi, amefanikiwa kudaka mechi nne pekee za Kombe la Mapinduzi ambalo Simba imeondolewa hatua ya makundi. Katika mechi hizo, Mseja amefungwa mabao manne, huku timu hiyo nayo ikifunga mabao manne.
Ikumbukwe kuwa, Mafisango raia wa Rwanda mwenye asili ya DR Congo, alifariki dunia Mei 17, 2012, jijini Dar es Salaam baada ya kupata ajali ambapo wakati wa kuagwa kwa mwili wake kwenye Viwanja vya Sigara, Chang’ombe, Dar, aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo kwa wakati huo, Ismail Aden Rage alisema uongozi wa Simba umekubaliana kutoitumia jezi namba 30 iliyokuwa ikitumiwa na kiungo huyo ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu yake.
“Mseja amefungwa mabao rahisi sana katika michuano ya Mapinduzi na eye ndiyo sababu kubwa ya timu kuondolewa mapema, mpaka sasa hajaonyesha uwezo wowote ndiyo maana hata kwenye ligi hachezi, hapa kapewa nafasi anashindwa kuitumia.
“Inawezekana ile jezi nayo inachangia kwa sababu kama unakumbuka ilikuwa ikitumiwa na marehemu Mafisango na wakati anaagwa, Rage alisema haitatumika tena, sasa inatumiwa na Mseja, hapa kuna tatizo.”
0 COMMENTS:
Post a Comment