Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina amerejea Bongo kimyakimya na jana alitarajiwa kwenda Zanzibar kuungana na timu kabla ya leo haijapambana na URA katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, imeelezwa.
Lwandamina ambaye aliondoka nchini mwishoni mwa mwaka jana baada ya kupata matatizo ya kifamilia, alirejea nchini juzi Jumatatu kuja kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho kilichopania kuwa bingwa wa michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.
Licha ya Lwandamina kurejea nchini, lakini viongozi wa Yanga wamekuwa wakificha na kukataa kabisa kuzungumzia ishu hiyo, lakini chanzo kimethibitisha hilo.
“Kocha amerejea jana (juzi Jumatatu) na leo (jana Jumanne), anatarajia kwenda Zanzibar kuungana na timu na kuna uwezekano akakaa kwenye benchi katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya URA au akaamua kumuachia Nsajigwa (Shadrack) amalizie michuano hiyo ili apate uzoefu,” kilisema chanzo.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten kuzungumzia hilo, alisema: “Muda wowote ataungana na timu.”
Alipotafutwa Lwandamina, alipopatikana alisema: “Nitarudi muda wowote kuanzia sasa, siwezi kuzungumzia mechi yetu na URA kwa sababu michuano yenyewe sijaifuatilia hata kwenye TV, hivyo siwezi kuzungumzia lolote kwenye hilo.”
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment