NA SALEH ALLY
KAMA utakuwa umewahi kusoma makala zangu, basi suala la kuhusiana na wachezaji kulipwa wanachodai kutoka kwa viongozi wa klabu, basi utakuwa unajua msimamo wangu.
Ingawa naweza kuitumia nafasi hii kidogo kukumbushana kwamba ninaamini hivi, ni sahihi kabisa mchezaji kusisitiza alipwe haki yake kwa mwajiri inapotakiwa.
Ni haki kwa mchezaji pia kushinikiza alipwe kama anaona kumekuwa na ugumu ingawa ni jambo zuri pia kuangalia na maslahi ya klabu ambayo ndiyo mwajiri wake.
Klabu kama itakuwa na majukumu, basi mchezaji anaweza kupima msaada wake kwamba hali ikoje, kuondoka kwake itakuwaje na kadhalika. Haya yote yanaweza kuwa mambo ya kibinadamu yatakayoongozwa na busara ya mtu.
Hivi karibuni, mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa aliomba ruhusa kwenda kwao Zambia kwa masuala ya kifamilia. Baada ya siku za kubaki Zambia kwisha, Chirwa akagoma kurudi akisisitiza kulipwa fedha zake za usajili anazoidai klabu.
Chirwa alionyesha kuwa hakuwa na utani na hilo jambo baada ya kuanza kutuma picha mitandaoni akiwa ‘bize’ na kilimo. Huu ulikuwa ni ujumbe kwa Yanga kwamba asingekuwa na utani hata kidogo kama asingelipwa kwa kuwa ana uwezo wa kuendesha maisha yake kupitia kilimo.
Baada ya msimamo wa Chirwa, Yanga iliona lingekuwa ni jambo zuri kumalizana naye. Hivyo mwisho Chirwa amerejea na kuungana na Yanga ikiwa Zanzibar katika michuano ya Kombe la Mapinduzi ambako alibeba lawama za kuing’oa mashindanoni.
Yanga walianza kulificha kwa juhudi kubwa suala la Chirwa kwa kuwa hawakutaka kuionyesha jamii ya Wanayanga kwamba kulikuwa na tatizo. Kukawa na hadithi nyingi kuhusiana na kutorejea kwake, mwisho ukweli ukasimama.
Sasa Chirwa amerejea, hakuna kiongozi wa Yanga anayeweza kusema alikuwa anadai kiasi gani na wamemlipa kiasi kipi lakini ukweli utaendelea kusimama kwamba hadi amerejea basi hakuna mjadala atakuwa amelipwa deni lake lote au amepunguziwa kiasi fulani kwa makubaliano fulani hivi.
Sasa kama ni hivyo, Yanga watakuwa wamefanya jambo zuri kwa kuwa kutimiza haki za msingi za wachezaji wao ni jambo bora kwa kuwa watumishi hao pia wanapaswa kuwa na furaha ili waifurahie kazi yao na mwisho kuiwakilisha klabu yao kwa juhudi na maarifa.
Sasa, anadai kipa Beno Kakolanya ambaye pia yuko katika mgomo baridi kama ambao alikuwa nao Chirwa naye akishinikizwa kulipwa fedha zake, jambo ambalo viongozi wa Yanga wanalijua.
Kweli sisi ni wanadamu na sote tuna matatizo na hadi Kakolanya amefikia kugoma au kushinikiza basi kutakuwa na tatizo yaani amefikia uamuzi huo baada ya kujaribu kiasi fulani na kuona mambo hayawezekani.
Kama Chirwa alilipwa, kwa nini Kakolanya asilipwe? Nafikiri uongozi wa Yanga unaweza kuziepuka zile hisia za huyu muhimu kuliko yule au zile za wachezaji wa kigeni wanapewa heshima kubwa kuliko wale wa nyumbani.
Zinaweza kuwa na ukweli ndani yake au la, lakini Yanga haiwezi kushindwana na kipa huyo hasa kama uongozi utaamua kumlipa angalau kiasi fulani na mwisho kufanya naye mazungumzo naye.
Msisitizo ni kwamba, lazima mkumbuke hawa wachezaji nao ni wanadamu na wanapishana hadi makuzi.
Wanapodai haki zao huenda wanakuwa wamebanwa na majukumu ingawa nasisitiza tena, hata wao wanapaswa kuwaangalia viongozi wao kama wanadamu pia na ikiwezekana busara iwe na nguvu zaidi.
Mwisho, niusisitize uongozi wa Yanga kuwapa wachezaji pia kipaumbele na ikiwezekana matatizo kama ya Chirwa na Kakolanya, yanaweza kutatuliwa kwa kauli nzuri na malipo kidogokidogo kabla ya kufikia hapo maana Yanga pia inatia hofu kama yataendelea kila baada ya siku kadhaa.
Upo sahihi kabisa. Wachezaji walipwe haki zao bila ya kubagua. Kwanza huyu Kakonyola atakuwa ana madai madogo ni rahisi kumalizana nae kuliko haya madai makubwa ya wachezaji wa nje.
ReplyDelete