Kikosi tajiri zaidi kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambayo uwanja wake umepitishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Azam FC, leo Jumamosi usiku inacheza fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya URA ya Uganda mjini hapa.
Mechi hiyo inayopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku wadau wengi wakiipa Azam nafasi kubwa ya kubeba ndoo kutokana na uwezo ulioonyeshwa na timu hizo tangu kuanza kwa michuano hiyo Desemba 29, mwaka jana.
Azam ilitinga fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuitoa Singida United, huku URA ikitangulia kuitoa Yanga.
Kocha wa Azam, Aristica Cioaba raia wa Romania, amesema kwamba hawatakubali kufungwa tena na URA.
“Tulikutana na URA katika hatua ya makundi na wakatufunga bao 1-0, lakini safari hii tumejipanga vizuri, ninaamini tutaibuka mabingwa wa michuano hii kwa mara nyingine tena.”
Naye Kocha wa URA, Nkata Paul amesema yupo tayari kwa lolote litakalotokea katika mechi hiyo lakini lengo lake kubwa ni kuiona timu yake hiyo ikiibuka na ushindi.
Azam ikitwaa ubingwa itakuwa mara ya nne kwao kufanya hivyo, lakini kama URA ikitwaa ubingwa hiyo itakuwa mara ya pili kwao.
0 COMMENTS:
Post a Comment