January 15, 2018




Na Saleh Ally
MSIMU huu, mshambuliaji John Raphael Bocco amejiunga na Simba akitokea Azam FC. Uamuzi wake ulielezwa kubeba mambo kadhaa kama mabadiliko, changamoto mpya na kadhalika.

Lakini kikubwa tulielezwa Bocco hakutaka dharau kwa kuwa Azam FC ilikuwa imeingia katika utaratibu mpya wa kupunguza gharama. Hivyo wakati wa usajili, mambo hayakuwa kama zamani na yeye akaona anaweza kuondoka.

Kutua kwake Simba kulikuwa gumzo na sasa kumekuwa gumzo zaidi baada ya masuala kadhaa kujitokeza likiwemo lile la Azam FC kuendelea kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara na juzi, imefanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.



Kinachoshangaza sana kwa wapenda mpira wengi sehemu mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania, kuhama huonekana ni kama uadui, kukosea au kukomoana.

Sasa inaonekana kama Azam FC ilifanya vizuri kumtoa Bocco, inaonekana Bocco ni kama alikosea Simba na huenda akafeli. Hata baada ya Azam kuchukua Kombe la Mapinduzi, mijadala imekuwa Bocco na wenzake kama Aishi Manula, Erasto Nyoni na kadhalika kwamba wameondoka na ubingwa umepatikana.

Leo tujikite kwa Bocco ambaye huenda Watanzania wameshindwa kuitambua kazi yake alikotoka na hadi sasa. Jambo ambalo linaonyesha wengi huzungumza bila ya kujikumbusha angalau kidogo.

Angalia katika kikosi cha Simba ambacho wengi wanalalamikiwa kutocheza kwa kujituma, hapa napo unaweza kuiona tofauti ya Bocco kwamba ni mchezaji anayetaka kitu fulani na hakiwezi kuwa tofauti na mafanikio.

Nchi pekee ambayo watu wanaweza kuambukizwa lawama ni Tanzania. Maana kila mmoja analaumu hata asiyekuwa na hoja ya msingi, ili mradi kasikia mwingine analalamika.

Bocco amekuwa akiifanya kazi yake kwa juhudi na hauwezi kumuweka katika kundi la watu wanaojituma bila ya majibu yenye mafanikio.

Tangu ametua Simba, Bocco amecheza mechi 10 za Ligi Kuu Bara, tayari amepachika mabao manne.  Alikosa mechi mbili tu za ligi hiyo Simba ikiivaa Njombe Mji na Ruvu Shooting. Amecheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya African Lyon na KMC na ana mabao manne. Ana bao moja katika mechi ya Kombe la Shirikisho na mechi tatu za Kombe la Mapinduzi akiwa na bao moja pia.

Katika mechi zote, Bocco kafunga katika ligi kuu, kirafiki, Kombe la Shirikisho na Kombe la Mapinduzi. Huyu ndiye mtu ambaye baadhi wanaamini Simba imekosea kumsajili kwa kuwa anakuwa majeruhi sana au tayari amebandikwa ule “uzee” uliowamaliza wachezaji wengi sana wa Tanzania.


Huyu Bocco, huenda ni mshambuliaji mzalendo ambaye timu nyingi sana za Tanzania zikiwemo Simba na Yanga hazikuwahi kuwa naye.

Akiwa na Azam FC ambayo si Simba wala Yanga na bado haijawa timu kongwe kama ambavyo wengi wanataka iwe sasa, aliiwezesha kubeba makombe lukuki, naye akashinda mataji mengi binafsi.



Ulitaka Bocco abaki Azam FC ili achukue nini? Ubingwa wa Afrika? Kama unaona amekosea kuondoka Simba, basi yanaweza kuwa mawazo yako lakini vizuri pia ukaanika hoja zako ukiwa na takwimu.

Bocco amewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiwa na Azam FC, akabeba ubingwa Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na timu hiyo aliyopanda nayo daraja.

Acha hivyo, ameiwezesha kubeba Ngao ya Jamii, leo Azam FC wanafurahia ubingwa wa Mapinduzi na wengine wanamzodoa Bocco lakini wanasahau ndiye nahodha wa kwanza wa Azam FC kubeba ubingwa huo, tena alikabidhiwa na huyohuyo Rais wa Zanzibar, Ali Mohammed Shein.
 


Kama tuzo za mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara wa mwezi pia Bocco amebeba zaidi ya mara mbili. Huyu mtu bado unaona amekosea kuhama Azam FC?

Nakukumbusha, wakati Azam FC inabeba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Bocco ndiye alikuwa nahodha wa kikosi. Sasa unataka abaki Azam FC na hasa kama anaona si sahihi akiwa anasubiri nini?

Siku Kocha Joseph Omog alipomtoa Shiza Kichuya, nafasi yake ikachukuliwa na John Bocco na mashabiki wa Simba wakaanza kulalama wakiona hana msaada, dakika chache akafunga bao la kwenye “kideo” na kuwafunga midomo, huenda ingekuwa siku nzuri ya kuanza kubadilika na kuamini kilicho sahihi.



Waungwana msimdharau Bocco kwa kuwa ni Mtanzania na kwa kipindi cha miongo miwili, inaonyesha ndiye mchezaji mwenye mafanikio zaidi hapa nchini akiwa hachezi Yanga au Simba.

Angalia rekodi uone kama kuna mchezaji aliwahi kuipandisha timu, akabaki nayo ligi kuu hadi kuipa ubingwa, akaipa ubingwa wa Kombe la Afrika Mashariki na Kati na Ngao ya Jamii na kadhalika. Hutapata zaidi ya Bocco ambaye, anapaswa apewe heshima yake.

Tukubali Bocco naye ni mwanadamu, hivyo kwa mnayoyasema, basi yafanyieni uchunguzi na kwa mchezaji mwenye mafanikio au anayejituma uwanjani, hauhitaji kuwa na darubini.

Jifunzeni kuthamini juhudi za wenzenu, jifunzeni kuwapa moyo wenzenu. Lakini mkumbuke pia kuwathamini wachezaji Watanzania bila kujali wanacheza timu ipi ni jambo jema na kama kukosoa iwe ya kujenga badala ya kukatisha tamaa tu.



Vipi hamumjui John? Nawakumbusha naye ni mwanadamu na hawezi kupatia kila siku na kama kupatia ndiyo kipimo bora pekee, basi angalieni na aliyoyafanya, wangapi unawaona bora hawajafanya kama yeye hadi hii leo wawe wa ndani na hata nje?


SOURCE: CHAMPIONI


3 COMMENTS:

  1. Ni kweli John Bocco ni bonge la mpambanaji ndio maana Simba wamempa heshima ya kuwa Captain wa timu. Ndani ya Simba anaheshimika. Niseme kwa sasa Bocco anastahili kuitwa kwenye timu yetu ya taifa. Ila nimesikitika alivyochezewa vibaya zanzibar kwenye kombe la Mapinduzi na timu ya Zanzibar beki yule akawa anamkumbatia mieleka na kudondoka nae chini lakini refa hakukemea wala kutoa kadi na waandishi wa habari wamekaa kimya. Hii sio sawa. Bocco angeweza kuumia kwa mchezo ule wa mieleka.

    ReplyDelete
  2. Brother umetumia maneno mengi kumsifia John Boko sikatai kuwa si kijana mwenye jitihada lakini bado John Boko anakosa vitu vingi amabavyo vingeweza kumjengea heshima zaidi kama mshambuliaji mahiri. Nilikuwa naangalia mechi ya ubingwa wa ulaya siku moja. Nakumbuka ilikuwa Real vs Buyern Munich kama sikosei. Na mtanagazaji akaendelea kuisifia Buyern hasa winga wake machachari Mholanzi Ruben ma wakali wengine kama Libbery nakadhalika..mtanagazaji akasema hii ni big match na matokeo ya mechi kama hii mara nyingi itategea zaidi umahiri wa watumbukizaji wa mabao wa pande zote mbili kwa sababu the best Diffence of any team is the Best offence. Mchezo ukaanza mara... pa .Ronaldo akafanya yake akatumbukiza mpira golini kama sikosei akatumbukiza na tena. Mara mtanagazaji akasema naam Fowadi wa ukweli ni yule aneisadia timu yake katika mechi ambazo zitaamua hatima ya timu yake kuendelea katika ushiki wa mashindano fulani na Ronaldo siku zote amekuwa akifanya hivyo kwa Madrid pengime hata kwa nchi yake he always been a game changer . Mtangazaji akaendelea kusema nanukuu kwa kigeni Ronaldo has been always shining in a big momentum this and that is to prove he is a big player and special for his team. Sitaki kumfananisha John Boko na Cristiano Ronaldo lakini wana majukumu yanayofanana John Boko anatakiwa kuthibitisha ubora wake katika mechi ambazo zitaamua hatima ya ushiriki wa Timu yake katika mashindano fulani ili kuthibitisha kuwa yeye ni mchezaji wa levo tofauti ni athibitishe kuwa ni mchezaji anaweza kutoa maamuzi ya mechi hasa ya ushindi katika mechi ya maamuzi (a game changer) na akifikia hapo basi simu kutoka vilabu kama mazembe, Orlando, zamaleki vitathibitisha ubora wake, lakin isio just lalala nyingi za magazeti na mitandao ya kijamii. Na sitaki kumtwisha John Boko zigo la lawama la kuondolewa kwa Simba kwenye mashindano yaliopita katika mechi ambazo zilihitaji mchezaji mwenye uwezo wa kuamua matokeo ya mechi kwa upande we Simba ku step up na kufanya vitu vyake lakini Simba ilimkosa mtu huyo licha yakuwa na kikosi kipana na cha gharama na John Boko ni miongoni mwa kikosi hicho.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Unapoyatazama mafanikio ya timu usimuangalie mchezaji mmoja,ukimfanya boco kuwa ndiye matokeo,utawaweka wapi wengine waliocheza chini ya kiwango?apewe heshima yake tu.

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic