January 19, 2018

AFRICAN LYON ILIPOKUWA LIGI KUU BARA

NA SALEH ALLY
KINACHOCHEKESHA ni kwamba kumekuwa na nguvu nyingi inatumika kusema katika Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, kuna dhuluma kubwa miongoni mwa timu.

Lakini pia kuna nguvu kubwa inatumika kuonyesha hakika hakuna dhuluma hata kidogo na mbaya zaidi, wapo wanaotaka kuonyesha wanaodhulumu ni wale na wala siyo wao.

Hili ni tatizo na kinachoonekana kila mmoja anajaribu kujisafisha huku akijua kweli kuna tatizo katika Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

Kwa hali ilivyo, baadhi ya matukio kupitia mashuhuda wakiwemo waandishi wa habari kumekuwa na mambo mengi ya kijinga yanaendelea na yanayoonyesha wazi kwamba kuna timu zitapanda ligi kuu kwa nguvu ya fitna badala ya uwezo.
Ligi hiyo imegeuka kuwa kichaka cha maovu, wale ambao wana nafasi ya kutumia nguvu ya ziada kama majina ya viongozi au nguvu ya kitu fulani, mfano wao ni timu ya jeshi, basi lazima washinde.

Wapo wanaoshinda si kwa mpira wao mzuri au wa uhakika, badala yake wanalazimisha kushinda kwa kuwa tayari ni kampeni ya mkoa kuangalia Ligi Kuu Bara na wanajua ili wafanikiwe hilo lazima wawe na timu ambayo wameipandisha.

Hivyo, timu kupanda inakuwa ni kampeni ya mkoa na bahati mbaya mkoa hauangalii ubora wa soka pekee, badala yake unaingia hadi katika fitina zinazoweza kuitwa upuuzi au dhuluma ili kuipambania timu yao kwa hali na mali ikiwa kwa dhuluma na vyovyote vile.

Msikatae kama ukweli uko wazi kwamba dhuluma imetawala katika mechi nyingi za Ligi Daraja la Kwanza na viongozi wanalijua hilo ingawa wamekuwa wakijikausha huenda wanaona ni tatizo linalohitaji nguvu nyingi sana kulishughulikia.

Nimeona Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliamua kutoa taarifa ambayo inakemea mambo yanavyokwenda katika Ligi Darala la Kwanza Tanzania Bara.

Kama TFF wamefikia kutoa taarifa, maana yake hata wao wanakiri kuna mambo hayaendi sawa na ndiyo maana wameamua kusimama na kukemea.

Kwangu naona kukemea pekee hakutoshi, badala yake viongozi wanapaswa kulivalia njuga suala hilo na kuhakikisha haki inatendeka angalau kwa mechi zilizobaki kabla ya ligi kwisha.

Tukubali, mechi hizo zitakuwa na shida zaidi kwa kuwa ligi yenyewe ndiyo inaenda ukiongoni ambako kuna nafasi kubwa ya watu kupanga matokeo kwa vile kwa hali ilivyo, mwishoni kutakuwa na ugumu wa juu hasa kwa timu zinazowania kupanda ligi kuu.

Katika kila kundi, mwishoni timu za juu zitakuwa na mvutano wa hali ya juu kabisa. Kwa kuwa kuna timu za mkoa, timu za majeshi, timu marafiki za viongozi wa juu TFF. Hii itachangia kuwe na mvurugano wa juu kabisa.

TFF iwe macho hasa, tena ikiwa na kumbukumbu ya msimu uliopita wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara ambayo iliisha kwa kashfa kubwa kabisa iliyosababisha hadi viongozi wa TFF kufikishwa mahakamani.

Wakati ule mambo hayakuwa yamelalamikiwa kwa kiwango kikubwa kama ilivyo sasa. Tuliona mwisho wake ukiwa ni wa aibu kubwa katika miaka ya mchezo wetu wa soka.

Leo karibu tokea mwanzo lawama hazijaisha. Kweli watu wanaweza wakawa wanalalamika tu lakini wingi wa malalamiko hayo unatulazimisha kuwakumbusha wahusika kulifanyia kazi jambo hilo angalau.

Kwamba wasidharau tu au wasikwamishwe na timu za taasisi, timu za mikoa au timu za marafiki wa viongozi wa shirikisho. Kikubwa kabisa ni haki na lazima itendeke.

 Kuendelea kusubiri timu zitakazopanda kwa msaada, mwisho ni kuifanya Ligi Kuu Bara kuwa na timu mpya dhaifu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic